Afghanistan: Matumaini ya kuwapata manusura hai yanapungua
4 Septemba 2025Msemaji wa serikali ya Taliban, Hamdullah Fitrat amesema miili zaidi bado ipo chini ya vifusi, hivyo huenda idadi ya vifo ikaongezeka. Tetemeko hilo la ukubwa wa 6.0 lilitokea Jumapili usiku katika maeneo ya milimani mpakani mwa Pakistan. Duru zinasema hadi Alhamisi idadi ya waliofariki imefikia watu 1,469 na zaidi ya 3,700 wamejeruhiwa.
Fitrat amesema ufikiaji wa maeneo yaliyoathirika zaidi, hasa katika Jimbo la Kunar, umekwamishwa na maporomoko ya mawe yaliyosababishwa na mitetemeko ya baadae ambayo imeziba barabara nyembamba zilizochongwa kwenye milima.
Waziri wa Maendeleo Vijijini Mullah Mohamad Younus Akhundzada, katika taarifa yake amesema tetemeko hilo limeathiri maeneo mengi nchini humo na kuacha athari kubwa za watu na vitu. "Ni janga kubwa, halijaathiri Kunar pekee, lakini pia sehemu za Nooristan, Panjsher, na Laghman. Bado tunashughulika na hali hapa Kunar, na tetemeko la ardhi limeathiri pia baadhi ya maeneo ya jimbo la Nangarhar.”
Juhudi za uokozi zimekuwa za kusuasua tangu tetemeko hilo la Jumapili, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likionyesha wasiwasi wake juu ya afya za waathirika. WHO imetoa wito wa kiasi cha dola milioni nne za Marekani ili kunusuru maisha ya waathirika na kuongeza huduma za afya, ikiwemo dawa na vifaa vya tiba.
Mashirika ya misaada na Umoja wa Mataifa yametahadharisha kuhusiana na mgogoro juu ya mgogoro kufuatia tetemeko hilo kwenye taifa ambalo tayari linakabiliwa na majanga mengi ya kibinadamu, likiwemo umasikini uliokithiri, ukame na athari za vita vilivyoendelea kwa zaidi ya miongo minne.
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi, kupitia mtandao wa X alisema tetemeko hilo limeathiri zaidi ya watu 500,000 mashariki mwa Afghanistan.