Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
16 Desemba 2005Uchaguzi wa Tanzania uliofanyika Jumatano iliyopita, ulishuhudia chama tawala cha mapinduzi kikipigiwa kura na idadi kubwa ya watanzania.
Gazeti la Die Welt lilimtaja mgombea wadhifa wa urais kwa tiketi ya chama hicho, waziri wa mambo ya kigeni, mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa kipenzi cha watanzania hata kabla tume ya uchaguzi ya kitaifa nchini humo kutangaza rasmi matokeo kamili ya uchaguzi huo.
Bwana Kikwete alionekana mwenye afya nzuri alipopiga kura yake katika eneo la pwani, baada ya kuanguka jukwaani siku ya mwisho ya kampeni yake.
Huku uchaguzi ukifanyika kwa hali ya utulivu katika eneo la bara, machafuko yalizuka visiwani Zanzibar, ngome kuu ya upinzani. Katika kisiwa cha Unguja, wafuasi wa chama cha wananchi, CUF, waliwazuia wapiga kura walioletwa kutoka nje ya visiwa hivyo wasipige kura zao.
Gazeti lilimnukulu mgombea mmoja wa chama cha CUF akisema jeshi la serikali liliwapeleka wapiga kura bandia katika visiwa hivyo, jambo lililosababisha vijana wafuasi wa CUF kuchukua hatua ya kuwazuia wasipige kura. Mtu mmoja alipigwa risasi mguuni katika vurugu hizo, lilisema gazeti hilo.
Kuhusu mada hii gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema upinzani nchini Tanzania haukutarajiwa kuwa tisho kubwa kwa chama tawala cha CCM.
Mada ya pili ilihusu hatua ya Ethiopia kutangaza kwamba itawaondoa wanajeshi wake kutoka eneo la mpakani na Eritrea, ambalo limekuwa likilindwa na majeshi ya umoja wa mataifa kuzuia kutokea kwa vita kati ya mataifa hayo mawili. Hatua hii imeisababisha Ethiopia kulitolea wito baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Gazeti la Die Welt lilimnukulu waziri wa mambo ya kigeni wa Ethiopia, Seyoum Mesfin, akisema kwamba baraza hilo lijitikwe jukumu la kuchukua hatua zifaazo na kwa dharura iwapo Eritrea itaitumia hatua ya Ethiopia kuwaondoa wanajeshi wake kutoka mpakani na kuivamia nchi.
Baraza la usalama la umoja wa mataifa lilitishia kuziwekea vikwazo vya kiuchumi Ethiopia na Eritrea kama hazitayaondoa majeshi yao kutoka eneo hilo la mpakani.
Nalo gazeti la Frankfurter Rundschau kuhusu mada hii liliandika juu ya waeritrea kulalamika kuhusu hatua za kikatili zinazotumiwa kuwasajili wanajeshi wapya. Wanaume na wanawake wenye umri kati ya miaka 18 na 40 wanasajiliwa lakini hata pia watoto wadogo.
Shughuli hiyo huanza katika shule na mitihani ya mwisho hufanywa jeshini, ambayo matokeo yake humlazimisha mwanafunzi kufanya kazi kama mwanajeshi. Maofisa waliokimbia jeshini na wakimbizi wameripoti juu ya vitendo vya kinyama vinavyofanywa na jeshi, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa makurutu wanawake, kuwadhalilisha kama watumwa na kuwatumia kusaidia katika shughuli za ujenzi.
Gazeti la Frankfurter Rundschau linatukamilishia na matumaini ya raia wa Burundi katika siku za usoni. Maisha ya kijana wa Burundi, Mohammed Nyabenda, yalizunguziwa na gazeti hilo. Mohammed ni mmoja wa warundi waliokimbilia nchini Tanzania miaka 15 iliyoipita wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, vilivyowauwa watu takriban elfu 300.
Mohammed amenukuliwa akisema maisha yalikuwa magumu katika kambi za wakimbizi nchini Tanzania, lakini yalikuwa afadhali. Mwaka wa 2000 Mohammed alirudi Burundi na kupigana katika kundi la CNDD – FDD na anasema huo ndio uliokuwa mwanzo wa kuleta matumaini katika maisha ya warundi.
Sasa Mohammed ni mmoja kati ya wapiganaji wanaopokea msaada wa kuwajumulisha katika jamii, mradi ambao unadhaminiwa na benki kuu ya dunia. Waasi wa zamani wanapokea kiwango cha dola 600 za kimarekani na Mohammed amezitumia kununua ardhi na anajenga nyumba ya kuishi na mkewe. Warundi wanafanya kazi kwa bidii ya kujenga barabara huku wakipokea chakula kutoka kwa shirika la chakula duniani, WFP.