Abiy asema Ethiopia haitafuti mzozo na Eritrea
20 Machi 2025Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameandika kwenye ukurasa wa mtandao wa X kuwa nchi yake haina dhamira ya kujiingiza kwenye mzozo na Eritrea kwa lengo la Ethiopia kujipatia nafasi ya kuifikia Bahari ya Shamu.
Eritrea inaituhumu Ethiopia, taifa lisilo na bandari kuwa inaimezea mate bandari yake ya Assab katika juhudi za serikali mjini Addis Abbaba kuifikia bahari ya Shamu.
Soma pia: Kwa nini Ethiopia na Eritrea ziko ukingoni kuingia vitani?
Hapo jana Eritrea iliitaka jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Ethiopia "iheshimu uhuru na hadhi ya mipaka ya Eritrea".
Nchi hiyo pia imekanusha taarifa za kujiandaa kwa vita baada ya asasi moja ya kiraia kusema serikali mjini Asmara imeamuru "kuandikishwa kwa wingi jeshini" kwa raia walio chini ya umri wa miaka 60.
Wiki iliyopita chanzo kimoja cha kijeshi kilisema misafara iliyobeba shehena ya silaha ilikuwa inaelekeamkoa wa kaskazini mwa Ethiopia wa Afar, unaopakana na Eritrea.