Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
24 Juni 2005Gazeti la DIE WELT lilizumngumzia juu ya matuamini makubwa ya mataifa ya Afrika kupata misaada kutoka kwa mataifa tajiri duniani. Hatua ya mataifa ya G8 kuyasamehe madeni ya mataifa maskini zaidi barani Afrika, ilikuwa ya kufurahisha na uamuzi uliokaribishwa na wengi. Lakini hata hivyo kutekelezwa kwa ahadi hiyo, ambayo bado imebakia makaratasini, ndio ngoma. Mataifa hayo yatabidi kusubiri hadi mkutano wa mataifa ya G8 utakaofanyika nchini Scotland kuanzia tarehe 6 hadi 8 mwezi ujao.
Sababu ya mkutano huo sio tu kuzungumza mpango wa Marshall Plan wa waziri wa fedha wa Uingereza bwana Gordon Brown, lakini pia ni kujadili hatua nyengine muhimu kuamua ni madeni gani yatakayofutwa. Mataifa 18 ya Afrika ambayo yamesamehewa madeni yao hulipa kiwango cha dola bilioni 1.5 kila mwaka kujaribu kupunguza madeni yao. Mwenye kubebwa hujikaza, Afrika inatakiwa kuongeza juhudi kujikwamua kutokana na umaskini.
Mada ya pili iliyozingatiwa na gazeti la DIE WELT ni kuachliwa huru kwa mateka sita wa rehani, wakiwemo raia wawili wa Ujerumani, nchini Nigeria. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni mjini Berlin, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alithibitisha kuachiliwa huru kwa mateka hao, bila masharti yoyote, baada ya juhudi nyingi kufanywa. Alizungumzia kuhusu ushirikiano na serikali ya Nigeria na kampuni la Shell.
Kundi la watekaji nyara la kabila la Iduwini lilitaka kulishinikiza kampuni la mafuta la Shell kutoa nafasi za ajira kwa raia wa eneo la Niger Delta na kudhamini miradi ya maendeleo. Msemaji wa serikali katika jimbo la Bayelsa, amesema mateka wote wako salama wasalmin, isipokuwa walionekana wakiwa na hofu kubwa.
Gazeti lilimalizia mada hii kwa kuandika kwamba mivutano kati ya kampuni la Shell na waakazi wa eneo la Niger Delta hutokea mara kwa mara. Kampuni hilo husafirisha mapipa milioni 2.3 ya mafuta yote yanayosafirishwa na muungano wa mataifa yanayosafirisha mafuta duniani, OPEC, lakini raia wa Niger Delta hawafaidi kutokana na utajiri huo wa mafuta.
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU lilikuwa na habari kuhusu hali ya wasiwasi nchini Nigeria kufuatia onyo lililotolewa na kundi la wanamgambo wakitaka kufanya mashambulio. Afisi za ubalozi wa Marekani, Uingereza na Ujerumani mjini Lagos, zilifungwa kwa siku kadhaa na kufunguliwa tena Jumatatu wiki hii, baada ya vitisho vya mashambulio kutolewa mjini Lagos.
Ilani hiyo ilitolewa baada ya Marekani na mataifa tisa ya Afrika, ikiwemo Nigeria, kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya majuma matatu katika eneo la Sahel. Wanajeshi 700 wa Marekani na 3,000 wa Afrika walishiriki katika mazoezi hayo.
Marekani ina wasiwasi kwamba magaidi hupitia eneo la Afrika Kakzini wakienda Irak. Katika eneo la kazkazini mwa Nigeria lililo na idadi kubwa ya waislamu, kuna wafuasi wa kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda, Osama bin Laden. Katika jimbo la Borno kuna kundi linalojiita taliban au Mujihajiru ambalo hushambulia vituo vya polisi.
Serikali imechukua hatua za dharura kujaribu kuzuia kutokea kwa mashambulio, ikiwemo kuwachunguza watu na magari yanayoingia katika maeneo muhimu na majumba makubwa yanayoweza kulengwa.
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linatumalizia makala haya na hali ya umaskini uliokithiri katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, licha ya kuwepo na utajiri mwingi nchini humo. Mji wa Busia katika mpaka wa Kenya na Uganda umetajirika na kuni na mbao zinazotoka wilaya ya Ituri nchini Congo kupitia Uganda.
Sio kiwango kikubwa lakini kinatosha kabisa kuwwawezesha raia wa Ituri kujenga nyumba zao na kununua magari kutokana na biashara ya mbao. Ukweli uliopo ni kwamba mataifa jirani na Congo ndio yanayofaidi sana kutokana na raslimilai za Congo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti kuhusu ´laana ya dhahabu, na kazi ya pamoja ya wauzaji wa madini hayo katika mataifa ya kigeni wakishirikiana na maongozi ya kikatili ya waasi wanaowalazimisha watu kufanya kazi ya kuchimba madini hayo. Ni ajabu kwamba jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ina utajiri mkubwa lakini haiutumii kuungamiza umaskini nchini humo. Ama kweli kozi mwana mandanda kulala na njaa kupenda.
Na kufikia hapo ndio nakamilisha Afrika katika mageti ya Ujerumani juma hili. Mimi ni Josephat Charo nawatakiwa wikendi njema.