Afrika katika Magazeti ya Ujerumani tarehe 16/17.04.2005
15 Aprili 2005Mojawapo kati ya majarida maarufu hapa Ujerumani ni DER SPIEGEL. Gazeti hili wiki hii limeandika makala isemayo: "Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo yaifikisha Uganda kwenye mahakama ya kimataifa kwa tuhuma za mauaji na wizi wa mali."
Wa-Kongo wamekuja juu sasa kwa madai kuwa, nchi ya jirani Uganda, zaidi ya kuendelea kuiba maliasili za Kongo, nchi hii inahusika pia na mauaji ya makumi ya maelfu ya wananchi wa Kongo.
Balozi wa Kongo Jacques Masangu-a-Mwanza wakati wa kufungua mashtaka haya, aliiambia mahakama ya Umoja wa Mataifa iliyo mjini Den Haag kwamba, Uganda inafanya uovu huu kwa kuwatumia viongozi wa makundi yanayopigana kwenye mkoa wa Ituri.
Itakumbukwa kuwa, vita vya wenyewe-kwa-wenyewe kati ya Wa-Hema na Wa-Lendu vilivyoanza mwaka 1999, mpaka sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 50,000. Hali kadhalika, zaidi ya watu 600,000 wamelazimika kuyakimimbia makazi yao.
Hata umoja wa mataifa unazituhumu Uganda na Rwanda kukiuka mkataba wa amani uliofikiwa miaka minne iliyopita baada ya vita kumalizika. Kwa kutokana na shinikizo kubwa la Umoja wa Mataifa, miaka miwili iliyopita, hatimaye Uganda iliafiki kuondoa askari wake 5,000 kutoka kwenye maeneo ya mashariki mwa Kongo.
Waziri wa sheria wa Kongo, Kisimba Ngoyi Ndalewe, amewataka mahakimu 15 wa mahakama ya kimataifa, kusitisha mara moja wizi wa maliasili unaofanywa na Uganda. Kupitia mahakama hii, Kongo inataka askari wote wa Uganda watoke nchini mwake, na inataka ilipwe fidia ya mauaji yaliyofanywa na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu.
Gazeti la DER SPIEGEL limemalizia kwa kuandika:
Mbali ya kesi hii, taasisi za mahamaka ya kimataifa ya makosa ya jinai zinachunguza uhalifu wa kivita uliofanywa wakati wa vita vya Kongo. Wakati mahakama hii inaweza kutoa hukumu kwa wahalifu moja kwa moja, mahakama ya Umoja wa mataifa ya Den Haag inashughulikia kesi baina ya nchi na nchi."
Gazeti la SÜDDEUTCHE ZEITUNG limeandika makala ndefu kuhusu ugonjwa hatari wa kuambukiza, homa ya Marburg, ulioibuka mara hii nchini Angola na kuua zaidi ya watu 173.
Kwa vile ugonjwa huu hatari, mara hii ulikuwa unasambaa kwa kasi, shirika la afya ulimwenguni, WHO, limependekeza taratibu za kufuata ili kukabiliana na tatizo hili.
Mkurugenzi mmoja wa shirika hili kwa upande wa mipango ya dharura, Mike Ryan, alisema, jambo muhimu kabisa kufanya baada ya mtu kupatwa na ugonjwa huu, ni kumtenganisha na wengine.
Idadi ya watu waliokufa kwa kutokana na ugonjwa huu unaofanana na Ebola, mara hii imekuwa kubwa mno. Mwanzoni watoto wa umri wa chini ya miaka 5 tu ndiyo walilkuwa wanaathirika na ugonjwa huu, lakini mara hii hata watu wazima wanapatwa na ugonjwa huu.
Mikakati ya Shirika la afya ulimwenguni kwa kushirikiana na wizara ya afya ya Angola pamoja na mashirika mengine imekuwa na mafanikio kwa vile idadi ya watu wanaoambukizwa na ugonjwa huu hivi sasa imepungua.
Ugonjwa wa homa ya Marburg hauna chanjo wala tiba. Virusi vya ugonjwa huu husambazwa kwa ute wa mwili wa binadamu."
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.
Kwa kumalizia makala hii ya udondozi wa "Afrika katika magazeti ya Ujerumani", tuangalie sasa kile kilichoandikwa kwenye gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG.
Chini ya kichwa cha habari, "Afrika yazidi kuzama kwenye umaskini", gazeti hili limechambua ripoti mpya ya shirika la fedha ulimwenguni na benki ya dunia.
Kwa kulingana na ripoti hii, bara la Afrika halina matumaini ya kutekeleza malengo ya umoja wa mataifa ya kupambana na umaskini.
Itakumbukwa kuwa, miaka mitano iliyopita, umoja wa mataifa uliazimia hadi kufikia mwaka 2015 kupunguza umaskini duniani kwa asilimia 50 na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia hata watu hohehahe duniani.
Kizungumkuti ni kuwa, ili kufikia malengo haya yaliyopitishwa na nchi 180 duniani kote, uchumi wa Afrika lazima ukue kwa kiwango cha mara dufu katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Jambo hili ni ndoto.
Ripoti ya mpya ya benki ya dunia na shirika la fedha ulimwenguni imebaini pia kwamba mpango huu unatekelezwa polepole mno na kwa viwango tofauti.
Wakati nchi za mashariki mwa Asia zinategemea kufikia malengo ya umoja wa mataifa, hususani kwa kuzingatia ukuaji wa uchumi wa Uchina na India, hakuna matumaini mazuri kwa bara la Afrika. Ripoti hii imesema, hali ikiendelea kuwa hivi, badi nchi za kusini mwa jangwa la Sahara hazitafikia malengo ya kupunguza umaskini kwa asilimia 50 miaka 10 ijayo.
Nchi 12 za Afrika ikiwa ni pamoja na Ghana, Mali, tanzania na Uganda, uchumi unastawi kwa zaidi ya asilimia 5.5. Lakini kwa ujumla bara la Afrika linaendelea kutokomea kwenye umaskini.
Kwa maelezo hayo ya gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG kuhusu ripoti mpya ya benki ya dunia na shirika la fedha duniani, ndiyo tunakamilisha makala hii ya "Afrika katika magazeti ya Ujerumani".