AfIGF2025: Afrika yazungumzia mustakabali wa kidijitali
30 Mei 2025Katika kipindi ambacho Afrika inaendelea kukumbatia maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, Kongamano la Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF) limerejea kwa kishindo mwaka huu, likifanyika jijini Dar es Salaam.
Likiandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Umoja wa Afrika (AU), Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (ECA), na wadau wengine wa sekta binafsi na ya kiraia, AfIGF limekuwa jukwaa muhimu la mjadala wa sera, ushirikiano na ubunifu.
Jukwaa la AfIGF 2025 linafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, likiwakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kujadili ajenda za kidijitali zenye mguso wa kijamii, kiuchumi na kiusalama.
Miaka ya majadiliano: Kutoka Misri hadi Tanzania
Kongamano hili lilianza safari yake nchini Misri, ambako lilifanyika kwa mara ya kwanza. Tangu wakati huo, limekuwa likifanyika kila mwaka katika nchi tofauti, likileta pamoja wataalamu wa teknolojia, watunga sera, wanaharakati wa haki za kidijitali, vijana na sekta binafsi.
Katika kipindi hicho, limechangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mtazamo wa bara la Afrika kuhusu usimamizi wa mtandao, haki za kidijitali, na maendeleo jumuishi ya TEHAMA.
AfIGF limechochea mijadala ya sera zinazozingatia mazingira ya Kiafrika, kusaidia ubadilishanaji wa mbinu bora, na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
Kongamano la mwaka huu: Vipaumbele na maudhui kuu
AfIGF 2025 limeweka mbele masuala kadhaa yenye umuhimu kwa bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI), ujenzi wa miundombinu ya kidijitali ya umma, usalama wa mtandao, na upatikanaji jumuishi wa mtandao hadi maeneo ya vijijini.
Lengo kuu ni kujenga mazingira ya usimamizi wa mtandao ambao unnachochea ushirikiano, kulinda haki, na kuwezesha wananchi wote kushiriki kwenye uchumi wa kidijitali.
Katika mkutano huo, washiriki kutoka sekta mbalimbali wamewasilisha uzoefu na suluhisho bunifu. Vijana walitoa maoni yao kuhusu matumizi bora ya teknolojia, wabunge walijadili sera za usalama wa kidijitali, na mashirika ya kiraia yamesisitiza haja ya ujumuishaji wa makundi yaliyo pembezoni.
Kauli za viongozi: Kusisitiza maadili ya kidijitali
Katika hotuba yake ya uzinduzi wa kikao cha Mabunge ya Kikanda, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, alitilia mkazo wajibu wa vijana katika matumizi ya mtandao. Alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuelekezwa kutumia mitandao kwa tija badala ya matumizi mabaya.
"Vijana ndio watumiaji wakubwa wa intaneti na wao ndio wanaoshinda zaidi mitandaoni... Kwa hiyo, ni sisi kutoa elimu kwa vijana wetu kuhakikisha wanatumia vizuri hii mitandao, wasifanye vitu ambavyo havifai na wasitumike vibaya,” alisema waziri Mahundi.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa Tech & Media Convergency (TMC), Edward Mbaga, alieleza kuwa haki za kidijitali ni msingi wa ushiriki wa kijamii katika zama za teknolojia.
"Haki za kidijitali ni msingi wa ushiriki jumuishi. Tunapaswa kuhakikisha kila mtu anapata fursa sawa, analindwa, na anaweza kushiriki salama na kwa uhuru katika mazingira ya kidijitali,” alisema Mbaga.
Vipaumbele vya majadiliano ya AfIGF 2025
Maeneo makuu yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na miundombinu ya kidijitali ya umma na utawala wa takwimu, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wote na kuongeza uwajibikaji.
Usalama wa mtandao na faragha ya watumiaji, hasa kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya mtandaoni.
Teknolojia mpya kama akili mnemba (AI), ambayo inabadilisha nyanja za elimu, afya na kazi, ikihitaji sera jumuishi na za kimaadili.
Upatikanaji wa mtandao hadi maeneo ya pembezoni, ili kufikia lengo la Afrika iliyounganishwa kwa mtandao wa gharama nafuu na lugha asilia.
Ushirikiano wa kidijitali, kwa kushirikisha serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kujenga mazingira bora ya TEHAMA.
AfIGF 2025 pia linatoa nafasi kwa vijana kupitia Youth IGF, ambako wanajifunza, kujadili na kuchangia ajenda za kidijitali. Aidha, AfriSIG (African School on Internet Governance) inaendelea kuwajengea uwezo viongozi chipukizi kutoka bara zima, kwa lengo la kuongeza sauti ya Afrika katika usimamizi wa mtandao duniani.
Tanzania mwenyeji: Nafasi ya kuonesha uongozi wa kidijitali
Kwa kuwa mwenyeji wa kongamano hili, Tanzania inaonesha dhamira yake ya kuimarisha mifumo ya kidijitali, kuhakikisha kila mtu anapata fursa ya kuunganishwa na teknolojia, na kusimama kama mfano wa kuigwa katika usimamizi wa mtandao. Ni nafasi ya kuongeza ushawishi wa kisera, kuvutia wawekezaji, na kujifunza kutoka kwa mataifa mengine.
Licha ya changamoto za kihistoria kama kuzimwa kwa mitandao na mitandao ya kijamii, kongamano hili limekuwa jukwaa la kuhamasisha umuhimu wa haki za kidijitali kama sehemu ya haki za binadamu, na kuonesha kuwa maadili ya kidijitali ni sehemu ya ajenda ya kitaifa.
Afrika ya kidijitali inawezekana
AfIGF 2025 ni zaidi ya mkutano – ni harakati ya pamoja ya kujenga Afrika ya kisasa na jumuishi kidijitali. Kupitia ushiriki mpana wa wadau, mazungumzo yenye tija, na dhamira ya kweli ya kushirikiana, bara hili linaweza kusimamia mwelekeo wake wa teknolojia na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.
Kwa Tanzania, huu ni wakati wa kuonesha uwezo wake wa kusimamia TEHAMA kwa mafanikio – na kujiweka mstari wa mbele kama kitovu cha sera na maendeleo ya kidijitali barani Afrika.