Afrika katika magazeti ya Ujerumani, tarehe 15.10.2005
14 Oktoba 2005Magazeti na majarida mengi ya Ujerumani hata wiki hii yameendelea kuandika na kuchambua wimbi la wakimbizi kutoka Afrika wanaotaka kuingia katika nchi za Ulaya.
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika juu ya mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuongeza msaada wa maendeleo kwa Afrika kwa lengo la kupunguza wimbi la wakimbizi.
„Tume ya Umoja wa Ulaya na jopo la mawaziri wa mambo ya ndani wamekubaliana kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika. Rais wa tume, MANUEL BARROSO, alipokuwa akiutambulisha mpango huu siku ya Jumatano, alisema: wimbi la wakimbizi wa Afrika lililofikia sasa hatua ya kutisha, linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa sera kabambe za pamoja za misaada ya maendeleo.
Kimsingi, Umoja wa Ulaya umepanga kuongeza misaada ya maendeleo kutoka kiasi cha Euro bilioni 17 mwaka 2003 hadi kufikia Euro bilioni 25 hapo mwaka 2010. Pia misaada ya moja kwa moja ya nchi wanachama inatarajiwa kuongezekam, miradi ya maendeleo itapitishwa kwa kushirikiana. Kipaumbele kitatolewa kwenye ujenzi wa barabara, reli na kuborehsa huduma za maji na nishati. Lengo ni kuongeza biashara ya ndani ya kontinenti la Afrika.
Umoja wa Ulaya ulitumia nafasi hii kusisitiza kuwa, asilimia 60 ya misaada ya maendeleo inayotoka katika nchi za viwanda, inatoka katika Umoja wa Ulaya, wakati Marekani inatoa asilimia 18 na Japani inatoa asilimia 2.
Naye rais wa Umoja wa Afrika, ALPHA OUMAR KONARE, aliwakumbusha wahusika kwamba, ujenzi wa kuta na jela katika nchi za kaskazini mwa Afrika, siyo suluhu ya tatizo la wakimbizi. Ni makosa kuliangalia tatizo hili kwa mtazamo wa kiusalama peke yake. Aliongezea kwa kusema na hapa namnukuu: „vijana hawa tunaowaona wamesimama kwenye uzio wa senyenge na kuta ndefu siyo wezi, siyo majambazi“. Aliyekuwa rais wa Mali, OUMAR KONARE alisema, kinachowafanya maelfu ya wafrika wakimbie makazi yao ni umaskini, tena umaskini ambao anasema umechangiwa sera za kilimo za Umoja wa Ulaya ambazo zinawanyima masoko wakulima wa Afrika.“
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU.
Kwenye tahariri ya gazeti la DIE TAGESZEITUNG – TAZ, mkakati wa Umoja wa Ulaya umechambuliwa kwa mtazamo mwingine:
„Wazo hilo ni zuri: Ulaya lazima iwe na mkakati wa kukaa pamoja na kontinenti jirani la Afrika. Mpaka sasa Ulaya ilikuwa haina mpango rasmi na ndiyo maana hali ya mambo inazidi kuwa mbaya. Mizozo ya Afrika inaweza kutatuliwa kwa ushirikiano wa kimataifa. Na hapa nchi za Ulaya zilizokuwa zinatawala kontinenti hili zina wajibu mkubwa zaidi wa kihistoria.
Mpango wa Umoja wa Ulaya wa kujenga njia za usafiri unanuia kufikisha kirahisi zaidi mazao ya Afrika katika nchi za nje na siyo wafanyakazi. Aidha kwa kufanya hivi wanatumai kukabiliana na tatizo la ukimbizi. Lakini wahusika wamesahau kuwa, hii ndiyo ilikuwa sera ya nchi za Ulaya wakati wa ukoloni, ambapo mkazo ulikuwa kuhakikisha malighafi za Afrika zinafika kirahisi kwenye masoko ya kimataifa. Lililopo ni kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya.“
Hayo ni maoni ya gazeti la TAZ.
Rais wa Ujerumani, Hörst Köhler, akiongea na gazeti la DIE ZEIT amesema, Ulaya inalihitaji kontinenti la Afrika hata kama kwa sasa linazongwa na matatizo mengi.
„Matatizo ya kontinenti jirani la Afrika, kama vile tatizo la watu kulazimika kuhama makazi yao, maradhi na uharibifu wa mazingira, yanaweza kutatuliwa kwa pamoja – hususani kwa ushirikiano wa makontinenti jirani ya Ulaya na Afrika.
Rais Köhler amenukuliwa akisema, „kama tunataka kuwa wakweli na kuonyesha utu wetu, hatuwezi kulisahau au kuliacha peke bara la Afrika.“
Alisema pia kuwa, Afrika inahitaji muda ili kusonga mbele kimaendeleo. Alisema, mataifa mengi yako huru tangu miaka 40 au 50 tu iliyopita, kufuatia historia mbaya ya utumwa na ukoloni. Kwa hiyo msingi wa kitamaduni wa nchi hizi ulivurugwa – kiasi kwamba hii leo chini ya mfumo wa utandawazi haziwezi kufanya miujiza. Aliongezea kwa kusema kwamba, watu wasisahau kwamba, Ulaya ilihitaji utulivu wa mamia ya miaka ili kujenga demokrasia na utawala wa kisheria.”