Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili
4 Novemba 2005Gazeti la Frankfurter Rundschau linatufungulia na wasiwasi wa kuzuka vita kati ya Ethiopia na Eritrea. Wanajeshi wa nchi hizo wamepelekwa katika eneo la mpakani wakiwa na vifaa vya vita. Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Kofi Annan, ameonya juu ya kuzuka kwa vita na kutoa mwito majeshi ya nchi hizo yaondoke katika eneo hilo la mpakani.
Mwezi uliopita, Eritrea ilifutilia mbali safari zote za helikopta za walinda amani wa umoja wa mataifa nchini humo, ambao wamekuwa wakililinda eneo linalozitenganisha nchi hizo mbili, ishara kwamba serikali ya Asmara ilitaka kuwatuma wanajeshi wake.
Annan amesema hatua hiyo ya Eritrea itasambaratisha juhudi za amani kati ya mataifa hayo. Lakini rais wa Eritrea, Isaias Afeworki, alisema katika barua yake kwa baraza la usalama la umoja wamataifa kwamba hajaliachilia jukumu lake katika kutafuta amani ya eneo hilo. Alisema uamuzi wa mahakama ya kimataifa mjini The Hague, Uholanzi mwaka wa 2002, iliupa mji wa Badme kwa Eritrea, lakini Ethiopia haiutambui uamuzi huo na bado imeendelea kuumiliki mji huo.
Mataifa hayo mawili yalipigana vita vya miaka miwili na nusu kutetea mpaka, ambapo watu takriban elfu 70 waliuwawa. Baraza la usalama la umoja wa mataifa linaendelea na juhudi zake za kuutanzua mzozo huo. Gazeti linasema katika mahojiano ya waziri mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi na shirika la habari la BBC, Zenawi alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na rais wa Eritrea Afeworki.
Gazeti la Die Welt lilizungumzia kuhusu machafuko yaliyotokea katika mji wa Addis Ababa, Ethiopia Jumatano iliyopita. Makundi ya kupigania haki za binadamu nchini humo yamesema watu wasiopungua 30 waliuwawa. Madaktari wamethibitisha kwamba watu zaidi ya 80 walijeruhiwa katika mapigano makali kati ya polisi na waandamanaji, wanaopinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwezi Mei. Machafuko hayo ambayo yameelezewa kuwa mabaya zaidi yamezidi kumbabaisha waziri mkuu Zenawi huku taifa lake likijiandaa kupigana na Eritrea.
Gazeti la Frankfurter Rundschau liliripoti juu ya kuzuka kwa vurugu kati ya wafuasi wa chama cha upinzani cha CUF na polisi visiwani Zanzibar. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji, waliopinga kuruhusiwa kupiga kura watu ambao waliletwa kwa mabasi kutoka nje ya visiwa hivyo. Gazeti lilisema waangalizi wa kimataifa walithibitisha kuwepo dosari na walishuhudia kupigwa kwa wafuasi wa chama cha CUF. Watu zaidi ya 200 walijeruhiwa na wengine kadhaa wakauwawa katika fujo hizo.
Kiongozi wa upinzani, Seif Sherif Hamadi, alinukuliwa na gazeti hilo akisema ataitisha maandamano makubwa kama yale yaliyofanwa nchini Ukraine kwa kile anachokiita wizi wa ushindi wake uliofanywa na chama tawala cha CCM. Kufuatia matamshi haya serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ilituma wanajeshi elfu 35 visiwani humo kuzuia kuzuka kwa ghasia.
Likitupeleka nchini Ivory Coast gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema vita vya wenyewe kwa wenyewe vinanukia nchini humo. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limesema jeshi la nchi hiyo linawasajili watoto kati ya umri wa miaka 13 na 15 kutoka nchini Liberia walio na uzoefu wa vita. Watoto hao wameahidiwa kupewa chakula, nguo na dola kati ya 300 na 400 za kimarekani kwa kazi watakayoifanya nchini Ivory Coast.
Vita huenda vikazuka kufuatia hatua ya rais wa nchi hiyo Laurent Gbagbo kuendelea kubakia madarakani licha ya awamu yake kumalizika rasmi mwishoni mwa juma lililopita. Pia kuahirishwa kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 30 na hatua ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kumruhusu Gbagbo kutawala kumewakasirisha waasi wa kazkazini. Rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria na rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini wanatarajiwa kuzuru nchini humo kuutanzua mzozo huo.