Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
26 Agosti 2005Gazeti la Frankfurter Rundschau linatufungulia kwa kuapishwa kwa rais mpya wa Burundi, Pierre Nkurunziza, ambaye ni rais wa kwanza kuchukua wadhifa huo kwa njia ya uchaguzi baada ya miaka 12. Rais aliyemtangulia aliuwawa mwaka wa 1993 na baadaye mapinduzi ya kijeshi na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilisababisha watu zaidi ya elfu 300 kuyapoteza maisha yao.
Gazeti limesema kuchaguliwa kwa Nkurunziza kuliongoza taifa hilo, ni kama ishara ya amani ya uongo nchini humo kwani haijulikani hasa mambo yatakavyokuwa katika siku za usoni. Kiongozi huyo mpya mwenye umri wa miaka 41 atakabiliwa na kibarua cha kuliunganisha taifa na kuyajumulisha makundi ya waasi katika kuliendeleza taifa hilo.
Mada ya pili ilihusu ziara rasmi ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa bwana Kofi Annan nchini Niger. Gazeti la Die Welt lilisema Annan aliyatolea mwito mataifa ya Afrika Magharibi kushirikiana katika kupambana na baa la njaa. Katika mkutano wake na rais wa Niger, Mamadou Tanja, bwana Annan aliahidi kwamba umoja wa mataifa utashirikiana na serikali ya Nger na mashrika yasiyo ya kiserikali kutoa misaada kwa raia wanaoteseka kwa njaa nchini humo. Annan aliongeza kusema kwamba iko haja ya kuhakikisha usalama wa chakula katika eneo la Afrika Magharibi.
Lengo la ziara yake Annan nchini Niger lilikuwa kujionea mwenyewe jinsi njaa ilivyowaathiri raia wa Niger. Shirika la kutoa misaada la madaktari wasio na mipaka limeulaumu umoja wa mataifa kwa kuchelewa kuchukua hatua za dharura kupambana na njaa nchini Niger. Lakini Annan amekwepa kuzungumzia madai hayo na badala yake kuzisifu juhudi za shirika hilo nchini humo.
Kuhusu mada hii gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema umoja wa mataifa utafanya kila linalowezekana kuzuia ukosefu wa chakula nchini Niger katika siku za usoni. Kwa majuma kadhaa kumekuwa na mabishano ni nani anayetakiwa kulaumiwa kuhusiana na tatizio la njaa nchini Niger. Gazeti lilisema umoja wa mataifa unalaumiwa lakini nao unailaumu jamii ya kimataifa.
Mada ya tatu ilihusu hatua ya rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kujitenga mwenyewe kutoka kwa majirani zake. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema kwamba katika barua yake ya kila juma katika mtandao wa internet, rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini aliwaonya wanachama wa jumuiya ya uiano wa kiuchumi wa mataifa ya kusini mwa Afrika, SADC, kwamba wote kwa pamoja wanatakiwa kujitahidi la sivyo wote watasambaratika.
Bila kuitaja Zimbabwe na hatua ya serikali ya kuyavunja makazi ya walalahoi, rais Mbeki alitaka mataifa ya SADC kuhakikisha usalama, kuboresha hali ya maisha ya raia wake, kuunda sera mpya za maongozi na hasa kukomeshwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Likitukamilishia makala hii gazeti la Frankfurter Allgemeine lilikuwa na habari za mwaliko wa rais George W Bush wa Marekani kuitembelea Libya. Rais wa Libya, Muammmar Gaddafi, amemualika rais Bush baada ya kuombwa afanye hivyo na mbunge Marekani, Richard Lugar, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bunge inayohusika na siasa za mataifa ya kigeni. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice pia amealikwa.
Bwana Lugar alifanya mazungmzo na serikali ya Libya kujaribu kurudisha uhusiano mwema kati ya Libya na Marekani. Libya ilichukua dhamana katika kulipua ndege ya abiria ya Marekani mwaka wa 1988 na kuahidi kutojihusisha na kutengeneza silaha za maangamizi ya halaiki. Kutoka wakati huo viongozi mashuhuri walioitembelea Libya ni kansela wa Ujerumani, Gerhard Schroeder, waziri mkuu wa uingereza, bwana Tony Blair na rais wa Ufaransa, Jacques Chirac.