30 wafa, 90 wajeruhiwa ajali ya treni Pakistan
7 Agosti 2023Mamlaka nchini humo zimesema shughuli za uokoaji zimekamilika na majeruhi wamepelekwa hospitalini.
Afisa mkuu wa shirika la reli nchini humo, Mahmoodur Rehman Lakho, amesema mabehewa 10 ya treni iliyokuwa ikitoka Karachi ikielekea Rawalpindi yaliacha njia na mengine kupinduka, na hivyo kusababisha maafa makubwa miongoni mwa abiria wakiwemo wanawake, watoto na wazee.
Soma zaidi:Watu 70 wafariki Pakistan kufuatia moto kwenye treni
Akiwa katika mkutano wa kisiasa huko Punjab, Waziri Mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif amesema amehuzunishwa na ajali hiyo na kusoma dua kwa waliofariki dunia pamoja na majeruhi.
Ajali za treni hutokea mara kwa mara katika nchi hiyo masikini kutokana na viwango duni vya usalama, ukarabati mbovu wa reli, mifumo elekezi na ya mawasiliano ambayo ni ya tangu enzi za ukoloni.