Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
21 Julai 2006Likutuanzia na hali ya wasiwasi wa kuzuka vita kati ya Somalia na Ethiopia, gazeti la Süddeutsche Zeitung lilisema hali sasa inatisha. Mhariri alisema mamia ya wanajeshi wa Ethiopia wamevuka mpaka na kuingia Somalia wakitumia malori.
Ethiopia inataka kuwachakaza wanamgambo wa kiislamu nchini Somalia ambao mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu waliuteka mji wa Mogadishu kutoka kwa muungano wa wababe wa kivita wanaoungwa mkono na Marekani.
Kwa mujibu wa taaarifa iliyotolewa na shirika la habari la BBC wanajeshi wa Ethiopia waliingia mjini Baidoa, makao makuu ya serikali ya mpito ya Somalia ambayo haina nguvu nchini humo, licha ya kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Hatua ya jeshi la Ethiopia huenda ikachochea mgogoro wa Somalia.
Mashehe wa muungano wa kiislamu wanaitazama serikali ya mpito kama chombo cha serikali ya mjini Addis Ababa. Wanamgambo wa kiislamu waliouteka mji wa Mogadishu wako tayari kufanya mazungumzo na wajumbe wa serikali lakini hatari ya kuzuka mapigano inazidi.
Iliripotiwa kwamba wanamgambo wa kiislamu waliukaribia mji wa Baidoa lakini muungano wa mahakama za kiislamu ukapinga madai hayo ukisema hauna mpango wowote wa kuushambulia mji wa Baidoa. Mapigano ya kijeshi kati ya Somalia na Ethiopia yatakuwa pigo kubwa kwa mazungumzo juu ya hali ya baadaye ya Somalia mjini Khatoum nchini Sudan, yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Gazeti la Süddeutsche Zeitung lilimnukulu msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni nchini Marekani, Sean McComark, akizitaka pande husika nchini Somalia zirudi katika mazungumzo.
Mada ya pili ilihusu mkutano kuhusu Darfur uliofanyika mjini Brussels Ubelgiji. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema mkutano wa Brussels haukuwa na ufanisi mkubwa. Walioshiriki katika mkutano huo wakiwemo wapatanishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika walitoa mwito kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Matafia wa kulinda amani kipelekwe Darfur.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, aliitolea mwito jumuiya ya kimataifa itoe fedha za kukisaida kikosi cha wanajeshi 7,000 wa Umoja wa Afrika walio Darfur.
Kuhusu mada hii gazeti la Süddeutsche Zeitung liliandika: Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya unataka wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa watumwe Darfur. Mashirika haya mawili yana wasiwasi huenda juhudi za kuleta amani Darfur zikasambaratika. Katika mkutano wa mjini Brussles, Kofi Annan alionya mapigano ya Darfur yasitishwe.
Mjumbe wa Ulaya anayeshughulikia sera za kigeni, Javier Solana, alinukuliwa na gazeti hilo akisema jeshi la Umoja wa Mataifa linatakiwa kuchukua kazi kutoka kwa kikosi cha Umoja wa Afrika huko Darfur kama njia ya hakika ya kuumaliza mzozo wa Darfur.
Mada ya tatu ilihusu hatua mpya ya kundi la waasi nchini Uganda la LRA kushiriki katika mazungumzo ya mjini Juba kusini mwa Sudan. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema kwa miaka 20 kundi la LRA limekuwa likiwahangaisha raia wa kaskazini mwa Uganda likitaka waishi kwa kufuata amri kumi za Mungu.
Kundi hilo huwateka nyara watoto na kuwatumia kwa nguvu kama vyombo vya mauaji. Kiongozi wa LRA, Joseph Kony, alikubali kushiriki katika mazungumzo mjini Juba katika juhudi za kuumaliza mzozo wa Uganda Kaskazini.
Likitukamilishai na mada hii gazeti la Frankfurter Rundschau liliandika: Mzozo wa Uganda Kaskazini ambao umesababisha unyama mkubwa dhidi ya binadamu, huenda ukamalizika hivi karibuni. Kwani viongozi wa serikali ya Uganda na waasi wa kundi la LRA wameanza mazungumzo mjini Juba. Amani inabisha hodi kaskazini mwa Uganda liliandika gazeti hilo.