AFD yaorodheshwa kuwa taasisi inayofuata itikadi kali
2 Mei 2025Shirika la ujasusi nchini Ujerumani limekitangaza chama cha mrengo mkali wa kulia, AfD, kama kundi la itikadi hali na kukitaja kama tishio kwa mustakabali wa demokrasia. Uamuzi huo uliotangazwa leo unafunguwa njia ya kuzipa idhini mamlaka zinazohusika na masuala ya usalama kufuatilia mienendo na shughuli za chama hicho kilichoshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Februari.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo la ujasusi wa ndani, BfV, imesema chama cha AfD kinaendekeza ubaguzi wa kimtazamo kwa watu wa Ujerumani na kuyabagua baadhi ya makundi katika jamii suala ambalo linakiuka misingi na sheria zilizoainishwa katika katiba ya Ujerumani.
Soma zaidi: AfD yaorodheshwa kuwa taasisi inayofuata itikadi kali
BfV ndiyo taasisi iliyopewa jukumu la kulinda misingi ya kikatiba nchini Ujerumani, ambayo miongoni mwa majukumu yake ni kuchunguza na kukusanya taarifa za viashiria vya kuvunjwa kwa misingi hiyo ndani ya nchi.
AFD imekuwa na tabia ya kuwatazama watu kwa asili na historia zao.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Nancy Faeser, amesema chama hicho kimekuwa na tabia ya kuwatazama wananchi wa taifa zima la Ujerumani katika kioo cha asili na historia zao, na kuwabagua na kuwaona wengine kama watu wa tabaka la pili.
Waziri huyo anayemaliza muda wake baadaye mwezi huu, ameongoza na hapa namnukuu: "Chama cha AfD kinawakilisha itikadi na mawazo ya kikabila na ubaguzi wa makundi ya watu na wananchi kwa ujumla kwa misingi ya kule walikotoka na kuwaona kama watu wa tabaka la chini." Mwisho wa kumnukuu.
Faeser ameongeza kuwa ubaguzi wa chama hicho umekuwa ukishuhudiwa kupitia kauli zao za kibaguzi ambazo zimekuwa zikiwalenga zaidi wahamiaji na hasa Waislamu.
Kwa miaka ya hivi karibuni, chama cha AfD kimekuwa kama kichocheo katika mizozo na mabishano ya hapa na pale na wanachama wake wamekuwa wakibeza na kupuuzia athari kubwa zilizosababishwa na utalawa wa Wanazi na kuendelea kumpongeza Rais wa Urusi Vladimiri Putin na sera zake.
Elons Mask alikipongzea chama hicho
Mapema mwaka huu bilionea wa Marekani na ambaye mwenyewe ni mfuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia, Elon Musk, alisikika akikipongeza chama hicho, akikitaja kama chama pekee kinachoweza kuinusuru Ujerumani kwa wakati huu.
Katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Februari mwaka huu, chama hicho kilijinyakulia nafasi ya pili kwa kupata asilimia 21% kikitanguliwa tu na muungano wa vyama ndugu vya CDU/CSUulioongozwa na kansela mtarajiwa Friedrich Merz, uliopata asilimia 28.5 ya kura.
Hata kura za maoni za hivi karibuni zinaonesha kwamba chama chaAfDkimeendelea kuongeza ushawishi wake miongoni mwa Wajerumani, huku tafiti kadhaa zikionesha kuwa kilikuwa mbele ya vyama vya mrengo wa wastani.
Hata hivyo, hakitakuwa sehemu ya serikali ya mseto itakayoanza kazi baadaye mwezi huu, kwani vyama vikuu na vikongwe vya kisiasa vimekataa kufanya kazi na chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia.