Afrika katika magazeti ya Ujerumani, tarehe 12-05-2006
12 Mei 2006Makampuni ya kompyuta duniani yamegundua umuhimu wa soko kubwa la bidhaa zao katika nchi zinazotumia lugha ya Kiswahili barani Afrika, na ndiyo maana makampuni ya Kompyuta kama vile Microsoft, yanatafsiri programu nyingi katika lugha ya Kiswahili.
Gazeti la Neue Züricher Zeitung limeandika:
„Kwa muda mrefu nchi za Afrika zilikuwa zinategemea lugha za Ulaya, lugha za makoloni yao, jambo ambalo linaweza kuchukuliwa kama kuendeleza mfumo wa kikoloni. Wasomi wa Afrika kama vile mwandishi maarufu wa vitabu wa Kenya, Ngugi wa Thiongo, walianza kuikemea tabia hii katika miaka ya 70. Tangiapo Ngugi anaandika vitabu vya katika lugha ya Kikuyu ili ujumbe wake uwafikie watu wengi zaidi. Hata hivyo mpaka sasa baadhi ya wasomi, wanasiasa na wazazi bado wanapuuzia lugha zao na ndiyo maana watoto wa mijini wanakua bila kujua lugha za wazazi wao.
Kwa upande mwingine jitihada za watu wachache kama Ngugi wa Thiongo na kushamiri kwa utandawazi zimezaa matunda: Mwezi wa Machi mwaka huu, kampuni kubwa la kimataifa la kompyuta Microsoft lilitangaza, litatoa hivi karibuni programu zote za matumizi ya ofisini pamoja na Operating System ya Windows XP katika lugha ya Kiswahili. Programu nyingine za vyanzio huria zinatolewa katika lugha ya Kiswahili tangu mwaka jana.“
Gazeti la Neue Züricher Zeitung limemaliza kwa kuandika:
„Hatimaye makampuni ya kimataifa ya Kompyuta yameng’amua kuna soko la kubwa bidhaa zao katika nchi zianazotumia Kiswahili, baadaye watashughulikia lugha za Hausa na Zulu.
Aidha siku hizi hata kwenye maeneo ya mbali vijijini, si jambo la kushangaza kupata huduma za Internet na Kompyuta. Mpaka sasa programu nyingi zinaweza kutumiwa na watu wachache tu waliobahatika kusoma kwenye shule nzuri za kulipia, kwani ni za Kiingereza tu.“
Hata wiki hii Sudan iliendelea kugonga vichwa vya habari kwenye magazeti ya Ujerumani. Baada ya mkataba wa amani, jumuiya ya kimataifa inayashinikiza zaidi makundi yote yanayopigana kuheshimu mkababa wa amani na kuruhusu kuletwa kwa kikosi cha kulinda amani.
Gazeti la DIE TAGESZEITUNG limeendelea kwa kuandika:
„Marekani inataka mpango wa kupeleka kikosi cha kulinda amani katika eneo la mzozo huko Darfur, magharibi mwa Sudan, utekelezwe haraka iwezekanavyo, ikibidi hata kwa kutumia vikosi vilivyo tayari kusini mwa nchi hiyo.
Mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika mjini Viena ulimalizika kwa azimio la kutaka „mazungumzo kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Sudan juu ya jukumu la Umoja huo katika eneo la Darfur“ yakamilishwe haraka.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Ulaya nchini Sudan, Peeka Haavisto, alisema, mkataba wa amani uliofikiwa ni wito pia kwa Umoja wa Mataifa kupeleka kikosi cha kulinda amani.“
Kwa kumalizia udondozi wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani, gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika makala ndefu kuhusu utalii barani Afrika.
„Maonyesho ya utalii ya Afrika Kusini – INDABA – mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa zaidi. Zaidi ya makampuni ya utalii 1,600 kutoka nchi mbalimbali yaliwakilishwa. Makampuni haya yanatoa huduma mbalimbali kama vile malazi, usafirishaji, uuzaji wa safari, hasa kwenye mbuga za wanyama na kadhalika.
Msemaji wa watayarishaji wa maonyesho hayo, Bi. Tholoana Qhobela, alisema idadi ya wageni pia iliongezeka kwa asilimia 25.
Kwa ujumla shughuli za utalii zinavuma katika nchi nyingi za Afrika na siyo tu Afrika Kusini ambayo mwaka jana ilipokea watalii milioni 7.3 Hadi kufikia mwaka 2010 kwenye michuano ya kombe la dunia la mpira, Afrika Kusini imepania kuwa inapokea zaidi ya watalii milioni 10 kwa mwaka.
Kenya imepania kuimarisha utalii wa utamaduni na ikolojia.
Nchi nyingi zinategemea utalii kwa ajili ya fedha za kigeni na ustawi wa uchumi. Afrika Kusini imetangaza inapata pesa nyingi kwenye utalii kuliko machimbo yote yaa madini; na inatarajia kutimiza malengo ya maendeleo ya Milenia kwa kutumia pato la utalii.