Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
17 Machi 2006Umoja wa Ulaya hatimaye umekubali kuwapeleka wanajeshi wake kulind amani katika jamhuri ya kidemokraisa ya Kongo. Hapo awali haikujulikana wazi ikiwa umoja wa Ulaya ungewapeleka wanajeshi wake katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo kulinda amani wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika nchini humo mwezi ujao.
Gazeti la Süddeutsche lilisema serikali ya Ujerumani ilionekana ikisita katika jambo hili na kansela Angela Merkel pamoja na waziri wake wa ulinzi Franz Josef Jung hawakuonekana kushawishika juu ya umuhimu wa kuwapeleka wanajeshi wa Ujerumani kwenda Kongo. Rais wa Ufaransa Jacques Chirac naye hajaeleza wazi jukumu la nchi yake katika tume ya amani ya umoja wa Ulaya kwenda jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
Gazeti lilimnukulu afisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Ujerumani akisema ipo haja ya kufikia uamuzi juu ya swala hili haraka inavyowezekana. Na ikiwa umoja wa Ulaya hautaki kuwapeleka wanajeshi wake kwenda Kongo basi afadhali kusema wazi badala ya kufanya mijadala mingi isiyotoa mwelekeo wowote. Na kama umoja wa Ulaya hautawapeleka walinda amani kwenda jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo litakuwa janga kubwa, alisema afisa huyo.
Mada ya pili ilihusu ziara ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan barani Afrika. Gazeti la General Anzeiger lilisema huku waafrika wakikabiliwa na njaa, vita na kuishi katika umaskini wana jukumu la kujishughulikia na hawawezi kuyalaumu madola ya kikoloni kwa mashaka yao. Kofi Annan alikuwa mwafrika wa kwanza kuchukua wadhifa wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa hivyo kupata fursa ya kuuhamasisha ulimwengu juu ya matatizo ya waafrika.
Annan aliitembelea Afrika Kusini na Madagascar na atakwenda Kongo Brazaville ambako atakutana na mwenyekiti wa umoja wa Afrika rais Dennis Sossou Nguesso. Ataikamilisha ziara yake katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo atakakokutana na raia Joseph Kabila na kuwahutubia wakongomani.
Gazeti la General Anzeiger limeitaja ziara ya Annan barani Afrika kama ziara ya kuwaaga waafrika, kwani atamaliza awamu yake kama katibu mkuu wa umoja wa mataifa mwishoni mwa mwaka huu.
Mada ya tatu ilihusu kurudishwa nyumbani kwa raia wa Togo ambaye amekuwa akiishi hapa Ujerumani kwa miaka saba kama mkimbizi. Gazeti la Neues Deutschland lilisema Houdou Tchaniley kutoka Togo alirudishwa kwao na utawala wa Potsdam, ijapokuwa maisha yake huenda yakawa hatarini atakapofika Togo. Tchaniley alihamishwa kutoka jela inayotumiwa kuwazuilia wakimbizi wasio halali ya Eissenhüttenstadt Alhamisi wiki hii na kupelekwa katika uwanja wa ndege wa Berlin Tegel, ambako alipandishwa ndegeni na kurudishwa kwao.
Ofisi ya kuwashughulikia wakimbizi ya Brandenburg ilisema haikuwezekana kuizuia hatua hiyo ya kumrudisha nyumbani. Mahakama ya Potsdam iliamua kwamba Tchaniley hana haki ya kuendelea kuishi Ujerumani kama mkimbizi wa kisiasa eti kwa sababu maisha yake yamo hatarini nchini Togo.
Likitukamilishia makala hii, gazeti la Neue Zürcher liliripoti juu ya wimbi kubwa la wahamiaji wanaotaka kuingia nchini Uhispania. Meli ya uokozi ya Uhispania iligundua maiti takriban 18 zilizokuwa katika pwani ya Mauritania. Wote walikuwa wahamiaji wa kiafrika kutoka kusini mwa jangwa la Sahara, waliofariki dunia baada ya dau walilokuwa wakisafiria kupinduka.
Juma lililopita watu 25 waliokuwa wakisafiri katika madau mawili walikufa maji. Mnamo Jumatano wiki hii serikali ya Uhispania mjini Madrid ilipitisha sheria za kuziongezea nguvu juhudi za usalama katika pwani zake. Ujumbe wa Uhispania ulisafiri kwenda Mauritania Alhamaisi juma hili kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya nchi hiyo juu ya ushirikiano mzuri katika kukabiliana na tatizo la wahamiaji.
Wimbi hili jipya la wakimbizi si sadfa. Kwa sababu ya matatizo yanayoendelea barani Afrika na Moroko kushinikizwa na umoja wa Ulaya na Uhispania kuzilinda pwani zake, wakimbizi wamebadili njia nyengine ya kuingilia Ulaya.