Afrika katika Magazeti ya Ujerumani 07.05.2005
6 Mei 2005
Gazeti la GENERAL ANZEIGER limeandika makala ndefu kuhusu ‚uhuru wa vyombo vya habari’ katika nchi za Afrika, kwa kuzingatia pia kuwa Jumatatu iliyopita ilikuwa siku ya uhuru wa uandishi wa habari.
Gazeti hili limeendelea kwa kuandika:
“Viongozi wengi wa nchi za Afrika hudai uhuru wa vyombo vya habari ni jambo la kigeni kutoka nchi za magharibi na si zuri kwa nchi za Afrika. Kwa mantiki hii hutumia nguvu za dola na sheria za ugandamizaji ili kuondoa kabisa uhuru wa uandishi wa habari. Waandishi wa habari wasioelemea upande wa serikali, hutishiwa kufungwa na pengine hata kuuliwa.
Kwa mfano waandishi wa habari wawili, Habteab na Habtemichael kutoka Eritrea. Baada ya nchi yao kujikomboa hapo mwaka 1993 -- kufuatia vita vya ukombozi vya miaka mingi dhidi ya Ethiopia -- waandishi hawa wa habari walitaraji nchi yao itakuwa ya uwazi na ya kidemokrasi. Kwa kutumia gazeti lao MEQALEH walisambaza ujumbe huu nchini kote. Lakini miaka 3 ½ tu baadaye, hapo mwaka 2001, magazeti mengi ya watu binafsi ikiwa ni pamoja na gazeti lao, yalipigwa marufuku na rais Isayas Afewerki. Kufumba na kufumbua, serikali ya Eritrea ikawafunga jela waandishi wengi nchini humo.
Mpaka leo haijulikani Habteab na Habtemichael, ambao hata hawajafunguliwa mashtaka mahakamani, hawajulikani wako wapi na wana hali gani. Hata hivyo watawala nchini Eritrea wamefanikiwa kuwatisha waaandishi wa habari, kiasi kwamba hivi sasa hawaikosoi tena serikali.
Gazeti la GENERAL ANZEIGER limesema, tukio hili la Eritrea ni mfano tu, kwani kila mwaka, matukio mengi kama haya yanatokea katika nchi mbalimbali barani Afrika.
Nalo gazeti la DIE TAGESZEITUNG limeandika habari za kusikitisha kuhusu wakimbizi wa kiafrika waoteseka kwenye kambi za wakimbizi nchini Libya.
Miaka miwili baada ya Libya na Italia kufunga mkataba wa kupambana na wimbi la wakimbizi, tume ya umoja wa Ulaya, iliyozitembelea kambi za wakimbizi nchini Libya, imetoa ripot i ya kusikitisha. Ripoti hii imesema, wakimbizi hao wanateswa, wananyimwa hata haki zao za kimsingi.
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2003, Silvio Berlusconi na Muammar al Gaddafi walifunga mkataba wa kupambana na wimbi la wakimbizi waliokuwa wanajaribu kuingia kwa mitumbwi katika umoja wa Ulaya kupitia kwenye pwani ya magharibi ya Italia – mara nyingi kutoka nchi za kaskazini mwa Afrika ikiwa ni pamoja na Libya.
Idadi ya wakimbizi imepungua na wale wanaofanikiwa kuingia nchini Italia, wanarejeshwa moja-kwa-moja kwa ndege kwenye kambi ya wakimbizi ya Tripolis.
Kwa muda mrefu serikali ya Italia imekuwa inagoma kutoa maelezo juu ya mkataba wake na Libya. Hata hivyo utata uliibuka baada ya Italia kugunduliwa imepelekea nchini Libya boti za mipira 100, magari makubwa 6, mabasi 3, vyombo vya kuonea usiku, kamera za majini, magodoro na mablanketi – lakini pia mifuko 1,000 ya kutunzia maiti. Kwa mara ya kwanza unyama wa makubaliano ya nchi hizi ukaanza kujulikana.
Mwaka jana wawakilishi wa Umoja wa Ulaya walitembelea kambi za wakimbizi na kuona jinsi watu 200 – wanaume, wanawake, watoto wanavyofungiwa kwenye chumba kimoja.
Gazeti la DIE TAGESZEITUNG limemalizia kwa kuandika, serikali ya Italia sasa inatakiwa kueleza, ina uhakika gani kwamba wakimbizi 1,500 waliofungwa kwenye kambi za Libya wanatendewa haki kulingana na makubaliano ya kinga ya wakimbizi ya Geneva. Na kwa nini Italia ilipeleka huko mifuko 1,000 ya maiti.
Nalo gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika juu ya mzozo unaoendelea nchini Togo.
Kinachoendelea nchini Togo hivi sasa ni hatua za mwisho kuelekea kwenye hali ya Somalia – yaani hali ya kusambaratia kabisa kwa utawala.
Hali hii ya kujiangamiza wenyewe ilianzia Somalia, ikafika Afrika magharibi Liberia na Sierra Leone na hatimaye Ivory Coast, nchi ambayo ilikuwa inachukuliwa kuongoza kwa utulivu barani Afrika.
Mara nyingi baada ya utawala wa kidikteta unapoangushwa, wananchi hujikuta wanapigana wao kwa wao badala ya kuanza kufurahia matunda ya demokrasia. Uhasama wa kikabila hufufuliwa upya na kuchochea vita.
Kwa maelezo hayo yaliyoandikwa kwenye gazeti la la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG ndiyo tunakamilisha kipindi hiki cha “Afrika katika Magazeti ya Ujerumani”