Afrika katika magazeti ya Ujerumani, tarehe 07-10-2005
7 Oktoba 2005Dunia nzima inaangalia kinachoendelea nchini Moroko, hasa kwenye eneo la mpaka wa ndani kati ya nchi hii na Hispania, ambako kila siku mamia ya wakimbizi kutoka Afrika, wanajaribu kuvuka mpaka na kuingia Ulaya.
Gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT limejishughulisha na sababu zilizopelekea kuzuka kwa wimbi hili la wakimbizi, kwa kuandika:
„Wakimbizi hawa wako Moroko, kwenye mpaka wa maeneo ya ndani ya Hispania MELILA na CEUTA, lakini wanatoka katika nchi mbalimbali za Afrika, wengine wamevuka hata jangwa la Sahara. Wanahangaika hivyo kwa lengo la kulitoroka kontinenti la Afrika, linaloelemewa na umaskini, njaa na hasa vita.
Kwa mujibu wa jumuiya ya utafiti wa vyanzio vya mizozo, hivi sasa barani Afrika kuna karibu vita vya silaha 16 kwenye nchi tofauti 53. Kwa kutathimi idadi hii, bara la Afrika linaongoza duniani kwa kuwa na mizozo mingi ya kivita. Kwa kutokana na vita hivyo, mwaka jana, zaidi ya watu milioni nne walilazimika kuhama makazi yao.
Huko Darfur – Sudan, takribani watu laki 3 wameuawa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Pia watu milioni mbili wamelazimika kuyahama makazi yao ili kutafuta chakula au kwa kukimbia wanamgambo wapanda farasi, janjawidi, wanaouwa watu ovyo na kuchoma nyumba za raia.
Nigeria nako, vita vya kugombania utajiri wa mafuta kwenye eneo la delta vinaendelea.Wanamgambo wa Ijaw wanapigana dhidi ya makampuni ya kigeni pamoja na majeshi ya serikali.
Mfano mwingine ni Kongo Kinshasa: Huko zaidi ya wakimbizi milioni 1.4 wameshindwa hata kupatiwa misaada ya kiutu kwa kutoka na vita. Hali si tafauti nchini Burundi, Uganda, Etihiopia na Ivory Coast.“
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT.
Kuhusu pia wimbi la wakimbizi wa Afrika kwenye mpaka wa Moroko na Hispania, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika makala ndefu hukusu mpango kabambe wa kulikwamua bara la Afrika kiuchumi.
„Hispania inaunga mkono wito wa Moroko wa msaada mkubwa wa kiuchumi kwa Afrika. Nchi hizi zinadai, mpango huu utapunguza wimbi la wakimbizi wa Afrika wanaotaka kuingia Ulaya ambao wengi wao wanatoka Ivory Coast na Niger.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Hispania, askari wa kulinda mpaka wa nchi hizo mbili wanashirikiana kuzuia mamia ya wakimbizi wanaojaribu kila mara kuvuta mpaka kwa nguvu.
Hali kadhalika wakimbizi wa Afrika walioingia kwenye maeneo ya Hispania kinyume cha sheria, wameanza kurudishwa Moroko. Mazungumzo yanaendelea kati ya Hispania na nchi nyingine za Afrika, mathalani Mali na Ghana.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Hispania, MORATINOS, aliyeomba msaada wa baraza la Ulaya na hapohapo kuunga mkono wito wa Moroko, amenukuliwa akisema, matatizo ya maeneo ya mpakani CEUTA na MELILA ni ya Ulaya nzima. Kwa hiyo kazi ya kudhibiti maeneo hayo ni ya nchi zote na siyo Hipania peke yake.“
Kwa kuhitimisha udondozi wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani, tuangalie makala ya kutia moyo iliyoandikwa kwenye gazeti la KÖLNER RUNDSCHAU juu ya mpango wa nchi za Afrika wa kupambana kikamilifu na tatizo la njaa.
„Alhamis iliyopita nchi za Afrika, kwa mara ya kwanza zilipitisha mpango wa miaka mitano wa kupambana kikamilifu na upungufu wa chakula katika kontineti zima.
Wawakilishi wa nchi 49 walishiriki kwenye kongamano hilo ambalo lililoandaliwa na shirika la chakula duniani FAO pamoja na shirika la Afya duniani WHO kwenye mji mkuu wa Zimbabwe mjini Harare. Nchi za Afrika zimekubaliana kuhimiza utafiti wa njia za kuongeza uzalishaji wa chakula, pia kupitisha sheria za kulinda watumiaji.
Sambamba na harakati hizo, kwenye kontinenti lote la Afrika kutaanzishwa mikakati ya kuboresha chakula.“