Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
3 Februari 2006Gazeti la Die Welt linatufungulia na ripoti ya kuachiliwa huru kwa mateka wa rehani wafanyikazi wa kampuni ya Shell waliokuwa wakizuiliwa na watekaji nyara wa kundi linalopigania umilikaji wa raslimali za eneo la Niger Delta nchini Nigeria. Lengo la utekaji nyara huo ni kupunguza umilikaji wa mafuta na makampuni ya kigeni kwa asilimia 30. Mzozo wa eneo la Delta umesababisha bei za mafuta kupanda.
Gazeti la Die Welt lilimnukulu mshauri wa usalama wa kampuni moja ya kigeni nchini Nigeria akisema huenda kukatokea tena visa vingine vya utekaji nyara. Nigeria ni mojawapo ya nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani, lakini wanigeria wengi katika maeneo yenye mafuta bado wanaendelea kuishi katika umaskini uliokithiri.
Likitubadilishia mada gazeti la Die Welt liliripoti juu ya hatua ya Kenya kukataa chakula cha mbwa kilichotolewa na kampuni ya Uholanzi kama msaada kwa watoto wa Kenya wanaoteseka kwa njaa. Mkurugenzi wa kampuni ya Mighty Mix, Christine Drummond, alitaka kutuma tani 42 za chakula hicho kwenda Kenya akisema kina virutubishi muhimu kwa watoto na ni kitamu.
Msemaji wa serikali nchini Kenya lakini amenukuliwa na gazeti la Die Welt akisema hali ya njaa haijafikia kiwango cha watoto kula chakula cha mbwa. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, wakenya takriban milioni 3.5 wanakabiliwa na njaa.
Tukiondoka nchini Kenya tuelekee nchini jamhuri ya kideomokrasi ya Kongo. Gazeti la Die Welt lilizungumzia juu ya vurugu zinazoendelea katika eneo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Wakongomani elfu 80 wamelazimika kuyahama makazi yao na kukimbilia maeneo yaliyo salama kutokana na mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Josef Jung anapinga kupelekwa kwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Ujerumani kwenda jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kujiunga na kikosi cha umoja wa mataifa kulinda usalama wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu.
Waziri Jung amenukuliwa na gazeti la Die Welt akisema Ujerumani haiwezi kuwatuma wanajeshi wake kila mahali ulimwenguni. Kufuatia hatua ya umoja wa Ulaya kusisitiza kwamba ni muhimu umoja huo upeleke wanajeshi wake nchini Kongo, Ujerumani ina jukumu la kuamua kuhusu swala hilo.
Licha ya kuwepo kwa wanajeshi elfu 17 wa tume ya amani ya umoja wa mataifa, MONUC, katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, machafuko bado yanaendelea katika mkoa wa Kivu kazkazini. Haijabainika wazi mpaka sasa ikiwa umoja wa Ulaya utapeleka wanajeshi wake kwenda nchini humo.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatupeleka mjini Cairo Misri ambako watalii 14 kutoka Hong Kong walifariki dunia katika ajali ya basi walilokuwa wakisafiria kusini mashariki mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa shirika la habari la Mena nchini Misri, watalii wengine 30 walijeruhiwa vibaya wakati basi hilo lilipobingiria mara kadhaa. Basi hilo lilikuwa na abiria 44 kutoka mji wa pwani wa Hurghada katika bahari nyekundu likielekea mji wa Luxor.
Manusura wa ajali hiyo walisema basi hilo lilikuwa likienda kwa kasi ya kilomita 150 kwa saa. Barabara mbaya na ulegevu wa askari wa barabarani kuangalia kasi za magari ni sababu zinazochangia ajali za barabarani nchini Misri.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatukamilishia na kuridhishwa kwa chama cha wandungu waislamu, Islamic Brotherhood, nchini Misri juu ya ushindi wa kundi la Hamas katika uchaguzi wa bunge nchini Palestina. Ushindi wa Hamas unadhihirisha wazi kutoridhisha kwa utawala wa kiimla katika mashariki ya kati.
Msomi wa Misri, Usama Ghazali Harb, amenukuliwa na gazeti hilo akisema ushindi wa Hamas unatakiwa kutizwámwa kwa karibu katika mataifa ya kiarabu. Ikiwa kundi hilo litaunda serikali, linaweza kuushangaza ulimwengu kwa kuendeleza demokrasia katika mashariki ya kati kinyume cha vile inavyotarajiwa.