Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
28 Julai 2006Tunaanzia mjini Kinshasa. Gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema hali ya wasiwasi inazidi huku uchaguzi ukikaribia nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Muangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya, Michale Schlicht; alinukuliwa na gazeti hilo akisema watu wengi nchini Kongo wamejawa na hasira kwa mataizo yanayojitokeza katika maandalizi ya uchaguzi huo.
Kuna vyama vingi na wagombea wengi wanaoshiriki katika uchaguzi huo. Kuna maandamano yaliyofanyika katika barabara za mjini Kinshasa ambapo waandamanaji waliwashambulia kwa mawe waangalizi wa Umoja wa Ulaya.
Gazeti la Frankfurter Rundschau liliripoti pia juu ya kushambuliwa kwa wanajeshi wa Ujerumani mnamo siku ya Alhamisi walipokuwa kuwa njia kuelekea katika kambi yao huko Ndolo wakitokea uwanja wa ndege wa Ndjili. Kamanda wa kikosi cha Ujerumani, Peter Fuss, alinukuliwa na gazeti hilo akisema mambo yanatokea haraka mno. Magari mawili ya jeshi la Ujerumani yalishambuliwa na waandamanaji kwa mawe na marungu.
Mashariki mwa Kongo wanajeshi wa serikali wamekuwa wakikabiliana na waasi katika mapigano ambayo yamesababisha watu takriban elfu 40 kuyakimbia makazi yao. Watu hawa hawatakuwa na nafasi nzuri ya kufika katika vituo vya kupigia kura kwa sababu ya hali mbaya ya usalama katika eneo hilo.
Habari kuhusu uwezekano wa kuzuka vita vikubwa katika pembe ya Afrika kati ya Ethiopia na Somalia ziliripotiwa sana na gazeti la Frankfurter Rundschau. Mhariri aliandika kwamba serikali ya Ethiopia inavuruga mambo. Serikali ya mpito ya Somalia nayo haitaki kujua kuhusu mgogoro huo.
Nchi hizi mbili zinadai kuwepo wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia ni kuisadia serikali ya mpito kuwadhibiti wanamgambo wa kiismalu ambao wanavaa sare walizopewa na serikali ya Ethiopia. Kuingia kwa wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia huenda kukasababisha vita vikali, limesema gazeti hilo.
Walioshuhudia, wakiwemo pia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wamesema wanajeshi takriban 5,000 wa Ethiopia wameingia Somalia pamoja na magari ya kijeshi na helikopta ambazo zimekuwa zikiitawala anga ya mji wa Baidoa na Wajid.
Mada nyengine ilihusu mamia ya wanasiasa kuzuiliwa gerezani nchini Ethiopia. Gazeti la Tageszeitung lilisema ukandamizaji wa upinzani unaofanywa na serikali ya mjini Addis Ababa unawafanya wadhamini kuwa waangalifu. Fedha zilizozuiliwa hutolewa tu wakati kukiwa na lazima, lakini kwa Marekani Ethiopia ni mshirika katika vita dhidi ya ugaidi, hususan dhidi ya Somalia.
Upinzani nchini Ethiopia uliitisha maandamano ya amani kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana ulioshindwa na chama tawala. Mwezi Novemba kulitokea machafuko yaliyozimwa kwa nguvu, zaidi ya watu 50 waliuwawa wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na wanawake.
Tangia hapo wakosoaji wa serikali, viongozi wa upinzani na waandishi habari bado wanasubiri kuhukumiwa kwa uhaini na kuchochea mauaji ya halaiki ya mbari ya Tigray, inayowakilishwa kwa idadi kubwa katika serikali ya sasa. Watuhumiwa wanakabiliwa na hukumu ya kifo iwapo watapatikana na hatia na hakuna uhuru wa vyombo vya habari nchini Ethiopia kwa sababu waandishi wamo gerezani, liliandika gazeti la Tageszeitung.
Na hatimaye gazeti la Süddeutsche Zeitung liliripoti juu ya mazungumzo kati rais George W Bush wa Marekani na kiongozi wa kundi la waasi la SLA katika jimbo la Darfur nchini Sudan, Minni Minnawi. Mhariri alisema mkataba wa amani umebakia katika makaratasi tu kwani kumetokea mapigano tangu kujsainiwa mkataba huo mwanzoni mwa mwezi Mei.
Rais Bush alimkaribisha Minnawi katika ikulu yake kujaribu kuukoa mkataba wa amani usivunjike. Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine liliandika kwamba viongozi hao walijadiliana juu ya kuzisaidia juhudi za kufikia amani Darfur na vipi kikosi maalumu cha umoja wa mataifa kinavyoweza kukisaidia kikosi cha Umoja wa Afrika kulinda amani huko Darfur.