Afisa wa polisi akamatwa kufuatia mauaji ya mwanablogu Kenya
13 Juni 2025Pia mtu aliyeivuruga kamera ya CCTV kwenye kituo cha polisi cha Central amekamatwa. Wakati huo huo Mamlaka huru ya usimamizi wa polisi nchini Kenya, IPOA, imebainisha kuwa watu 20 wamepoteza maisha yao mikononi mwa polisi katika muda wa miezi minne iliyopita.
Kwa mujibu wa msemaji wa idara ya polisi Michael Muchiri,konstabo mmoja amekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwalimu Albert Ojwang akiwa mikononi mwa polisi.
Hata hivyo hakuelezea zaidi na kuitwika mamlaka ya usimamizi wa polisi, IPOA, jukumu la ufafanuzi.
Amri ya kuwakamata maafisa 3 na raia 2
Kwa upande wake, waziri wa usalama wa taifa wa Kenya Kipchumba Murkomen amesisitiza kuwa watawaunga mkono polisi kutimiza majukumu yao ila sheria lazima zifuatwe na wote,.
"Maafisa wetu wa polisi na usalama sharti wajue kuwa kama wizara na serikali tunawaunga mkono kikamilifu.Hatutasesereka, haijalishi kinachosemwa,wajibu wetu katika afisi ya usalama ni kuwalinda wote,,,,na kuwataka polisi na pia raia wawajibike,” alisema Murkomen.
Wakati huohuo,makachero wanawasaka maafisa wengine 2 wa polisi kwa tuhuma za kuhusika na kisa hicho hicho.
Mamlaka ya IPOA iliamuru maafisa 3 na raia 2 wa kawaida kukamatwa baada ya watu hao kutoweka.Duru zinaeleza kuwa wamezima simu zao na hawapatikani.
Ifahamike kuwa maafisa hao wa polisi wanaosakwa walishaandikisha taarifa kwa mamlaka ya IPOA.Kadhalika maafisa wengine 17 waliohojiwa wamerejea kwa mamlaka ya usimamizi wa polisi kubadili taarifa zao.
Polisi wanasaka rungu lililotumiwa katika kisa hicho cha mauaji.Kufikia sasa watu wasiopungua 23 wakiwemo maafisa wa polisi wamehojiwa.
Wakati huohuo, mtu aliyeaminika kuvuruga na kuchezea kamera za CCTV kwenye kituo cha polisi cha Central amekamatwa.
Maandamano ya wanaharakati kudai haki
Amekiri kuwa alilipwa shilingi alfu tatu za Kenya kufuta picha cha kamera hizo ambayo yeye ndiye aliyewajibika kuzitundika awali.
Kisa hicho kimezua hisia mseto na kuwasukuma wanaharakati kuandamana kudai haki kwa wahusika. Huko kaunti ya Homabay, maandamano yanaripotiwa kutokea kupinga mauaji ya Albert Ojwang.
Kufuatia maandamano ya saa chache zilizopita katikati ya jiji la Nairobi, waziri mkuu wa zamani wa chama cha ODM, Raila Odinga ameikosoa serikali kwa kile anachokiita matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia.
Kwenye taarifa yake ya mtandao wa X,ODM inaeleza kuwa visa hivyo vinamaliza nguvu makubaliano ya ushirikiano kati yao na chama tawala cha UDA. Kadhalika wanatiwa shaka na utekaji na ukamataji wa vijana ukizingatia mauaji ya Albert Ojwang.