Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
10 Machi 2006Kwanza majadiliano katika Muungano wa Ulaya kuhusu kupeleka jeshi kutoka nchi hizo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kulinda amani wakati wa uchaguzi mkuu mwezi wa Juni mwaka huu; ya pili matokeo kwenye pwani ya Afrika Magharibi ambapo wakimbizi 45 walikufa walipojaribu kufika visiwa vya Canary; na hatimaye filamu “Tsotsi” kutoka Afrika Kusini yapewa tunzo la filamu muhimu kabisa “Oscar” nchini Marekani.
Bado Muungano wa Ulaya haujafika uamuzi kuhusu kupeleka jeshi lake Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Masuala ambayo ni wasi mpaka sasa wanajeshi wangapi wapelekwe na kutoka nchi gani. Gazeti la kila wiki “Der Spiegel” linaandika:
“Huweza kusema tena kwamba Ulaya inatoa dalili ya kisiasa. Mpango huo kwa sasa ni ujumbe mdogo tu. Wataalamu wa kijeshi wa Ulaya walichagua malengo matatu kwa jeshi hilo: Kulinda uwanja wa ndege wa Kinshasa, kuwahamisha wasaidizi wa uchaguzi pamoja na wafanyakazi wa Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa ikiwa hali itakuwa mbaya au kulisaidia jeshi la Umoja wa Mataifa katika kuhifadhi amani kama vita vitaepukwa. Serikali ya Ujerumani lakini bado inatumai kwamba huenda mwishowe hakuna haja ya kupeleka jeshi lake ikiwa uchaguzi utafutwa kwa sababu yoyote. Hivyo, Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya angalau zingeonyesha kuwa ziko tayari kusaidia.”
Na kuhusu suala hilo hilo, gazeti la “Sueddeutsche Zeitung”linandika yafuatayo:
“Bila shaka watu wengi nchini Kongo wanasubiri kwa hamu uchaguzi huo wa kwanza tangu kupata uhuru, hasa wale wanaoathirika vibaya na vita vilivyoendelea kwa miaka mingi. Wote wana matumaini kwamba uchaguzi huo hatimaye utaleta amani. Lakini inaonekana kuwa uchaguzi utaleta tu machafuko mengine au hata vita vipya. Kwani kila mmoja atakayeshindwa atatumia silaha zake tena. Umoja wa Mataifa kuomba jeshi lingine kutoka Ulaya kusimamia amani wakati wa uchaguzi kunaonyesha kwamba hauamini amani iliopo hivi sasa. “
Na katika mada nyingine: Wiki iliyopita wakimbizi 45 kutoka nchi za Kiafriak walikufa wakati mashua yao ilipozama kati ya pwani ya Mauretania na visiwa vya Canary. Juu ya hayo gazeti la “Kölner Stadt-Anzeiger” linaandika:
“Bila jumuiya ya kimataifa kupata habari yoyote, wakimbizi wengi dunia wanapata shida kubwa kama kwa mfano katika kupitia bahari ya kwenda nchi za Ulaya. Idadi ya watu wanaokufa haijulikani. Mwaka uliyopita polisi ilihesabu maiti za wakimbizi 500 kwenye pwani za Uhispania, Italia na Afrika Kaskazini. Lakini kwa mujibu wa mashirika ya kutoa msaada kwa wakimbizi idadi hii ni kubwa zaidi kwa kuwa watu wengi wanazama pamoja na mashua zao bila polisi yoyote kujua. Serikali ya Spain ilianza kushirikiana na serikali ya Marokko kuzuia wakimbizi kuondoka bara la Afrika na inataka ushirikiano huo uanzishwe pia na nchi nyingine za Afrika Kaskazini. Lakini wahalifu hawa wanaowapeleka wakimbizi wanatafuta njia nyingine ya kuingia Ulaya kupitia Libya au Mauretania.”
Na mwisho tunaelekea Afrika Kusini ambayo imeshinda katika mashindano ya filamu nchini Marekani. Kwa filamu yake “Tsotsi”, mwendeshaji filamu Gavin Hodd amepata tunzo la Oscar katika kundi la filamu kutoka nchi za nje. Tsotsi ni kijana kutoka kitongoji cha Johannesburg ambaye anampiga risasi bibi mmoja wa Kiafrika ili kuiba gari yake, lakini ndani ya gari hiyo anamkuta mtoto mchanga. Halafu anamtunza mtoto huyu kwa upendo ambao yeye mwenyewe hakuwahi kupata utotoni.
Kuhusu filamu hii gazeti la “Frankfurter Allgemeine Zeitung” linaandika:
“Mafanikio ya filamu kutoka Afrika Kusini yanakuwa ni mengi siku hizi na zinapendwa duniani kote. Kwa miaka mingi ilibidi Waafrika wa Afrika ya Kusini wafanye sanaa zao katika hali ya kubaguliwa na kupigania uhuru. Hivyo uhodari wa wasanii umeongezeka kama inavyoonekana kwa mfano katika tunzo mbili za Nobel katika fasihi. Katika filamu tena kuna waigizaji wazuri, muundu mbinu mzuri na aina nyingi za mazingira pamoja na ufundi sanifu wenye ujuzi mkubwa. Halafu tena, katika Afrika Kusini kuna watoaji hadithi wema kama vile Athol Fugard aliyeandika riwaya ya “Tsotsi” iliyogeuzwa kuwa filamu hii. Kizazi hiki kipya cha Afrika Kuzini hakijali tena malumbano masuala la upinzani na ubaguzi, yaani yaliyotokea hapo zamani. Lakini kinazingatia masuala ya kisasa na za siku za usoni, yaani matatizo kama ukimwi na watu kuzikimbia nchi maskini za Kiafrika kwenda kutafuta maisha bora Afrika Kusini.”