Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
12 Agosti 2005Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaanza na maziko ya John Garang wikendi iliyopita. Linasema maelfu ya raia wa kusini mwa Sudan walikusanyika kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo. Kifo chake kimeelezewa na gazeti hilo kuwa tisho kubwa kwa juhudi za amani kati ya eneo la kusini na kazkazini. Marais wa Afrika Kusini, Kenya, Ethiopia, Tanzania na rais wa jumuiya ya nchini za kiarabu walihudhuria maziko ya shujaa Garang.
Gazeti lilimnukulu rais wa Uganda Yoweri Museveni aksiema kwamba helikopta yake ambayo ilikuwa ikimrejesha nyumbani marehemu Garang ilianguka kwa sababu ya hali mbaya ya hewa. Hata alisema pia inawezekana ilianguka kwa sababu nyengine.
Mjumbe maalumu wa umoja wa mataifa nchini Sudan, Jan Pronk aliyapinga madai ya Museveni akisema hakuna ushahidi wowote. Pia waziri wa habari nchini Sudan alisema kwamba matamshi ya Museveni hayana ukweli na ni yanatatanisha. Serikali ya Sudan na kundi la SPLM imeanza uchunguzi wa kifo cha Garang, ambao umoja wa mataifa unataka pia kushiriki.
Mada ya pili iliyozingatiwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine ni kuapishwa kwa Silva Kiir kuwa makamu wa rais wa Sudan kuchukua mahala pake marehemu Garang. Gazeti limesema kuteuliwa kwa Kiir, ambaye hajulikani sana, ni mtihani mkubwa kwa kundi la SPL ikiwa kweli litaendeleza juhudi za amani likishirikiana na serikali ya Khartoum.
Gazeti la Frankfurter Rundschau lilizungumzia mazungumzo kati ya waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Peter Strück na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Kofi Annan. Strück alielezea wasiwasi wake juu ya hatua ya serikali ya Khartoum kuzuilia visa za kusafiria za wanajeshi wa Ujerumani na mataifa mengine wanaotakiwa kulinda amani tangu mkataba wa kusitisha mapigano uliposainiwa kusini mwa Sudan.
Struck amenukuliwa na gazeti hilo akisema kwamba Ujerumani itashiriki katika juhudi za kepeleka misaada kwa eneo lililokumbwa na mzozo la Darfur. Walinda usalama 300 kutoka Ghana na Malawi watapelekwa kwa ndege za Ujerumani huko Darfur katika siku chache zijazo.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine kuhusu mada hii limemnukulu waziri Strück akiutaka umoja wa mataifa uishinike serikali ya Sudan ili isiitatize tume ya kulinda amani kusini mwa Sudan.
Kufuatia baa la njaa nchini Niger, umoja wa mataifa umeanza sasa kupeleka chakula kwa wingi nchini humo. Gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema tani 35 za chakula zimewasili magharibi mwa mji wa Niamey kitakachogawanywa kwa wahanga 2000.
Kupitia ushirikiano na serikali ya Niger, watu milioni 2.5 watasaidiwa katika kipindi cha miezi miwili ijayo. Kuhusu tatizo la njaa nchini Niger, gazeti la Frankfurter Allgemeine limemnukulu waziri wa miksaada ya maendeleo wa Ujerumani Bi Heidermarie Wieczorek-Zeul akiilaumu serikaliy a Niger kwa kechelewa kuitisha misaada kutoka kwa jamii ya kimataifa.
Mada nyengine iliyoripotiwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine ni matokeo ya uchaguzi nchini Ethiopia. Gazeti lilisema baada ya miezi mitatu ya mivutano kufuatia uchaguzi, tume ya uchaguzi nchini Ethiopia ilitangaza ushindi wa serikali ya Meles Zenawi. Upinzani umekataa kuyatambua matokeo hayo na unataka kuwasilisha mashtaka mahakamani. Serikali ya muungano inayoongozwa na Zenawi imelikataa pendekezo la upinzani kutaka kuundwe serikali ya umoja wa taifa.