AFC/M23: Lazima wafungwa waachiwe kabla ya mazungumzo
29 Julai 2025Lakini chama cha UDPS cha rais Felix Tshisekedi kinasema baadhi ya wafungwa hao washirika waasi, ni raia wa Rwanda. Miongoni mwa wafungwa 700 ambao waasi wa AFC/M23 wanataka waachiwe ni Ruttens Baseane Nangaa, mshauri wa kimkakati wa kiongozi wa muungano huo wa waasi Corneille Nangaa, ambaye pia wanao uhusiano wa karibu wa damu.
Mwingine ni Eric Nkuba Shebandu ambaye pia ni mshirika wa muda mrefu wa Corneille aliyetiwa mbaroni Januari mwaka jana mjini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa hadi Kongo. Wafungwa hao wawili wanaopewa uzito wa juu na AFC/M23 wanashikiliwa katika gereza la kijeshi la Ndolo mjini Kinshasa, wakikabiliwa na hukumu ya kifo.
Mapigano yamezuka tena mashariki mwa Kongo
Chanzo kilicho karibu na mazungumzo ya Doha kinaeleza kuwa kuachiliwa kwao ni miongoni mwa masharti yaliyowasilishwa na AFC-M23 kwa wapatanishi. Kwa upande wake serikali ya Kinshasa imesema bayana kuwa kamwe masharti hayo ya waasi hayatokubaliwa. Licha ya msimamo huo lakini, Adolphe Amisi Makutano ambaye ni mbunge wa chama cha UDPS, anasema bado kuna uwezekano wa kufikia makubaliano.
"Serikali ya Kinshasa imetulia na inajua namna ya kukabiliana na suala hili na kulipatia suluhisho. Sisi ni dola, waasi ni wahalifu wanaopaswa kutendewa kama wahalifu. Kuhusu mazungumzo, naamini daima kutakuwa na suluhisho, hata kama hawatapata kile wanachokitafuta," alisema Adolphe Amisi Makutano
Mazungumzo ya Doha yatiliwa shaka
Mbunge huyo wa chama cha Rais Tshisekedi anawapa moyo raia wa Kongo wanaoishi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi, akisema hatimaye Kongo itarudi kuwa nchi moja isiyogawanyika.
Wachambuzi wengine lakini wanatilia shaka ikiwa mazungumzo ya Doha yataleta suluhu. Profesa Bob Kabamba wa Chuo Kikuu cha Liege nchini Ubelgiji, anaamini itakuwa vigumu kwa serikali ya Kinshasa kuwapata wafungwa wote wanaodaiwa na waasi wa AFC/M23.
Qatar yawasilisha mswada wa amani kwa Kongo, waasi wa M23
"Siioni serikali ya Kongo ikilazimika kutekeleza masharti ambayo haiwajibiki nayo kisheria. Orodha ya watu 700 ni ya wafungwa ambao hawajasajiliwa rasmi. Wapo watu waliokamatwa bila hati ya kukamatwa, bila sababu inayojulikana, na hawajulikani walipo. Wengine wametoweka. Haya yote yanachangia kuufanya mchakato wa Doha kuwa mgumu kutekelezeka."
Zaidi ya wiki moja baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya msingi ya Doha, hakuna mabadiliko yaliyoshuhudiwa katika maeneo ya vita ambapo mapigano yanaendelea, huku pande zote zikilaumiana kwa kukiuka makubaliano waliyoyatia sahihi.