Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
4 Agosti 2006Na tukianzia na uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema uchaguzi huo ulifanyika baada ya matayarisho makubwa ya usalama. Raia zaidi ya milioni 25 wa Kongo walikuwa na jukumu la kumchagua rais wao mpya na wabunge.
Pamoja na machafuko yaliyozuka wakati wa kampeni kulikuwa na visa vya hapa na pale vya ghasia siku ya kupiga kura. kwa mujibu wa tume huru ya uchaguzi nchini Kongo vituo saba vya kupigia kura vilichomwa moto katika mkoa wa Kasai, nyumbani kwa kiongozi wa upinzani Etienne Chisekedi.
Gazeti la Frnkfurter Allgemeine lilisema Jumamosi ya kuamkia siku ya kura, magari yaliyokuwa yamebeba vifaa vya kupigia kura ambavyo vingetumiwa katika vituo 70, yalishambuliwa na wafuasi wa Chisekedi na kuviharibu vifaa hivyo.
Mjini Kinshasa watu walianza kuunga foleni alfajiri na wengine walilala wakisubiri nje ya vituo vya kupigia kura. Tume ya uchaguzi iliyajengea masanduku ya kura kuzuia udanganyifu. Lakini matataizo yalitokea katika kitongoji cha Shobo mjini Kinshasa, ambako mamia ya wapiga kura waliambiwa nambari za kadi zao za kura zinawaruhusu kupiga kura mjini Lubumbashi, yapata kilomita 2,000 kutoka Kinshasa.
Nalo gazeti la Frankfurter Rundschau kuhusu uchaguzi wa Kongo liliandika: machafuko mengi yaliripotiwa katika jimbo la Kasai, ngome ya kiongozi wa chama cha UDPS, Etiene Chisekedi, ambaye alitisha watu waugomee uchaguzi huo. Wafuasi wake walilivichoma moto vituo vya uchaguzi na kuwatisha raia katika barabara za mjini Mbuji Mayi. Gazeti lilisema rais Joseph Kabila na nafasi kubwa ya kuushinda uchaguzi wa Kongo lakini atakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Jean Pierre Bemba.
Likitubadilishia mada gazeti la Frankfurter Rundschau liliripoti juu ya kuahirishwa kwa kesi ya rushwa inayomkabili makamu wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, bwana Jacob Zuma. Mahakama ya mjini Pietermaritzburg iliamua Jumatatu wiki hii kuiahirisha kesi ya Zuma hadi Septemba 5. Kuahirishwa kwa kesi hiyo kutawapa nafasi waongoza mashataka wa serikali na mawakili wa bwana Zuma kujiandaa vizuri zaidi kabla kesi hiyo kusikilizwa.
Zuma anashtakiwa kwa kupokea rushwa ili kuiolinda kampuni ya silaha ya Ufaransa kutokana na uchunguzi wa serikali. Bwana Zuma amekanusha mashtaka hayo. Zuma aliyezaliwa mwaka wa 1942 alikuwa hadi mwaka waka 2005 makamu wa rais wa Afrika Kusini na alipigiwa upatu kuchukua wadhifa wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2009. Mshauri wake wa maswala ya fedha, Shabir Shaik tayari amehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.
Je wanajeshi wa Ethiopia wameondoka kweli kutoka nchini Somalia? Liliuliza gazeti la Neue Zürcher. Mwishoni mwa juma lililopita iliripotiwa kwamba wanajeshi wa Ethiopia hawakuonekana tena mjini Baidoa , makao makuu ya serikali ya mpito ya Somalia. Gazeti lilimnukulu msemaji wa serfikali ya mpito ya Somalia akikanusha habari za vyombo vya habari na kusema hakuna tena wanajeshi wa Ethiopia nchini Somalia.
Gazeti la Neue Zürcher lilisema kwamba wanamgambo wa kislamu ambao wanaudhibiti mji wa Mogadishu wametumia kuwepo kwa wanajeshi wa Ethiopia mjini Baidoa kama sababu ya kukataa kushiriki katika mazungumzo ya kutafuta amani mjini Khartoum nchini Sudan. Kiongozi wa wanamgambo hao, Sheikh Hassan Dahir Aweys, ametangaza vita vya Jihad dhidi ya adui. Inaonekana wanamgambo hawaamini kwamba wanajeshi wa Ethiopia wameondoka Somalia na bado wanasubiri kuona jambo hili likitimia.
Naibu waziri wa Marekani, anayeshughulikia maswala ya Afrika, Jendayi Frazer, alizionya Ethiopia na Eritrea kwa kuingilia mambo ya ndani ya Somalia. Frazer alisema serikali ya mpito ya Somalia na wanamgambo wa kiislamu wanapokea misaada kutoka mataifa ya nje na kwa njia hiyo wamewaingiza raia wa kigeni nchini Somalia.