Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
3 Machi 2006Gazeti la Frankfurter Allgemeine limekutaja kuchaguliwa tena kwa rais Yoweri Museveni kama mfano mbaya kabisa wa kisiasa barani Afrika. Ni kama ufunguo kwa mataifa mengine kubadili katiba ili kuongeza awamu za utawala wa rais. Chad tayari imeshafanya hivyo na sasa inakisiwa Nigeria huenda nayo ikafanya hivyo.
Rais Museveni mwenyewe alisema miaka 20 iliyopita kwamba tatizo kubwa barani Afrika ni viongozi wasiotaka kubanduka madarakani lakini sasa yeye mwenyewe amejikuta katika mtego huo. Wanaomuunga mkono rais Museveni wanamtaka aendelee kutawala eti aweze kuisimamia nchi wakati huu wa vyama vingi vya kisiasa. Lakini gazeti linasema hizo ni porojo kwani kama mpaka sasa hakuna mfumo mzuri wa vyama ulioweza kudumishwa, bila shaka Museveni hataweza kwani yeye mwenyewe ndiye kipingamizi.
Gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema ni kawaida kwa viongozi wa Afrika kutaka kubakia madarakani mpaka wafariki dunia wakiwa bado wanatawala na kama ingewezekana wangeendelea kutawala hata wakiwa kaburini.
Likitubadilishia mada gazeti la Berliner Zeitung liliripoti juu ya kuenea kwa homa ya mafua ya ndege barani Afrika. Lilizungumzia juu ya kuku 400 waliopatikana wametupwa katika kitongoji cha Kasarani mjini Nairobi Kenya, ambao ilihofiwa walikuwa wameambukizwa homa hiyo.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa ulidhihirisha kuku hao hawakuwa na virusi vya H5 N1vinavyosababisha homa ya mafua ya ndege. Kosa la maafisa wa serikali na wananchi kutojua juu ya homa hii kunaweza kusababisha janga kubwa la kibinadamu barani Afrika.
Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema homa ya mafua ya ndege sasa imefika nchini Niger, baada kuzuka nchini Misri na Nigeria. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kimataifa la afya ya mifugo, kuku walipatikana na virusi vya H5N1 nchini humo. Maafisa sa serikali ya Niger lakini wanasema hakuna ushahidi kwamba kuku hao walikuwa wanaugua homa hiyo kama vile maafisa wa Nairobi Kenya walivyoripoti baada ya uchunguzi kufanywa kwenye kuku 400.
Nalo gazeti la Süddeutsche liliripoti juu ya kisa cha wakaazi wa kijiji kimoja katika jimbo la Bauchi kuiba kuku waliokuwa wamechinjwa baada ya kupatikana na homa ya mafua ya ndege. Mwandishi habari wa shirika la habari la AFP, Godwin Agbara amenukuliwa na gazeti hilo akisema wakaazi takriban 30 waliingia katika shamba moja la kuku na kuwaiba. Imethibitishwa jamaa hao waliwala kuku hao.
Kwa mujibu wa viongozi wa mkoa wa Bauchi, kuku wasiopungua 700 waliokuwa na virusi vya H5N1 waliibiwa na wakaazi hao wakisema kuwachinja kuku na kuwatupa au kuwachoma badala ya kuwala ni kutupa chakula.
Mada ya tatu ilihusu juhudi za chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Movement for Democratic Change, MDC, kutafuta suluhu kwa mzozo unaokikabili chama hicho. Chama hicho kimegawanyika makundi mawili moja likiongozwa na Morgan Tsvangirai na lengine likiongozwa na Arthur Mutambara.
Mgawanyiko wa chama hicho ulisababishwa na mzozo kuhusu chama hicho kushiriki katika uchaguzi wa baraza la senate uliofanyika nchini humo mwezi Novemba mwaka jana.
Mada ya nne ilihusu umoja wa Ulaya kutaka kupeleka wanajeshi wake katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Tageszeitung lilisema kadri umoja huo unavyokawia kufikia uamuzi wa kuwapeleka wanajeshi wake, ndivyo unavyozidi kutokuwa na uhakika wa wanajeshi hao kupelekwa Kongo kulinda amani wakati wa uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini humo mwezi Aprili.
Wabunge wa umoja wa Ulaya wamefanya azimio jipya. Ujerumani, Ufaransa, Ubelgiji na Sweden zimekubali kushiriki ijapo bado hazijatangaza rasmi. Lakini tatizo lililopo ni kwamba hakuna taifa lolote kati ya haya linalotaka kuongoza kikosi cha walinda amani wa umoja wa Ulaya katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.